Baraza la Maaskofu Katoliki Nchi za Scandinavia: Kongamano III la Familia Kitaifa: 2020: Kauli mbiu "Upendo ndani ya familia, Nguvu ya Kanisa" Baraza la Maaskofu Katoliki Nchi za Scandinavia: Kongamano III la Familia Kitaifa: 2020: Kauli mbiu "Upendo ndani ya familia, Nguvu ya Kanisa" 

Kongamano la Familia Scandinavia 2020: Familia nguvu ya familia!

Baraza la Maaskofu Katoliki katika Nchi za Scandinavia, limeanza maandalizi ya Kongamano la Tatu la Familia Kitaifa litakaloadhimishwa kuanzia tarehe 21-24 Mei, 2020. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Upendo ndani ya familia, nguvu ya Kanisa”. Kongamano hili linapania kujenga na kuimarisha tunu msingi za ndoa na familia; umoja, upendo na mshikamano kati ya waamini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ni dira na mwongozo wa maisha ya ndoa na familia. Ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Hili ni jibu kwa familia moja moja kadiri ya hali na mazingira yake. Wosia huu unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Unakazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki katika Nchi za Scandinavia, limeanza maandalizi ya Kongamano la Tatu la Familia Kitaifa litakaloadhimishwa kuanzia tarehe 21-24 Mei, 2020. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Upendo ndani ya familia, nguvu ya Kanisa”. Familia ya Mungu katika nchi za Scandinavia litapenda kuyaangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini kutokana na ongezeko la idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki. Hii inatokana pia na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama, hifadhi na maisha bora zaidi kupata fursa ya kuonja ukarimu wa wananchi wa Scandinavia! Kundi hili linachangia amana na utajiri wa Kanisa katika eneo hili.

Katika kipindi cha Mwaka 2018, Masalia ya wazazi wa Mtakatifu Theresa wa Lisieux yalitembezwa kwenye nchi za Scandinavia. Hili limekuwa ni tukio la uekumene wa sala na ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama anavyokaza kusema Kardinali Anders Arborelius, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Stockholm, nchini Sweden. Maadhimisho haya ya kitaifa yanasaidia kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa waamini. Maaskofu wanasema, matukio yote haya yanachangia pia kuhamasisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa!

Scandinavia: Familia
09 April 2019, 09:38