Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetangaza Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia, matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetangaza Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia, matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Mwaka wa Familia 2019

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC limetangaza Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia: matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji, Kumbu kumbu ya Miaka 25 ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Bara la Afrika; Miaka 25 ya tangu Umoja wa Mataifa kutangaza Siku ya Familia; Miaka 50 Halmashauri Walei Tanzania na Miaka 50 ya Chama cha Wanafunzi Wakatoliki.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. – Dar es Salaam.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetangaza kwamba, Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. Haya yamo kwenye Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Familia Kanisa la Nyumbani na ni shule ya imani na maadili. Maaskofu wanakazia kwa namna ya pekee familia kama msingi wa jamii ya binadamu kama inavyofafanuliwa na Mapokeo ya Kanisa. Maaskofu wanadadavua kuhusu dhana ya familia mintarafu Maandiko Matakatifu: Ukuu na Utakatifu wa Ndoa kadiri ya Agano Jipya.

Maaskofu wanakiri kwamba, familia ni shule ya imani na maadili inayofumbatwa katika maisha ya: Sala, Sakramenti za Kanisa na Liturujia; mambo msingi yanayoiwezesha Familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa makuzi na elimu makini kwa watoto! Familia ya Kikristo ni kituo cha maendeleo jamii na endelevu na mwishoni, Maaskofu katika ujumbe wa Kwaresima wanahimiza kuhusu Amri kuu ya Upendo, elimu ya dini; kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, Bikira Maria ni Malkia wa familia! Mwishoni, wanahitimisha kwa Sala kwa ajili ya kuombea familia bora na imara! 

UTANGULIZI: 1.1. Ujumbe wa Kwaresima 2019

Kama ilivyo ada kila mwaka, sisi Maaskofu Katoliki hutoa ujumbe mahsusi katika kipindi cha Kwaresima. Kila ujumbe huwa na dhamira maalum ya kuzingatia, ili katika kujitafakari na kuamsha upya maisha yetu ya Imani Katoliki na Maadili yake, tutambue zaidi na tukiri kwa dhati jinsi hali yetu ilivyo mbele ya Mungu ambaye ndiye chanzo cha utakatifu, na sisi kama wadhambi tulio safarini kuelekea huo utakatifu. Hivyo basi, kwa mwaka huu wa 2019 baada ya kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania mwaka jana 2018, tumeona ujumbe wa mwaka huu uzingatie dhamira inayohusu familia zetu. Dhamira hii ni “Familia kama Kanisa la Nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.  Kwa mwaka huu basi, tutafakari kwa namna gani hili lifanyike kwa kuzingatia kuwa Familia ya Kikristu ni Shule ya Imani Katoliki na Maadili yake.

SURA YA KWANZA: FAMILIA NI MSINGI WA JAMII YA KIBINADAMU: Mwaka 2019 kuwa Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei, Miaka 150 ya Uinjilishaji: Kwa kuzingatia hayo, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, pamoja na kuwa na dhamira hiyo, tumeuteua mwaka huu wa 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia, kama ishara na fursa ya kutafakari kwa undani zaidi matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania kama Familia ya Mungu. Uamuzi huo unajengwa juu ya sababu kuu nne za msingi kuhusu mwaka huu wa 2019.

Kwanza,ni miaka ishirini na mitano tangu ilipoazimishwa Sinodi ya kwanza ya Afrika, ambapo Kanisa lilikubaliana na mtazamo wa Kiafrika kuwa Kanisa ni Familia ya Mungu. Kwa hivyo, kiimani na kijamii binadamu anakiri kwamba familia ndiyo msingi wa jamii ya kibinadamu, na hivi kuijenga familia imara ni kuwa na jamii na Kanisa imara. Mababa wa Kanisa walielezea familia kuwa ni kiini cha kwanza na cha uhai wa jamii. Kama tunavyosoma kutoka Ecclesia in Africa, “Kwa kuwa Muumba wa vitu vyote ameanzisha ushirika wa mume na mke kama asili na msingi wa jamii ya kibinadamu, familia ni kiini cha kwanza cha uhai wa jamii.” (Ecclesia in Africa no. 85). Lakini Kwaresima hii tunaalikwa kutambua utume wa Familia kupitia wanafamilia ambao wengi wao ni walei, kama Mababa wa Kanisa wanavyotuambia kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Ni juu ya walei , kutokana na wito wao, kutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadri ya Mungu. Wanaishi ulimwenguni, yaani katika kazi zozote na shughuli za kidunia na katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kifamilia na ya kijamii, ambayo maisha yao yamefungamanishwa nayo.

Hapo wanaitwa na Mungu kusaidia kuutakatifuza ulimwengu, kama kutoka kwa ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, na hivyo wamdhihirishe Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo. Kwa hiyo yawahusu hao kwa namna ya pekee kuyatangaza na kuyapanga mambo yote ya kidunia, ambayo wamefungamana nayo, ili daima yafanyike na kukua kadri ya Kristo na kuwa kwa sifa ya Muumba na Mkombozi”(Lumen Gentium no. 31). Ili hiki kitelezeke inabidi familia iwe imara kiimani na kimaadili.

