Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu yalipotokea Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda, tarehe 7 Aprili 1994: Ukweli na Upatanisho! Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu yalipotokea Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda, tarehe 7 Aprili 1994: Ukweli na Upatanisho! 

Jubilei ya Miaka 25 ya Mauaji ya Kimbari Rwanda: Upatanisho!

Takwimu zinaonesha kwamba, wahudumu wa Injili wapatao 248 waliuwawa kikatili. Kati yao kuna: Maaskofu 3, Mapadre 103, Watawa wa kiume 47 na watawa wa kike 65 na waamini walei waliojiweka wakfu walikuwa ni 30. Katika matukio haya, Kanisa likajiuliza swali msingi, Je, juhudi zote za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, zilipotelea wapi?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbu kumbu ya miaka 25 tangu mauaji ya kimbari yalipotokea nchini Rwanda kunako tarehe 7 Aprili, 1994 na kupelekea watu laki nane kupoteza maisha yao. Wananchi wa Rwanda wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, sasa wanajifunga kibwebwe kwa ajili ya ujenzi wa misingi ya haki, amani upendo, umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa; utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Hii Ni changamoto ya kuendeleza mchakato wa majadiliano yanayopania kuponya madonda ya chuki na uhasama, ili kuanza hija ya ujenzi wa Rwanda mpya unaosimikwa katika dhana ya haki, amani na maridhiano, ukabila, ukiwekwa pembeni kabisa! Ukweli na upatanisho ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Rwanda!

Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda, yaliacha kurasa chungu ndani na nje ya Rwanda yenyewe! Wahanga wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda wanaendelea kutoa changamoto ya kuangalia athari za matendo haya katika jamii. Kumbu kumbu ya kweli inayoweza kufanywa ni kuhakikisha kwamba, mauaji kama haya hayatendeki tena. Rais Paul Kagame, Jumapili tarehe 7 Aprili 2019, amewasha mwenge wa kumbukumbu katika  Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari mjini Kigali ambako inaaminika kwamba, zaidi ya waathirika 250,000 walizikwa mahali hapo. Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda yaligusa na kutikisa maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha Karne ya XX, kiasi cha kulitumbukiza Kanisa katika kashfa ya mauaji ya kimbari ingawa Kanisa pia lilipa gharama kubwa katika tukio hili!

Takwimu zinaonesha kwamba, wahudumu wa Injili wapatao 248 waliuwawa kikatili. Kati yao kuna: Maaskofu 3, Mapadre 103, Watawa wa kiume 47 na watawa wa kike 65 na waamini walei waliojiweka wakfu walikuwa ni 30. Katika matukio haya ya kusikitisha na kutia simanzi, Kanisa likajiuliza swali msingi, Je, juhudi zote za uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, zilipotelea wapi? Kwa sasa familia ya Mungu nchini Rwanda imegundua kwamba, badala ya kujikita katika ushabiki wa mashujaa wa Rwanda, kuna haja ya kukimbilia na kuambata huruma, upendo, msamaha, ukweli na upatanisho! Ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu neema na ushuhuda wa imani, pale ambapo ukweli wote kuhusu Mauaji ya Kimbari utakapofahamika, bila shaka, Kanisa Katoliki nchini Rwanda, itabidi kuandika ukurasa mpya wa watakatifu na mashuhuda wa Injili, waliojisadaka kwa ajili ya kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo wakati huo!

Kati yao, kwa namna ya pekee kabisa anakumbukwa Mama Fèlicitas Niyitegeka, Mhutu kwa asili, aliyeuwawa kikatili kwa sababu tu alitoa hifadhi kwa Watutsi, ambao walionekana kuwa ni adui kwa wakati ule! Kwa Mama huyu, wote walikuwa ni ndugu zake na wala hakuona ukabila ni kitu cha kung’ang’ania sana! Kuna orodha ndefu ya watu wenye haki, waliojisadaka ili kuokoa maisha ya ndugu zao, waliokuwa hatarini kupoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kimbari! Familia ya Bwana na Bibi Cyprian na Daphrose Rugamba, viongozi wa Jumuiya ya Emmanuel, waliouwawa kikatili tarehe 7 Aprili 1994, tayari wako kwenye mchakato wa kutangazwa wenyeheri na hatimaye, watakatifu kutokana na ushuhuda wa kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Kwa hakika, katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda, dhambi iliongezeka maradufu, lakini pengine, hata neema iliweza kufunika zaidi!

Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kudumisha amani, umoja na mshikamano ambavyo ni tunu walizoachiwa na waasisi wa Taifa. Ameyasema hayo Jumapili, Aprili 7, 2019 katika kumbukumbu ya miaka 25 ya Mauaji ya Kimbari iliyofanyika katika jiji la Kigali nchini Rwanda. Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika kumbukumbu hizo, amewasisitiza Watanzania kudumisha amani na utulivu. Awali, Waziri Mkuu alijumuika na viongozi kutoka nchi mbalimbali kutoa heshima kwenye eneo la kumbukumbu ya mauaji hayo la Gisozi lililopo jijini Kigali. Baada ya kutoa heshima kwenye eneo la kumbukumbu za mauaji hayo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alitoa maelezo ya kina kuhusu mauaji hayo yaliyotokea Rwanda 1994. Viongozi wengine waliohudhuria kumbukumbu hizo ni pamoja na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Rais Mstaafu wa Nigeria, Ulusegun Obasanjo.

Mauaji ya Kimbari Rwanda
08 April 2019, 09:22