Jumapili ya Huruma ya Mungu: Kristo Yesu ni Uso wa huruma ya Mungu; muhtasari wa imani ya Kanisa. Jumapili ya Huruma ya Mungu: Kristo Yesu ni Uso wa huruma ya Mungu; muhtasari wa imani ya Kanisa. 

Jumapili ya Huruma ya Mungu 2019: Yesu Uso wa Huruma ya Mungu!

Mtakatifu Toma kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, akatubu, akaongoza na kuwa shuhuda wa Fumbo la Pasaka. Fumbo la Huruma ya Mungu limekaziwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II na Papa Francisko akaliwekea mikakati ya kichungaji, kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa naye kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ibada ya Upatanisho ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia huruma, upendo na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, waamini wanakirimiwa tena maisha mapya baada ya kuanguka dhambini na kupoteza ile neema ya utakaso waliyopokea wakati walipokuwa wanapokea Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya upatanisho, Kanisa linazidi kukua na kupanuka, kwa kumfuasa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa. Huu ni mwaliko wa kujitakasa kwa kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuzungumza kutoka katika undani wa maisha ya watu, ili kweli wakleri waendelee kuwa ni vyombo vya huruma na upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Katika maisha na utume wa kipadre, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza! Mtakatifu Toma kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, akatubu, akaongoza na kuwa Shahidi wa Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Fumbo la Huruma ya Mungu limekaziwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Francisko akaliwekea mikakati ya kichungaji, kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji!

Inashtusha sana kuona chama cha upinzani chenye wafuasi wengi na kilichokuwa karibu kunyakua dola, ghafla kinayumba na kuwa hatarini kusambatika. Dalili za maanguko ya chama zilianza kujitokea pale kada mmoja wachama aliyekuwa mtaalamu wa sheria na aliyeaminishwa madaraka makubwa katika chama, alipomtuhumu mwenyekiti wake mambo ya uwongo, na alidiriki hata kujibizana naye vibaya sana hadharani. Hakuishia hapo tu, bali alienda kumsaliti kwa Wakuu wa dola na kwa Viongozi wakuu wa dini. Akapokea kiburungutu cha hela ili wamshughulikie mwenyekiti wake. Wakaagizwa askari kumkamata mwenyekiti huyo na kumsukuma ndani akajibu mashtaka yasiyo na msingi. Wanachama wengi wamemtoroka mwenyekti, na wachache waliobaki wamejifungia kwenye ofisi ya chama wamejawa na uchungu na msongo mkali wa mawazo na hawajui hatima yao. Ila wanao uhakika kwamba sasa chama chao kimeishia. Hii ndiyo hali halisi waliyokuwa nayo mitume wachache siku ile ya Jumapili jioni ya Pasaka ya kwanza baada ya kukaa chumbani kuanzia Ijumaa mchana alipokufa Bwana Yesu Msalabani.

Mle chumbani walikusanyika wafuasi kumi tu, kwa sababu kati ya wanafunzi kumi na wawili alikosekana Yuda (aliyeasi) na Tomaso ambaye haikujulikana alikuwa wapi: “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi… Walakini mmoja wa wale Thenashara, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu.” (Yoh 20:19). Kumbe wakiwa wamejaa wasiwasi na msongo wa mawazo, Yesu alikuja na kusimama katikati yao na kuwasalimia: “Amani iwe kwenu.” (Yoh 20:19). Kama vile angewaambia: “Jamani kateni pumzi” au “Shusheni pumzi” au “Tulieni”. Hilo lilikuwa amkio la Wayahudi hata kabla ya Yesu: “Shalom aleichem – au – “assalamu alaikum” na anayeamkiwa anajibu “aleichem shalom” (Iwe nawe pia). Sasa hivi wanaamkiana kwa kifupi “Shalom” yaani salamu au amani. Wakatoliki tunapeana amani kabla ya kwenda kupokea komunio Takatifu kwa kupeana mikono na tunatakiana “Amani kwako!”

Kwa vyovyote amkio la Yesu liliwashtua Mitume na kuwapa mashaka. Lakini kukutana na kumwona Yesu mfufuka kuliwaondolea wasiwasi mkubwa na msongo wa mawazo waliokuwa nao na wakapata amani mioyoni na akilini. Aliporudi Tomaso wakamshirikisha furaha yao na kumwambia kuwa Yesu ni mzima na wamemwona. Hapo hata ungekuwa wewe ndiye Tomaso ungepata taabu sana kukubali. Tomaso akafikiri kwa haraka haraka na kuona kwamba sasa kama ni utani na dharau kwa Yesu imepita mipaka. Ni sawa na kupiga maiti.

Hivi unaweza kupata picha jinsi ambavyo Tomaso angeweza kuwajibu Mitume wenzake: “Ninyi wenyewe mlishuhudia jinsi mwili wake ulivyoshushwa kutoka msalabani. Alikuwa hapumui kabisa. Halafu mishipa ya mwili wake haikuwa na damu kwani yote ilikuwa imechuruzika. Mliona wenyewe jinsi askari alivyoutoboa moyo wake kwa mkuki. Ndugu zangu ni dhahiri kwamba msiba wa Yesu ulikuwa mzito sana, lakini yabidi pia mkubaliane nami kwamba msiba huo umewachanganya akili! Basi kwa kujiridhisha kidogo, Tomaso akataka kuthibitishiwa kwa hoja zenye mshiko, ndipo atawasadiki vinginevyo hakitaeleweka kitu. Hivi akatoa msimamo wake kwamba: “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkononi wangu katika ubavu wae, mimi sisadiki hata kidogo.” (Yoh 20:25).