Pili, mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka ishirini na tano tangu pale Umoja wa Mataifa ulipotamka kuwa mwaka 1994 ni mwaka wa familia. Ni vema tukanukuu maneno ya msingi kuhusu nia ya Umoja wa Mataifa kwa kutenga mwaka huo kuwa ni mwaka wa familia. Umoja wa Mataifa ulitamka kwamba: “Familia inaunda kitengo cha msingi cha jamii na kwa hiyo inahitaji kuhakikishiwa uangalizi maalum. Hivyo basi, ulinzi mpana kabisa iwezekanavyo na msaada husika lazima vitolewe kwa familia zote ili nazo ziweze kuchukua majukumu yake ndani ya jamii, kutokana na matakwa ya  Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Tamko kuhusu Ustawi na Maendeleo ya Kijamii, na Mkataba wa Kufutilia Mbali Namna Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake

 Familia ni kitovu/kiini cha jamii (cell of the society) na ni lazima ijengeke katika hadhi ya binadamu kadri ya hulka ya binadamu iliyokusudiwa na Muumba, na sivyo inavyotafsiriwa bila kurejea kwa Mungu.Hii ndiyo italeta umaana wa familia kuwa msingi wa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anathibitisha kuwa ukweli unaojikita kwenye hulka upo kwenye jamii tayari kama wote tuko kwenye hulka aliyoitengeneza Mungu kama wote tunakubaliana naye. “The splendour of truth shines forth in all the works of the Creator and, in a special way, in man, created in the image and likeness of God (cf. Gen 1:26). Truth enlightens man's intelligence and shapes his freedom, leading him to know and love the Lord” (Veritatis Splendor page no.1).

Tatu, mwaka huu pia ni mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 tangu Halmashauri ya Walei ya Kanisa Katoliki ilipoanzishwa mwaka 1969. Kwa kuwa Halmashauri ya Walei katika ngazi zake zote inayo Kamati Ndogo inayohusika na Familia na Malezi, ni haki na ni vema Dhamira ya Familia ikawa ndiyo kiini mwafaka cha ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka huu tunapoidhimisha Jubilei hiyo. Na hasa kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya Waumini Wakatoliki ni walei wanaotakatifuza malimwengu kupitia maisha ya kitume katika familia zao, kama baba na mama, au babu na bibi, au mjomba na shangazi, au kaka na dada, shemeji au binamu. (Gaudium et Spes, no. 43 / Lumen Gentium, no. 31, 33).

Nne, mwaka huu pia ni adhmisho la mwaka wa Jubilei ya Dhahabu (Miaka 50) tangu chama cha kitume kinachowaunganisha wanafunzi wote Wakatoliki walioko sekondari; chama kinachojulikana kwa jina la Young Catholic Students, au kwa kifupi YCS. Kwa kuwa vijana bado wako chini ya wazazi wao na familia kwa upana wake kimalezi na kimakuzi, ni mwafaka basi tukatafakari kwa namna gani familia zinaweza kuwa kweli shule za Imani Katoliki na Maadili Yake kwa vijana hawa ambapo kwa sasa tunaona wengi. Idadi yao kitakwimu ni takribani zaidi ya milioni moja na laki saba kidato cha kwanza hadi cha sita. Hiki chama cha kitume katika jubilei yao ya miaka hamsini hatuna budi kama familia tutafakari upya tuwaongezee malezi gani ili wawe raia wema zaidi, na hatimaye waweze kuwa msingi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani na mbinguni.

Haja na Hoja ya Kuitafakari Familia: Leo hii, baada ya neema, baraka na mwanga zaidi wa Jubilei ya miaka 150 kuhusu nini maana ya kuwa Mkristo; maana na utume wa Familia ya kikristo ni vitu ambavyo haviwezi kuendelea kuchukuliwa juu juu tu. Ni lazima vitamkwe kwa dhati, vielezwe upya, vitetewe bila mashaka yoyote, na wanafamilia wenyewe watoe ushuhuda kwa jamii nini maana ya familia, kuwa ni Kanisa la nyumbani, na hivyo kuwa ni Shule ya imani na maadili. Sababu kuu ya kuwa na msimamo thabiti juu ya familia ni nini na ndoa na maana halisi ya ndoa, ni kwa sababu leo hii kuna dhana potofu na hata nadharia zisizo sahihi zinazolenga kuhalalisha vitendo vinavyopelekea kutenganishwa kwa ndoa na familia.

Kutenganisha huku kunatokana na dhana yenye maana potofu ya ndoa inayotolewa kwamba ndoa ni maridhiano ya wawili bila kufungamanishwa na jinsia zao. Hii ni maana potofu inayotetewa na baadhi ya jamii. Hii ni dhana iliyopotoka kihulka (unnatural), kiimani na kimaadili. Imani Katoliki na maadili yake inapingana kabisa na mtazamo wa namna hii, au hoja zinazoweza kutokana na mtazamo kama huo. Hii ni kwa sababu Muumba wa vitu vyote ameisimika taasisi ya familia kwa kuweka muungano wa kindoa kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ndiyo chanzo na msingi wa jumuiya ya kibinadamu, yaani familia. Kwa maana hiyo, familia ndiyo kiini cha kwanza cha uhai wa jamii.

Siku zote tutilie maanani kuwa katika mpango wake Mungu Muumba, mahali pa msingi ambamo watu wanajifunza kuwa watu ni kwenye familia. Hii inamaanisha kuwa ni katika familia ambamo kila mtoto kwanza anajifunza uwepo wa Mungu, kumpenda Mungu huyu, kutenda yanayoendana na huyu Mungu na mtoto huyu kutamani kuungana na Mungu huyu milele. Mtoto hupokea haya kutoka kwa wazazi wake na walezi wake, yaani kutoka kwenye familia. 

Tanzania: Mwaka wa Familia
09 April 2019, 08:13