Tafuta

Umoja wa Mataifa: Mkutano kuhusu mchakato wa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi kwa kudumisha fursa sawa kwa wote! Umoja wa Mataifa: Mkutano kuhusu mchakato wa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi kwa kudumisha fursa sawa kwa wote! 

Mapambano ya wanawake dhidi ya ukosefu wa haki duniani!

Kuanzia tarehe 11-22 Machi 2019 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kunafanyika mkutano wa Kimataifa unaoongozwa na tema “Mifumo ya Hifadhi za Jamii; Huduma za Kijamii, Miundo Mbinu Endelevu ili kudumisha usawa pamoja na kuwajengea uwezo wanawake na wasichana”. Wajumbe wanawataka kuwajengea wanawake uwezo ili wajiletee maendeleo wao wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa unasema, hatima ya wanawake wengi duniani iko mashakani kutokana na ubaguzi, nyanyaso, dhuluma na unyonyaji wanaofanyiwa kila kukicha. Kuna idadi kubwa ya wanawake wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na huduma hafifu kwa mama na mtoto pamoja na ukosefu wa dawa muhimu. Ndoa za utotoni pamoja na ndoa za shuruti ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kusababisha mateso na machungu mazito katika maisha ya wanawake. Bado kuna watu wanaodekeza mila na tamaduni ambazo zimepitwa na wakati kama vile: ukeketaji wa wasichana pamoja na urithi wa wanawake wajane, kwani matokeo yake ni kuambukizwa magonjwa na hatimaye, maafa makubwa kwa jamii!

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kila mwaka ni sehemu ya mchakato wa kutoa fursa wanawake wasiokuwa na sauti, ili waweze kusikilizwa na matamanio yao halali kutekelezwa. Umefika wakati wa kuvunjilia mbali nyanyaso na mateso wanayokabiliana nayo wanawake, sehemu mbali mbali za dunia. Wale wote wanaohusika na uhalifu dhidi ya wanawake wanapaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, ili sheria iweze kushika mkondo wake. Huu ndio msimamo wa Wanawake wa Kiekumene wanaoshirikiana na wanawake wengine pamoja na watu wenye mapenzi mema, wanataka kuona kwamba, utu na heshima na haki msingi za wanawake zinapewa msukumo wa pekee katika medani mbali mbali za maisha!

Kuanzia tarehe 11-22 Machi 2019 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kunafanyika mkutano wa Kimataifa unaoongozwa na tema “Mifumo ya Hifadhi za Jamii; Huduma za Kijamii, Miundo Mbinu Endelevu ili kudumisha usawa pamoja na kuwajengea uwezo wanawake na wasichana”. Wajumbe pamoja na mambo mengine, wanajadili kuhusu “Mchakato wa kuwajengea uwezo wanawake mintarafu maendeleo endelevu na fungamani. Wanawake wa Kiekumene wanapania kudumisha umoja, usawa na udugu, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 25, tangu umoja huu ulipoanzishwa kunako mwaka 2000. Umoja wa Mataifa unaandaa tena: “Wanawake Mwaka 2000. Usawa, Maendeleo na Amani katika Karne ya XXI”.

Huu ni mwendelezo wa Mkutano wa Wanawake Kimataifa, uliofanyika mjini Bejing kunako mwaka 1995, chini ya uongozi wa Mama Getrude Mongella kutoka Tanzania. Mkutano huu, utaangalia: matatizo na changamoto zilizojitokeza hata kukwamisha Maazimio yaliyokuwa yamefikiwa kwenye Mkutano wa Wanawake Kimataifa huko Bejing. Wanawake wa Kiekumene wanaendelea kujiekeleza zaidi katika kupigania: haki, usawa na umuhimu wa wanawake kupata huduma msingi kwa kuzingatia ulinzi na usalama wa maisha yao. Wanataka kuona kwamba, wanawake wanapata pia fursa za ajira na ujira sawa; wanaheshimiwa na kulindwa kwenye maeneo ya kazi; wanajengewa nguvu za kiuchumi ili kukabiliana na hali pamoja na mazingira yao, lakini zaidi, wanataka kuona kwamba, wanawake na wasichana ambao walibakizwa nyuma kwenye sekta ya elimu, wanapewa nafasi ya kuendelea na masomo.

Kumbe, Jamii inawajibika kulinda na kudumisha haki zao katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni. Wanawake wanataka kuona Jumuiya ya Kimataifa ikisherehekea umoja na mshikamano unaofumbatwa katika utofauti wao wa kijinsia kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Haki Msingi Wanawake
12 March 2019, 09:11