Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Ctistabal Lòpez Romero: Changamoto za maisha na utume wa Kanisa baada ya hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Morocco! Askofu mkuu Ctistabal Lòpez Romero: Changamoto za maisha na utume wa Kanisa baada ya hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Morocco! 

Hija ya Papa Francisko Morocco: Changamoto za utume wa Kanisa!

Askofu mkuu Cristabal López Romero wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco anamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa changamoto alizotoa kwa familia ya Mungu nchini Morocco kuhusu : majadiliano ya kidini ; uekumene wa huduma ya upendo na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Sasa kuna haja ya kuanza kuzivalia njuga!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Morocco limekita mizizi yake katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na haki: Kanisa la linaendelea kujipambanua kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uekumene wa huduma ya upendo na kwamba, hili ni Kanisa ambalo ni daraja kati ya Wakristo na Waislam, Kati ya Bara la Afrika na Ulaya. Askofu mkuu Cristabal López Romero wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco anamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa changamoto alizotoa kwa familia ya Mungu nchini Morocco  kuhusu : majadiliano ya kidini ; uekumene wa huduma ya upendo na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji.

Askofu mkuu Cristabal López Romero anasema Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchakato wa kuzima kiu ya amani duniani, kwa kuitafuta, kuidumisha na kuhakikisha kwamba, waamini wanakuwa ni vyombo vya amani duniani vinavyofumbatwa katika udugu wa kibinadamu. Amekazia umuhimu wa Familia ya binadamu na ujasiri wa kuwathamini wengine; Majadiliano ya kidini na sala; elimu na haki; pamoja na udugu kama Sanduku la Agano na maendeleo fungamani. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kuanzia sasa!

Kuhusu uekumene wa huduma ya upendo, Baba Mtakatifu amesema, “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” ni muhtasari wa sera na mikakati ya Kanisa Katoliki katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kama njia ya kujenga na kudumisha mafungamano na kundi hili badala ya kukaa kimya. Ni mwaliko wa kuwaokoa badala ya kuwatenga, ili kuwajengea uwezo badala ya kuwatelekeza. Watu wote wanahusika ili kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji wanapatiwa maisha bora, wanahakikishiwa usalama pamoja na kuoneshwa mshikamano. Askofu mkuu Cristabal López Romero anasema, jambo la msingi ni kuwafungulia kwanza watu nyoyo na mengine yanafuata.

Uinjilishaji nchini Morocco unapaswa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si katika wongofu wa shuruti. Hii ni changamoto ambayo ilikwisha kutolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Uinjilishaji iwe ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na maridhiano ; udugu, ukweli na uwazi ; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kanisa Morocco
03 April 2019, 15:29