Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury anawaalika Wakristo kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa waliokata tamaa! Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury anawaalika Wakristo kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa waliokata tamaa! 

PASAKA YA BWANA 2019: Askofu mkuu J. Welby: Injili ya Matumaini!

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa kwake mbinguni, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kustahirishwa tena kuitwa mwana wa Mungu! Fumbo la Pasaka linapyaisha imani, matumaini na mapendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa katika Kanuni ya Imani anasadiki na kufundisha kwamba, “Akasulubiwa pia kwa ajili yetu sisi; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akafa, akazikwa. Akafufuka siku ya tatu ilivyoandikwa”. Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa kwake mbinguni, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kustahirishwa tena kuitwa mwana wa Mungu!

Fumbo la Pasaka linapyaisha imani, matumaini na mapendo ya watoto wa Mungu, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani katika ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2019 anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, kutokana na ubinafsi, uchoyo na tabia ya watu kutojali sana kazi ya Uumbaji. Bado kuna vita inayoendelea kurindima sehemu mbali mbali za dunia.

Watu wanashuhudia vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kuhatarisha maisha, utu na haki msingi za binadamu. Bado kuna waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, wasiokubali kuambata maridhiano, umoja na mshikamano kwa kutambua na kuheshimu tofauti zao msingi kama sehemu ya utajiri mkubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Askofu mkuu Justin Welby anakaza kusema, matatizo na changamoto zote hizi, zinayafanya mataifa kuyumba sana na watu wengi kukabiliana na hali ngumu ya maisha.

Watu wamekata tamaa ya maisha, wanahitaji kutangaziwa na kushuhudiwa Injili ya matumaini mapya inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Katika kipindi hiki cha Pasaka, Kanisa linatangaza mbiu ya ufufuko wa Kristo Yesu kwa kusema, “Yesu amefufuka kweli kweli aleluiya, Ameshinda mauti, aleluiya”.  Huu ni ushindi unaodhihirisha utukufu wa Mwana mpendwa wa Mungu, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Fumbo la Pasaka ni kiini cha wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Injili ya matumaini inayotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka, inapaswa kufumbatwa katika imani na unyenyekevu mkuu. Hakuna sababu ya msingi ya kufanya wongofu wa shuruti, bali Habari Njema ya Wokovu imwilishwe katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu. Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Injili ya matumaini, ishuhudiwe kwa matendo ya huruma na mapendo:kiroho na kimwili; kwa kuheshimiana na kuthaminiana, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Kwa kutekeleza yote haya kwa dhati kabisa, Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, watakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya matumaini. Wakristo wainue nyoyo zao, wapaze sauti zao kwa nguvu, wafurahi na kushangilia, kwa kuwa Kristo Yesu amefufuka kweli kweli!

Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury na Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani katika ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2019 anawahimiza Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa pamoja na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kama ilivyokuwa kwa Maria Magdalena alipokutana na Kristo Mfufuka akaambiwa kwenda kuwatangazia ndugu zake kwamba, kweli amefufuka kutoka kwa wafu!

Huu ndio ujumbe wa matumaini ambao kila Mkristo anapaswa kuutangaza na kuushuhudia katika maisha yake kama chemchemi ya matumaini kwa wale wote waliokata tamaa! Askofu mkuu Justin Welby anawaombea watu wote wa Mungu, ili kweli amani na furaha iweze kuwaambata wote hata kama bado kuna matatizo na changamoto za maisha zinazoendelea kujitokeza kila kukicha!

Justin Welby: Matumaini
23 April 2019, 08:21