Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amewahimiza waamini wa Jimbo Katoliki Mpanda kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu mkuu Gervas Nyaisonga amewahimiza waamini wa Jimbo Katoliki Mpanda kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kanisa. 

Askofu mkuu mteule Nyaisonga: Wosia kwa Jimbo la Mpanda

Askofu mkuu mteule Nyaisonga amekazia umuhimu wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda kujenga na kudumisha: Umoja, Upendo na Mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kanisa. Wawe wepesi kuyaenzi yale mema yaliyotendwa na waasisi wa Jimbo Katoliki Mpanda lililoanzishwa kunako mwaka 2000, Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo chini ya Hayati Askofu Chikoti.

Na P. Wencesilaus Bamugasheki & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu anafundisha, anatangaza na kushuhudia kwa mamlaka yote Habari Njema ya Wokovu kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa ndiye aliyefufuka kwa wafu! Askofu anayo dhamana ya kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na mafumbo matakatifu, yanayowakirimia waamini chachu ya utakatifu pamoja na kuwaongoza watu wa Mungu kwa mfano wa Kristo Mchungaji mwema, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwa ufupi sifa kuu za Askofu kuwa ni: unyenyekevu na huduma; mambo yanayofafanuliwa vyema na Mtakatifu Paulo, Mtume katika Waraka wake kwa Tito, akionesha mambo msingi yanayopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Maaskofu, ili kukamilisha yale yanayopungua katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuwachagua na kuwasimika wazee wanaofaa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa; watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa na jamii inayowazunguka.

Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe Askofu kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi!

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, alizaliwa kunako mwaka 1966, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1996. Mwaka 2011 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Kunako mwaka 2014, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Huko akaendeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tarehe 21 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu Katoliki la Mbeya na anatarajiwa kusimikwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019, wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu.

Askofu mkuu mteule Nyaisonga, Jumatano, tarehe 24 Aprili 2019, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kumshukuru Mungu pamoja na kuiaga familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda, anapoanza kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wake kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya, Tanzania. Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda akiwemo pia Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu mteule Nyaisonga amekazia umuhimu wa familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda kujenga na kudumisha: Umoja, Upendo na Mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Katoliki Mpanda.

Wawe wepesi kuyaenzi yale mema yaliyotendwa na waasisi wa Jimbo Katoliki Mpanda lililoanzishwa kunako mwaka 2000 kama sehemu ya matunda ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo na kuwekwa chini ya uongozi wa Hayati Askofu William Pascal Kikoti. Unyenyekevu na huduma ya upendo viwe ni nguzo msingi itakayoiwezesha familia ya Mungu Jimbo Katoliki Mpanda kuweza kutumia vyema karama na mapaji yake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu! Wenye unabii watoe unabii kadiri ya imani ya Kanisa Katoliki; Wenye huduma wahudumie kwa mfano wa Kristo Mchungaji mwema; wenye kufundisha waendelee kujisadaka bila kuchoka; yaani yote yafanyike kwa ukarimu, moyo mweupe, juhudi, maarifa na bidii kama kielelezo cha ushuhuda wa furaha ya Injili.

Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu mteule Nyaisonga amewasihi Mapadre kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, daima wakijitahidi kushirikiana na Mamlaka halali za Serikali, ili kuweza kuwahudumia vyema watanzania: kiroho na kimwili. Hizi ni tunu msingi zitakazochochea kwa namna ya pekee kabisa: ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Mpanda katika masuala ya kiuchumi, kijamii na kiroho. Lengo ni kutafuta, kujenga na kudumisha amani inayojikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kama anavyofafanua Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani duniani” wa mwaka 1963.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Runangaza Ruzoka wa Jimbo kuu la Tabora, ameikumbusha familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Mpanda, historia ya uinjilishaji katika eneo kuzunguka Ziwa Tanganyika. Jimbo Katoliki la Mpanda asili yake ni Parokia ya Karema, yaliyokuwa makazi ya Askofu wa kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ameitaka familia hii, kuendeleza shughuli za kichungaji na utume ulioanzishwa na Askofu mkuu mteule Nyaisonga, ambaye katika kipindi cha miaka michache ya uongozi wake, amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Jimboni humo. Anasema, ni kiongozi ambaye ameonesha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kushirikiana na watu wote wa Mungu bila ubaguzi wala kujali umri, hali, tabaka, dini au itikadi ya mtu; mambo ambayo yamemjengea heshima kubwa ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Mpanda.

Askofu mkuu mteule Nyaisonga amejitahidi kujenga na kuboresha miundo mbinu ya shughuli za kichungaji. Kwa kuendelea kuhamasisha miito, lakini kikubwa zaidi kwa kuwekeza katika malezi na majiundo makini ya majandokasisi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanakuwa na nyumba ya malezi. Ni kiongozi anayetambua karama za Mashirika mbali mbali ya Kitawa na Kazi za Kitume na alihakikisha kwamba, anawakaribisha watawa wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Kati ya Mashirika haya ni Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kutoka Kenya pamoja na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, ambalo limepewa dhamana ya kuendeleza maisha na utume kwenye Parokia ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Shamwe! Yaani hadi raha!

Jimbo la Mpanda

 

25 April 2019, 14:07