Tafuta

Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa amefafanua kuhusu alama za Liturujia ya kesha wa Pasaka katika historia ya Ukombozi. Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa amefafanua kuhusu alama za Liturujia ya kesha wa Pasaka katika historia ya Ukombozi. 

PASAKA YA BWANA 2019: Kesha la Pasaka Nchi Takatifu: Alama!

Historia ya wokovu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Aliwapenda, akawachagua, akawakomboa na kuwaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini, akawatakasa na kuwapatia Nchi ya ahadi. Hii ni historia endelevu inayotekelezwa katika maisha ya kila mwamini na Kanisa katika ujumla wake. Ukombozi huu unatekelezwa “Usiku wa manane”! Alama muhimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkesha wa Pasaka ni Mama ya mikesha yote ya Liturujia inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake. Mkesha huu wenye utajiri mkubwa wa maisha ya imani, umegawanyika katika sehemu kuu nne: Liturujia ya Mwanga inayopambwa kwa Mbiu ya Pasaka, kielelezo cha Kristo Mfufuka. Pili: Liturujia ya Neno la Mungu linalosimulia historia nzima ya wokovu tangu Agano la Kale hadi Agano Jipya. Tatu ni Liturujia ya Ubatizo, waamini wanarudia ahadi za Ubatizo kwa kumkataa Shetani, Ibilisi na mambo yake yote na Wakatekumeni wanabatizwa na kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu tayari kutangaza na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Nne ni Liturujia ya Ekaristi Takatifu na hapa waamini wanapata chakula cha njiani, baada ya kutafakari historia nzima ya ukombozi, tayari kwenda kuimwilisha kama ushuhuda wa imani tendaji!

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu katika Mkesha wa Pasaka, tarehe 20 Aprili 2019, ulioadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Kaburi Takatifu, mjini Yerusalemu amekazia kuhusu: historia ya wokovu na alama kuu ambazo zimejikita katika Liturujia ya Kesha la Pasaka. Historia ya wokovu ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Huyu ni Mungu ambaye aliwapenda, akawachagua watu wake, akawakomboa kutoka utumwani, akawaongoza jangwani kwa muda wa miaka arobaini, akawatakasa na hatimaye, akawapatia nchi iliyojaa maziwa na asali. Hii ni historia endelevu ya ukombozi ambayo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo anaendelea kuitekeleza katika maisha ya kila mwamini na Kanisa katika ujumla wake. Ukombozi huu unatekelezwa “Usiku wa manane”.

Huu ndio Usiku Mtakatifu unaoonesha ufunuo wa Mungu anayetenda kazi zake na kuwaokoa waja wake. Ni usiku wenye hofu na mashaka makubwa; upweke na hatari zinazomsonga mwanadamu. Huu ni usiku wa dhambi ambamo, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka anamkomboa mwanadamu na kumrejeshea tena ule utu wake wa kwanza uliokuwa umechakazwa kwa dhambi ya asili! Huu ndio usiku wa hofu, mashaka na hatari unaowaandama wakimbizi na wahamiaji; vijana wasiokuwa na kazi wala fursa za ajira. Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa anaendelea kufafanua kwamba, hili ni giza la kinzani za kidini, kisiasa, kijamii na kiuchumi; utengano, vita na ukosefu wa amani kutokana na misimamo mikali ya kidini, uchu wa mali na madaraka.

Hili ni giza linalochafua na kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu kutokana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Hili ni giza linalomsukumizia mwanadamu katika mauti, kutokana na ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, inayowageuza baadhi ya watu kulewa na hivyo kupoteza dira na mwelekeo sahihi wa mahusiano na mafungamano ya kijamii. Kumbe, Mshumaa wa Pasaka unaosimuliwa kwa Mbiu ya Pasaka ni kielelezo cha Kristo Yesu aliyefufuka kutoka kwa wafu. Huu ni wakati wa kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka kwa kuachana na matendo ya giza yanayochafua utu, heshima na haki msingi za binadamu! Waamini wawe ni nuru ya Mataifa na chumvi ya dunia!

Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, aliwaongoza Waisraeli ndani ya moto mfano wa nguzo, ili kuwapa nuru, ili wapate kusafiri mchana na usiku. Ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana, wala ile nguzo ya moto haikuondoka usiku, mbele ya hao watu. Mwenyezi Mungu ametumia alama ya moto kama dira na mwongozo kwa waja wake. Hiki pia ni kielelezo cha hukumu, maamuzi mazito na utakaso. Ni mwaliko wa kuambata mwanga na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka kwa kuchagua kutenda na kuambata mema; kwa kusimamia haki na kutenda haki.

Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa anasema, Maji ni alama ya Roho Mtakatifu anayewatakasa waja wake na kuzima kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yao. Maji ni uhai. Waamini waendelee kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho kwa njia ya Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na maisha adili! Maji ni alama ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowawezesha waamini kuzaliwa upya kwa Maji na Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika kuwa waana wa Mungu aliye hai! Mkate ni alama ya Sakramenti ya: Sadaka, Shukrani, Kumbu kumbu na Uwepo endelevu wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi.

Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni kifungo cha umoja wa Kanisa na Siku kuu inayomzunguka Mwanakondoo wa Mungu aliyeshinda dhambi na mauti. Waamini wanahamasishwa kushiriki mara kwa mara chakula hiki, ili kuganga na kuzima njaa ya maisha yao ya kiroho, kwa kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yao. Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, Chakula hiki, kiwe ni chemchemi ya haki, amani, usawa na maisha yanayosimikwa katika utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wawe ni Ekaristi, kwa kujimega bila ya kujibakiza kwa ajili ya mahitaji msingi ya jirani zao. Kristo Yesu ni Mkate wa maisha ya milele! Kaburi tupu, liwe ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti kwa kuzingatia mambo na vielelezo msingi vilivyooneshwa kwenye Liturujia ya Kanisa katika Mkesha wa Sherehe ya Pasaka!

Askofu mkuu Pizzaballa
21 April 2019, 15:26