Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu Katoliki la Mbeya, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 28 Aprili 2019 anasimikwa rasmi! Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu Katoliki la Mbeya, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 28 Aprili 2019 anasimikwa rasmi! 

Askofu mkuu Nyaisonga, Jimbo kuu la Mbeya Kumekucha! Yaani!

Jimbo kuu Katoliki la Mbeya linazinduliwa rasmi 28 Aprili 2019, lina jumla ya Parokia 52 zinazohudumiwa na Mapadre 122. Kwa sasa Jimbo lina jumla ya waseminari wadogo 248, na mafrateri 75. Kuna mashirika 12 ya kitawa na kazi za kitume yanayoshiriki maisha na utume wa Kanisa mahalia. Jimbo kuu la Mbeya lina “jeshi” la Makatekista wapatao 1, 200 wanaolitegemeza Kanisa huko vigangoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, alizaliwa kunako mwaka 1966, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1996. Mwaka 2011 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa na hatimaye kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma. Kunako mwaka 2014, akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Huko akaendeleza utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Tarehe 21 Desemba 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu Katoliki la Mbeya na anatarajiwa kusimikwa rasmi tarehe 28 Aprili 2019, wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu.

Jimbo kuu Katoliki la Mbeya kwa sasa lina jumla ya Parokia 52 zinazohudumiwa na Mapadre 122. Limebahatika kuwa na idadi kubwa ya miito ya kipadre, kwani kwa sasa Jimbo lina jumla ya waseminari wadogo 248, na mafrateri 75. Kuna mashirika 12 ya kitawa na kazi za kitume yanayoshiriki maisha na utume wa Kanisa mahalia. Jimbo kuu la Mbeya lina “jeshi” la Makatekista wapatao 1, 200 wanaolitegemeza Kanisa huko vigangoni. Tukio hili linatanguliwa kwa namna ya pekee na mapokezi makubwa ya Askofu mkuu mteule Nyaisonga na ujumbe wake kutoka Jimbo Katoliki Mpanda shughuli inayoongozwa na Padre Francis Magala, Msimamizi wa Jimbo kuu teule la Mbeya. Akiwa njiani kuelekea Mbeya, Askofu mkuu mteule Nyaisonga atapata nafasi ya kusalimiana pamoja na kusali na waamini wa Jimbo Katoliki Sumbawanga na atapokelewa kwenye Parokia ya Mpemba, Jimbo kuu Katoliki la Mbeya, Jumamosi, tarehe 27 Aprili 2019.

Ifuatayo ni Sala ya Kumwombea Askofu mkuu mteule wakati wa mapokezi: Tunampokea mchungaji wetu mkuu wa Jimbo Kuu Teule la Mbeya, tunakuomba umjalie Roho Mtakatifu ampe nguvu na uwezo ili awafahamu vizuri kondoo wake, nasi kondoo wake tuisikie sauti yake na kuifuata kwa kushirikiana naye kikamilifu ili tuweze kulijenga na kuliendeleza kanisa lako. Tunaomba umjaze Roho wa upendo, umoja, amani, ukarimu kwa watu wote, tunapounganishwa kwa pamoja chini ya kiongozi wetu huyu mkuu tuweze kwa pamoja kulijenga Kanisa lako.  

Jioni, Askofu mkuu mteule Nyaisonga ataonesha hadharani hati za uteuzi wake, atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, ataongoza masifu ya jioni, atakiri Kanuni ya Imani pamoja na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ifuatayo ni sala ya kumwombea Askofu mkuu mteule wakati wa Masifu ya Jioni, Ee Mungu uliye mchungaji wa milele wa waamini,Wewe unalisimamia kwa hekima nyingi Kanisa lako na kulitawala kwa mapendo.Tunaomba huyu mtumishi wako Askofu Mkuu mteule Gervas J.M. Nyaisonga atusimamie sisi taifa lako, umjalie aliongoze kundi lako kwa niaba ya Kristo, afundishe imani ya kweli, awe Kuhani wa ibada takatifu na Mtumishi mwenye madaraka.

1. KUKIRI IMANI – Profesi Fidei

Mimi Askofu Gervas J.M. Nyaisonga Kwa imani thabiti ninasadiki na kuungama na kila moja ya yale yaliyomo katika kanuni ya imani yaani: Nasadiki kwa Mungu mmoja, Baba mwenyezi, muumba wa mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, mungu kweli kwa mungu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa. Mwenye umungu mmoja na baba ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Alishuka kutoka mbinguni, kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu.

Akasulubiwa kwa ajili yetu sisi, kwa mamlaka ya Pontio Pilato; akateswa, akafa na akazikwa, siku ya tatu akafufuka kadiri ya Maandiko, akapaa mbinguni ameketi kuume kwa Mungu baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu Bwana na mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana, anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki, la mitume. Naungama ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi.

Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele. Aidha kwa dhati kabisa, nakiri na kushika mambo yote ya pamoja na kila moja peke yake, yanayohusu mafundisho ya imani, na desturi ambazo zimeamriwa na Kanisa kwa maamuzi rasmi, au yaliyoagizwa na kutangazwa na ualimu wa kawaida wa Kanisa, au yale yanayotolewa na Kanisa lenyewe, hasa mintarafu fumbo la Kanisa takatifu la Kristo, Sakramenti zake, Sadaka ya Misa takatifu, na Ukhalifa wa Baba Mtakatifu wa Roma.

