Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea katika Waraka wake wa kichungaji linahimiza: amani, msamaha na upatanisho wa kitaifa! Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea katika Waraka wake wa kichungaji linahimiza: amani, msamaha na upatanisho wa kitaifa! 

Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea: Waraka wa Kichungaji: Amani

Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka, 2019 limetoa Waraka wa Kichungaji unaokazia umuhimu wa amani sanjari na upatanisho kati ya Mungu na binadamu, ili kuweza kujichotea baraka kutoka kwa Kristo Mfufuka. Waraka huu wa kichungaji unaongozwa na kauli mbiu “Amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwa wale waliokuwa karibu”. Efe. 2:17.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru. Amani inadumishwa kwa kulinda usalama wa raia na mali zao. Waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani: kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Injili ya amani ni muhtasari wa upendeleo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Uchafuzi wa mazingira unatishia amani na mafungamano ya kijamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2019, limetoa Waraka wa Kichungaji unaokazia umuhimu wa amani sanjari na upatanisho kati ya Mungu na binadamu, ili kuweza kujichotea baraka kutoka kwa Kristo Mfufuka.

Waraka huu wa kichungaji unaongozwa na kauli mbiu “Amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwa wale waliokuwa karibu”. (Efe. 2:17). Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea linapenda kuchukua fursa hii kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuiwezesha familia ya Mungu nchini humo, mwaka 2018 kuanza mchakato wa amani. Maaskofu wanawaombea wakimbizi na wahamiaji; wafungwa na wale wote waliotekwa nyara; waathirika wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, sanjari na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo.

Huu ni mwaliko wa kuangalia huruma na upendo wa Mungu na pale inapowezekana, kuanza mchakato wa kurejea tena nyumbani, kwani mambo yameanza "kunoga"! Maaskofu wanawaombea watu wa Mungu amani, usalama na utulivu, kwa wale wote ambao bado wanaishi katika hali tete na mazingira magumu. Demokrasia ya kweli, isaidie mchakato wa maboresho ya maisha, mahusiano na mafungamano ya kijamii. Maaskofu wanasema, wako tayari kushirikiana na Serikali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Eritrea.

Hii ni changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengano na badala yake, kuanza kujenga na kudumisha Injili ya haki, amani na matumaini kati ya watu! Vita nchini humo imekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya wananchi wasiokuwa na hatia na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Eritrea kujikuta linaendelea kuogelea katika mateso na nyanyaso kubwa huko ughaibuni. Umefika wakati wa kuhakikisha kwamba, tatizo na changamoto zinazowapelekea vijana wengi kuikimbia nchi yao zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha amani.

Maaskofu wanasema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu inayofumbata majadiliano katika ukweli na uwazi; amani inasimikwa katika: uhuru, haki na upendo. Maendeleo fungamani yanapaswa kuwaambata na kuwakumbatia wananchi wote wa Eritrea. Utajiri na rasilimali za nchi ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Familia ya Mungu nchini Eritrea, kama taifa, inapaswa kuanza mchakato wa: msamaha na upatanisho, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Eritrea mwishoni mwa Waraka wake wa kichungaji lina sema, maadhimisho ya Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya: imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Mfufuka. Ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Maaskofu Eritrea
30 April 2019, 10:46