Tafuta

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa, amewataka watanzania kusimama kidete: kutafuta, kulinda na kudumisha amani! Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki Iringa, amewataka watanzania kusimama kidete: kutafuta, kulinda na kudumisha amani! 

PASAKA YA BWANA 2019: Watanzania dumisheni amani!

Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika sherehe za Pasaka kwa mwaka 2019 linawahamasisha watanzania kutambua umuhimu wa kuwa na afya njema  kwani Kristo Mfufuka mwenyewe ndiye chanzo cha uzima kama alivyosema katika Injili  ya Yohane 10:10b kuwa ‘Mimi nalikuja ili wawe na uzima , kisha wawe nao tele’  Maaskofu wanashukuru na kutambua juhudi za Serikali ya Tanzania za  kuweka mfumo wa Bima ya Afya Jumuishi unaolenga kumfikia kila mwananchi. Hata hivyo imethibitika ya kuwa asilimia 28% ya watanzania, ambao ni sawa na Watanzania million 14.2 (kwa mujibu wa Taasisi ya Takwimu ya Taifa) ni maskini kabisa hivyo basi hawana kabisa uwezo wa kujilipia bima ili kugharamia huduma za afya.

Kwa mantiki hii, kwa ujumla kama Taifa, bado kuna jukumu la kuhakikisha wananchi hawa maskini  wanawezeshwa kupata huduma bora za afya sehemu mbali mbali za Tanzania. Maaskofu wanasema, wao kama sehemu ya jamii, wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa wanazihimiza kaya zote zenye uwezo wa kujiunga na bima ya afya kufanya hivyo, na pia wanaiomba serikali, iweke  mikakati madhubuti ya kifedha na utaratibu wa kuchangia na hatimaye, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa watanzania ambao hawana uwezo wa kujigharimia huduma za afya.

Wakati huo huo, Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tanzania, amewataka watanzania kusima kidete: kutafuta, kulinda na kudumisha amani. Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo!

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa katika mahubiri yake, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kufanya tathmini ya kina, kila mmoja kadiri ya nafasi, wajibu na dhamana yake katika jamii, ili kuangalia ni kwa jinsi gani ambavyo wanalinda, wanakuza na kudumisha amani nchini Tanzania. Kuchezea amani kunaweza kulitumbukiza taifa kwenye maafa makubwa na waathirika wakuu ni watoto na wanawake. Udini, ukabila, itikadi za kisiasa na umajimbo visiwe ni chanzo cha kuwakoroga na kuwavuruga watanzania katika mambo msingi.

Ikumbukwe kwamba, ulinzi na usalama wa Tanzania ni dhamana na wajibu wa kila mtanzania na wala si viongozi peke yao! Askofu Ngalalekumtwa amewasihi watanzania kuendelea kumsindikiza kwa njia ya sala na sadaka zao, Rais John Pombe Magufuli na Serikali ya awamu ya tano, ili aweze kuwa na afya njema, ujasiri, ari na moyo mkuu ili kuweza kupambana kiume na maovu pamoja na changamoto zinazojitokeza miongoni mwa watanzania, daima akisimamia na kutenda kwa haki na usawa kwa kuzingatia na kuheshimu utu wa binadamu. Rais Magufuli anaendelea kusimamia ukweli ambao umekuwa ni kauli mbiu yake, kwani “Msema kweli ni mpenzi wa Mungu” maneno ambayo amekuwa akiyatumia mara kwa mara anapopata nafasi ya kukukutana na kuzungumza na watanzania!

JUMAMOSI KUU: KESHA LA PASAKA: Historia ya wokovu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni Mwenyezi Mungu ambaye: aliwapenda, akawachagua, akawakomboa na kuwaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini, akawatakasa na kuwapatia Nchi ya ahadi. Hii ni historia endelevu inayotekelezwa katika maisha ya kila mwamini na Kanisa katika ujumla wake. Ukombozi huu unatekelezwa “Usiku wa manane”! Kesha la Pasaka ni Mama wa mikesha yote ya Liturujia ya Kanisa inayosheheni: Ibada ya Neno la Mungu, Liturujia ya Ubatizo na hatimaye, Liturujia ya Ekaristi Takatifu. Humu ndimo kunakoimbwa ile “Mbiu ya Pasaka” inayosimulia “Sifa ya Mshumaa wa Pasaka”, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Ni wakati kwa waamini kurudia tena ahadi zao za Ubatizo na Wakatekumeni kuzaliwa tena kwa maji na Roho Mtakatifu!

Mwaka huu 2019, Profesa Adelardus Kilangi, Mwanasheria mkuu wa Tanzania, ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipobatizwa kunako mwaka 1969 na kumwimbia Mungu “Mbiu ya Pasaka” kwenye Parokia ya Nyantakubwa, Jimbo Katoliki la Geita. Mara nyingi, Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza Wakristo kusherehea Siku kuu yao ya Ubatizo, kwani hii ni siku ambamo wamezaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu!

Maaskofu Tanzania
25 April 2019, 13:36