2. KIAPO CHA UAMINIFU –Profesio Fidelitatis

Mimi Askofu Gervas J.M. Nyaisonga niliyeteuliwa kuwa Askofu Mku wa Jimbo Kuu Teule la Mbeya. Nitakuwa daima mwaminifu kwa Kanisa Katoliki na kwa Askofu wa Roma, ndiye mchungaji wake mkuu, tena Wakili wa Kristo, Khalifa wa Petro mtume katika ukulu wake. Nitakuwa pia mwaminifu kwa urika wa maaskofu. Nitajali utekelezaji huru wa mamlaka makuu ya Papa kuhusu Kanisa ulimwenguni kote. Tena nitajibidisha kuhifadhi na kupigania haki za madaraka hayo. Nitazitambua na kuzilinda haki na nyadhifa za wajumbe wa Askofu wa Roma, kwa maana hao huwakilisha nafsi ya mchungaji mkuu mwenyewe.

Nitajitahidi kwa bidii kubwa kuzitekeleza kazi walizokabidhiwa maaskofu, yaani kulifundisha Taifa la Mungu, kulitakatifuza na kuliongoza. Hayo nitayafanya nikiunganika na kichwa cha urika wa maaskofu, nikiunganika pia na maaskofu wengine wote katika umoja wa hiarakia. Nitaulinda umoja wa kanisa ulimwenguni. Kwa hiyo nitajishughulisha kwa bidii ili hazina ya imani, tuliyoipata kutoka kwa mitume, itunzwe safi na kamili. Nitautunza pia ukweli ulio wa lazima kusadikiwa na kutekelezwa kimaadili. Huo ukweli nitauangalia ufundishwe na uelezwe kwa wote kama anavyoeleza mwalimu Mama Kanisa. Lakini waliopotoka katika kazi nitawaonesha moyo wangu wa kibaba na nitatumia misaada yote mpaka waufikie ukamilifu wa ukweli Katoliki.

Nitajiwekea Kristo, Kuhani mkuu wa milele, mbele ya macho yangu kama mfano wangu nitaishi kikamilfu na kitakatifu. Tena nitautimiza utumishi wangu niliokabidhiwa jinsi hii hata nionekane kielelezo kamili cha kundi langu, niweze kuwaimarisha waamini katika njia ya ukamilifu wa Kikristo. Nitahifadhi nidhamu inayohusu Kanisa kwa ujumla na nitasisitiza kwa busara yote ili sheria zote hasa zile za kitabu cha sheria za Kanisa zishikwe. Papo hapo nitaangalia daima ili mazoea mabaya yasijijenge hasa kuhusu utumishi wa Neno na kuhusu maadhimisho ya Sakramenti. Nitashughulikia kwa uangalifu mali ya Kanisa, hasa mali ile iliyowekwa kwa kuendeshea Ibada takatifu na ile kwa ajili ya wakleri na ya watumishi wengine wa Kanisa.

Nitatunza pia kwa bidii mali iliyotolewa kuendeshea utume na matendo ya huruma. Katika kutekelea wajibu nilokabidhiwa nitawatendea kwa upendo wa pekee mapadre na mashemasi wote, maana hao wamewekwa kuwasaidia maaskofu. Watawa waume kwa wake watapata upendo wangu wa pekee kwa vile nao ni wasaisidizi wa maaaskofu. Vivyo hivyo nitajishughulisha sana kustawisha miito mitakatifu, ili mahitaji ya kiroho ya Kanisa yapatikane inavyotakiwa. Nitaitambua na kuikuza hadhi ya waamini walei, kwa maana wana sehemu yao ya pekee katika utume wa Kanisa.

Naam, nitavitunza kwa jitihada kubwa vyama vilivyoundwa kuhifadhia na kuendeshea uenezaji wa Habari Njema kwa Mataifa. Niitwapo kwenye Mitaguso na kwenye shughuli nyingine za kirika nitahudhuria, isipokuwa nimezuiliwa, au nitaitikia itakiwavyo. Wakati uliopangwa au kwa nafasi yoyote ya pekee nitatoa ripoti kuhusu kazi yangu ya kichungaji kwa Baba Mtakatifu na kupokea na kukubali maagizo na mashauri yake na kuyatekeleza kwa jitihada yote. Kwa hayo yote Mungu anisaidie na hizi Injili takatifu za Mungu ninazogusa kwa mikono yangu.

Jumapili ya huruma ya Mungu tarehe 28 Aprili 2019, Mwanzo mpya Jimbo la Mbeya: Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Misericordiae vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Yesu Kristo ni uso wa huruma ya Baba wa milele na kwamba, Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ya Mungu ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa njia ya maisha na utume wake, Kristo Yesu amewafunulia walimwengu huruma ya Mungu. Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati zote. Huruma ya Mungu ni daraja linalomuunganisha Mungu na binadamu na kuufungulia moyo wa binadamu mlango wa matumaini ya kupendwa daima, licha ya dhambi na mapungufu yanayo mwandama mwanadamu!

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo, aliamua kuipatia Jumapili hii, umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa ili kutoa nafasi kwa watu wa Mungu kutafakari huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujichotea nguvu na neema zinazobubujika kutoka katika huruma ya Mungu kwa njia ya  maadhimisho ya Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho inayowakirimia waamini: upya wa maisha, amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka katika maisha yao!

Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anasimikwa katika maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Jijini Mbeya. Rais John Pombe Magufuli ndiye mgeni maalum katika tukio hili. Waswahili wanasema eti jamani Mbeya kumenoga kwani macho na masikio ya familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania kwa sasa wanayaelekeza Jimbo kuu Katoliki la Mbeya.

Jimbo kuu la Mbeya
26 April 2019, 13:41