Vatican News
Askofu Almachius Rweyongeza: Ujumbe wa Pasaka 2019: Dhamiri nyofu, Amani, Elimu na Afya! Askofu Almachius Rweyongeza: Ujumbe wa Pasaka 2019: Dhamiri nyofu, Amani, Elimu na Afya!  (2017 Getty Images)

PASAKA YA BWANA 2019: Askofu Rweyongeza: Amani, Elimu & Afya!

Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2019 amekazia umuhimu wa familia ya Mungu nchini Tanzania kufanya tathmini juu ya maisha yao, kwa kukumbatia amani, kila mtu akiwajibika barabara; kujenga dhamiri nyofu pamoja na kuendelea kupambana na maadui wa taifa yaani: ujinga, magonjwa na umaskini.

Na Sarah Pelaji, - Dar es Salaam.                           

Waamini: “Tunaposherehekea Pasaka tunapaswa kukumbuka kuwa baada ya Yesu kufufuka alituachia zawadi ya amani.  Amani kwenu” (Yohane 20:19, 21, 26).  Tunaweza kusema Pasaka ni Sherehe ya kutakiana amani. Amani hii inatokana na msalaba au kuwajibika na kubeba majukumu yetu tukimuiga Yesu. Kumbe amani siyo tu kutokuwepo kwa vita. Tena amani si tu matokeo ya utawala wa mabavu, bali inaitwa kwa usahihi kamili: ‘Kazi ya haki’ (Isaya 32:17). Amani haiwezi kufikiwa mara moja kwa daima, bali inadaiwa kujengwa siku kwa siku.  Aidha, maadam utashi wa binadamu ni dhaifu na umejeruhiwa na dhambi, kuleta amani kunadai siku zote kila mtu azitawale tamaa zake, na serikali ijihusishe katika kulinda amani” (GS, na 78).”

Hayo yamesemwa na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga, katika Ibada ya Misa Takatifu Sherehe ya Pasaka iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu George, Jimbo Katoliki Kayanga Karagwe, Kagera. Akiendelea kuihusisha Pasaka na wajibu wa taifa kudumisha amani Askofu Rweyongeza amesema kuwa, Pasaka ni wakati wa kufanya tathmini ya maisha ya mtu binafsi, familia, jumuiya, Kanisa na taifa kwa ujumla. “Tufanye tathmini juu ya maisha yetu, kama yanaendelea kuikumbatia amani ya Kristo Mfufuka ama la. Kama tuambiwavyo na hekima ya wazee: ‘Biashara asubuhi, jioni mahesabu,” ‘Mali bila daftari hupotea bila habari.’ Nasi katika kusherehekea Pasaka hii tujitafiti, tujichunguze, tujitathmini” amesema.

Amewataka waamini kufanya tathmini juu ya maisha yao ya sala kwani sala zinafariji, zinatia nguvu, zinatia moyo, haukwami. Yesu alisali kabla ya kila tukio; aliwaasa wanafunzi wake kusali (ndio sisi), na alifundisha namna ya kusali (Mathayo 6:9-13; Luka 11:1-13). Pia kufanya tathmini juu ya Sakramenti za Kanisa ambazo wanapaswa kuzipokea hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu. Aidha wafanye tathmini juu ya vipaji na karama zako. Vipaji hivyo si kwa ajili ya mtu binfsi bali kwa ajili ya maendeleo ya jamii na Kanisa kwa ujumla.  Amelitaka taifa kufanya tathmini juu ya adui ujinga na kupambana naye kwa silaha ya Elimu. “Tunapojitahidi kwa ujumla wetu kuleta maendeleo ya pamoja, tusisahau kujenga dhamiri (consciences) za watoto wetu na zetu pia. Maandiko Matakatifu husema: “Dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi-Mungu; huchunguza nafsi yake mtu mpaka ndani kabisa” (Methali 20:27),” amesema.

Askofu Almachius Rweyongeza amesema kuwa, maendeleo bila dhamiri safi na njema hubomoka mara moja. Bila dhamiri safi, jasho la muda mrefu la kuleta maendeleo na ustawi huharibiwa kwa muda mfupi. Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa, katika Barua yake ya Kichungaji juu ya Utume wa Kanisa (Redemptoris Missio) anatuasa juu ya umuhimu wa malezi na ujenzi wa dhamiri akisema: “…maendeleo ya watu, kwanza hayajengwi katika misingi ya pesa, vitu na teknolojia, bali yanatokana na malezi bora ya dhamiri na makuzi bora ya fikra na tabia njema” (Redemptoris Missio, n.58, 7 Desemba, 1990).  Kumbe, mtu akiwa na dhamiri njema, anakuwa bora zaidi na akimiliki mali, ataitumia kwa moyo wenye shukrani na atawajali wengine.

