Tafuta

Vatican News
Kardinali Polycarp Pengo amewataka Masista Wakarmeli kuwekeza katika: Elimu, malezi na makuzi fungamani kwa watoto na vijana nchini Tanzania! Changamoto zipo! Kardinali Polycarp Pengo amewataka Masista Wakarmeli kuwekeza katika: Elimu, malezi na makuzi fungamani kwa watoto na vijana nchini Tanzania! Changamoto zipo!  (Vatican Media)

Kardinali Pengo: Wakarmeli wekezeni katika elimu, malezi & makuzi

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 25 Machi 2019 amebariki na kufungua nyumba mpya ya Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Tanzania; akaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule ya Sekondari Mapinga pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia wa kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, umeandikwa katika mfumo wa barua kwa vijana. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ndiye matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria msichana kutoka Nazareti kwa kukubali kwake kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake, amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa wale wote wanaothubutu kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao!

Bikira Maria ni msichana aliyekumbatia ahadi kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu na kuitikia kwa “Ndiyo” tayari kuutekeleza katika maisha yake. Baba Mtakatifu anawauliza vijana ikiwa kama wako tayari kuthubutu katika maisha yao kama alivyofanya Bikira Maria? Hata Bikira Maria katika maisha na utume wake, alikumbana na changamoto za maisha, lakini hakukata tamaa, bali alimtegemea Mwenyezi Mungu. Itakumbukwa kwamba, Wosia huu wa kitume, ulitiwa sahihi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2019 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Kupashwa Habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu.

Ni katika muktadha wa matukio haya, ili kweli yaweze kuwa ni endelevu katika maisha na utume wa Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, nchini Tanzania, Kardinali Polycarp  Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 25 Machi 2019 amebariki na kufungua nyumba mpya ya watawa hawa; akaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule ya Sekondari Mapinga pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa! Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha huruma, upendo na mshikamano wa Mungu na biunadamu, kwa njia ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu na kwamba, watoto wa Kanisa wanahamasishwa kuendeleza mchakato wa ukombozi kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Hili ndilo lengo kuu la kuanzisha Jumuiya mpya ya Masista Wakarmeli huko Mapinga, Kimele, kwenye barabara iendayo Bagamoyo. Hawa ni watawa ambao sasa wanataka kukita utume wao katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima:kiroho na kimwili na hasa zaidi kwa njia ya elimu bora kwa wasichana, hasa wale wanaotoka kwenye familia maskini zaidi. Ndiyo maana Kardinali Polycarp Pengo ameweka jiwe la msingi, ili kazi iliyoanzishwa Parokiani Chang’ombe, Jimbo kuu la Dar es Salaam kunako mwaka 1984 kwa kufungua shule ya awali na baadaye shule ya msingi, iweze kukamilika kwa kuwa na shule ya Sekondari.

Mheshimiwa Sr. Vestina Tibenda, CMTBG, katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Masista wa Karmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, nchini Tanzania wamesoma alama za nyakati na kuitikia kilio cha wazazi na walezi wanaotamani kuona watoto wao wakipata malezi makini na elimu bora, ili waweze kuwa ni watakatifu, raia wema na waaminifu, tayari kushiriki katika ujenzi wa familia ya Mungu nchini Tanzania. Mradi huu mkubwa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2021, utakuwa na kidato cha kwanza hadi kidato cha sita!

Kardinali Pengo katika mahubiri yake alikazia kuhusu utayari wa Bikira Maria kukubali mpango wa Mungu na kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake! Amesema, hata Mtakatifu Yosefu, mtu wa haki, alipata taabu sana kukubaliana na mpango wa Mungu, lakini hatumaye, akakabidhiwa dhamana ya kuwa ni mlinzi wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa njia hii, Mtakatifu Yosefu, Baba mlishi wa Yesu, akaingia na kuambata mpango wa Mungu katika maisha yake.

Kardinali Pengo anakaza kusema, hii ndiyo changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi na Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, nchini Tanzania, kwa kuishi kati pamoja na watu wa Mungu, lakini zaidi wale walioko pembezoni mwa vipaumbele vya jamii kama inavyojionesha kwa sasa kwenye Kitongoji cha Kimele-Mapinga. Amewashukuru kwa namna ya pekee kabisa, Sr. Karatina Hilonga, Sr. Catherine Woisso, Sr. Devotha Tarimo pamoja na Sr. Sylvia Ernest kwa kuitikia “Ndiyo” yao kwa Mungu na viongozi wa Shirika, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, ili kwenda kuishi na kutoa huduma, kama ushuhuda wa uwepo wa Kristo Yesu, Neno wa Mungu kati ya waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume: “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, anawataka vijana wakishikwa na utume wa Mama Kanisa, washikamane, kwa kutambua kwamba, wao wanapaswa kuwa ni wadau wa kwanza. Waoneshe kipaji chao cha ubunifu; watumie vyema milango yao ya fahamu na hatimaye, wasimame kidete kupambana na changamoto mamboleo katika maisha yao. Utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, uwe ni fursa ya kuwapatia elimu na majiundo bora yanayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anasema, iwe ni nafasi ya kusikiliza na kusikilizwa; mahali pa kukutana na Mungu aliye hai katika Neno, Sakramenti za Kanisa na ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Lengo ni kuwawezesha vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, upendo, mshikamano na maridhiano kati ya watu! Taasisi za elimu ziwe ni mahali pa kuwafunda vijana utamaduni wa kukutana sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Kardinali Pengo
10 April 2019, 07:28