Kwa hiyo sasa hali unayoweza kuiona hapa ni ya mgawanyo mwingine katika jumuiya ya mitume iliyolala kwenye msingi wa imani. Kwa upande mmoja, wako mitume kumi wenye imani ya ufufuko na wanaojua kabisa kwamba Yesu ni mzima. Kwa upande mwingine yuko Tomaso mtume wa kumi na moja bado hakijaeleweka kitu. Yeye amekataa katakata kusadiki yaani hana imani. Ameonesha msimamo wake hadi mwisho kwamba anahitaji kupata vigezo na hoja zenye mshiko. Maana yake, anaona ni upuuzi kuwa na imani isiyo na hoja na vigezo vyenye mshiko. Kumbe Tomaso angekushtuka walau kidogo tu na kuwaangalia vizuri mitume wenzake angegundua jinsi walivyobadilika ghafla kutoka pale alipowaacha. Kwamba aliwaacha wakiwa na uchungu mkali uliochanganyika na msongo wa mawazo juu ya kuondokewa na Bwana lakini amewakuta wametulia na wana amani na furaha ya pekee. Wakati yeye bado anaendelea kuteseka na wasiwasi na msongo wa mawazo.

Ndugu zangu mgawanyiko huu katika kundi hili moja la Mitume juu ya imani, unaweza kutokea katika familia au jumuiya yoyote ile hata taifa. Huo ni mgawanyiko kati ya wale ambao imani (itikadi) na hoja (vigezo) zimeoanishwa pamoja au ziko sawa, halafu kuna mgongano na wale ambao imani (itikadi) na hoja (vigezo) havijaoana kabisa yaani vimetengana na vinakinzana. Mgongano na sintofahamu hiyo inaweza kutokea hata leo katika jumuiya ya Kikristu. Unapowaona wale wenye imani na hoja zilizooana vizuri wanapojaribu kuwaelewesha wenye imani gongana wanavyokataliwa na kwa hoja nzito kutoka kwa Tomaso mambo leo. Tomaso wa leo anaweza kukosa imani juu ya sala na kukupatia hoja: “Ukinilazimisha mimi siwezi kwenda Misa, kwani kuna nini cha pekee chenye mshiko kwenye Misa?” Maana yake Tomaso huyu atakuwa tu na imani kanisani endapo atafanyiwa kitu chenye mshiko na Bwana Yesu.

Ni dhahiri kwamba Tomaso wa awali na huyu wa sasa ni mtu anayejidhani kuwa ni mkuu, hodari, mwenye nguvu. Kwake mtu huyu imani ni danganya toto. Kwa sababu yeye anataka kupata vigezo na hoja za kisayansi zinazomthibitisha Mungu. Tomaso anashindwa kutambua kuwa haitakiwa kuwa na ukinzani na mgongani kati ya imani na sayansi (elimu), au kati ya imani na hoja.  Inabidi ajifunze kwamba imani na sayansi vinatakiwa vioane na viwe kitu kimoja. Leo baada ya kupita siku nane, Yesu anafika tena kwa namna ileile. Anawatakia amani Mitume na anamthibitishia Tomaso kwa vigezo vya mantiki ya kisayansi anavyovitaka anamwita na kumwambia: “Tomaso, lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” (Yoh 20:27) Tomaso akamjibu akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yoh 20:28). Sasa imani na hoja zimeunganika katika Tomaso, imani na sayansi zimeoanishwa kwa nguvu. na sasa Tomaso amemwona Yesu.

Hali ya kutegemea sayansi (hoja na mantiki) peke yake ndivyo vilivyofunga akili ya Tomaso asiweze kuona ufufuko wa Yesu. Umajikuu na majivuno yake, hasa ya kutaka kuwa mtawala wa maisha yake mwenyewe, wakutaka kuongoza maisha kivyakevyake badala ya kuruhusu imani kuungana au kuoana na hoja ndiyo yaliyomfanya alipoteze juma nzima bure. Yaani kwa wiki moja nzima alimfungia Yesu nje ya maisha yake. Kumbe inatakiwa kuruhusu sayansi (hoja na mantiki) kuungana na kufanya kazi pamoja na imani kwa Mungu. Sayansi na maendeleo bila imani kwa Mungu haitakuacha bila machungu ya kukukatisha tamaa. Bali ukiunganisha na imani kwa Mungu hapo hupotezi chochote bali unapata zaidi na utakuwa na furaha inayodumu. Tomaso alipomwona Yesu akajitoa na kusadiki. Halafu akampokea Yesu.

Leo Tomaso anatufundisha kwamba ukimwaminia na kumsadiki Yesu, utakuwa na furaha ambayo hutaipata popote wala kutoka kwa yeyote yule. Kinyume chake ukikosa furaha ujue wewe upo mbali sana na Mungu. Sisi hatutaki kupoteza muda kama Tomaso aliyepotea kwa wiki moja bila kujulikana alikokuwa. Tumepata fursa ya pekee ya kuwa watoto. “Kila mtu aaminiye kwamba Yesu ni Kristo amezaliwa na Mungu.” (1 Yoh 5:1) Ndugu zangu tusipoteze bure maisha yetu bali tuchangamkie fursa ya kuwa waana wa Mungu. Kama hujakutana na Yesu, basi jaribu kuliviringisha jiwe na utamkuta. Iruhusu imani yako kuwa na mtandano na akili au hoja zako. Amini, jitoe, sadiki utamwona tu Yesu Mfufuka.

27 April 2019, 12:22