Ameeleza kuwa, baada ya taifa kupata uhuru Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alibaini maadui watatu wa Taifa letu, maadui wa amani, maendeleo na ustawi: ujinga, maradhi na umaskini.  Baada ya kumshinda mkoloni aliona bado taifa lina kazi kubwa ya kupamba na maadui hao. Amesema: Kwenye geti la Chuo Kikuu fulani kuna maandishi yasomekayo: “Ukitaka kuangamiza taifa lolote, huhitaji kutumia silaha za nyukilia.  Njia nzuri ya kuangamiza taifa ni kuharibu mfumo wa elimu.  Ruhusu mbumbumbu waonekane ‘wamefaulu’ na wasonge mbele hadi Vyuo Vikuu. “Matokeo yake yatajidhihirisha baada ya muda:  mbumbumbu hao ‘wakishahitimu’ kwa kupata vyeti hewa / feki, wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari na manesi; majengo yataporomoka mikononi mwa wahandisi; pesa zitapotelea mikononi mwa wachumi na mafisadi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini na serikali, na haki itapotea mikononi mwa mahakimu na wanasheria.”

Askofu Almachius Rweyongeza amesema, kuchezea elimu ni kuchezea amani, ni kuangamiza Taifa. Mungu alionya watu wake kupitia kinywa cha Nabii Hosea akisema: “Watu wangu wameangamia kwa kukosa maarifa” (Hosea 4:6).” Ametaka taifa kutathmini mfumo wa elimu nchini akisema akihoji kama mfumo tulionao, ni njia sahihi ya malezi bora ya dhamiri safi na uwajibikaji, ama ni bomu: “Tunahitaji tufufuke toka kaburi hili la ujinga. Je, Mfumo wetu wa elimu ni kama biashara? Au ni haki Elimu bila wajibu? Kubadilishwa badilishwa kwa Sera na miongozo ya Elimu, si ishara wazi kwamba Watanzania kama Taifa, bado hatujui tunachokitaka, hatujui rasilimali watu wetu wawe na sifa gani, na hatujui tunataka Taifa letu la leo na kesho liweje? Mwelekeo wetu ni upi?

Kila mara tunashuhudia mitaala ya Elimu inabadilishwa bila kufanyiwa utafiti wa kina na kujiridhisha kwa maslahi mapana na kwa mustakabali wa Taifa.  Tunahitaji Elimu bora kama Taifa, inayomwezesha mwanafunzi, kutatua changamoto za maisha ya kila siku nje ya darasa,” amesema.  Aidha taifa lijitathmini katika kulegeza Vigezo au Viwango vya Ufaulu, Wanaokuwa na ufaulu wa chini ndio wanaelekezwa kuchukua taaluma ya ualimu. Je, ni sahihi? Taifa pia lifanye tathmini kama somo la Dini na Maadili linapewa kipaumbele stahiki, ubora wa elimu ni kupunguza mada au darasa katika makuzi ya mtoto? Kutokariri/Kurudia Darasa? Kama Elimu yetu na soko la ajira Afrika au Ulimwengu.

Askofu Almachius Rweyongeza amezungumzia pia kuhusu sekta ya afya nchini akitaka TASAF licha ya kutoa misaada ya fedha na chakula kwenye kaya masikini, inapaswa kuwasaidia masikini hao kupata bima ya afya ili wapate matibabu ya uhakika. “Tunashukuru na kutambua juhudi za Serikali za kuweka mfumo wa Bima ya Afya jumuishi unaolenga kumfikia kila Mwananchi. Hata hivyo, imethibitika ya kuwa asilimia 28 ya Watanzania, ambao ni sawa na Watanzania Milioni 14.2 (kwa mujibu wa Taasisi ya Takwimu ya Taifa) ni maskini kabisa; hivyo basi, hawana kabisa uwezo wa kujilipia bima ili kugharimia huduma za Afya.

Kwa mantiki hii, kwa ujumla kama Taifa, tunalo jukumu la kuhakikisha Wananchi hawa maskini wanawezeshwa kupata huduma bora za afya kote nchini. Tunaomba TASAF (Tanzania Social Association Fund/ Mfuko wa kunusuru Kaya maskini) jambo la kugharimia Bima ya Afya kwa Kaya maskini lipewe kipaumbele badala ya kuwagawia pesa kama karanga.  Bima ya Afya kwanza, kisha wape mapesa kwa mahitaji mengine ya msingi. Hivyo basi, sisi kama sehemu ya jamii, tunalo jukumu la kuhakikisha kuwa tunahimiza Kaya zote zenye uwezo wa kujiunga na Bima ya Afya kufanya hivyo. Na pia tunaiomba Serikali iendelee kuweka mikakati madhubuti ya kifedha na utaratibu wa kuchangia, na hatimaye kuhakikisha upatikanaji wa Huduma za

Mwishoni, Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga, amesema Rais Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano wanayo kazi kubwa ya kuendelea kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini na kunyosha mifumo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya mafisadi, uvivu na uzembe, rushwa na mengineyo. Amewataka wananchi waendelee hivyo, tunayo kila sababu ya kuendelea kumwombea Rais Magufuli ili Kristu Mfufuka aliyeshinda mauti amjalie nguvu ya kushinda majaribu yote, ili nchi izidi kusonga mbele katika maendeleo na kudumu katika amani.

26 April 2019, 13:09