Cerca

Vatican News
Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika Ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2019 anakazia umuhimu wa kufunga ba kusali katika maisha na utume wa Kanisa Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika Ujumbe wake kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2019 anakazia umuhimu wa kufunga na kusali katika maisha na utume wa Kanisa  (ANSA)

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Patriaki Bartolomeo: Kufunga!

Kufunga na kusali kunawawezesha waamini kuvuta msaada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili kutakaswa na kuondolewa dhambi zao, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa kusimama thabiti katika imani, matumaini na mapendo, na kamwe wasiwe tena chini ya kongwa la utumwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Toba na wongofu wa ndani ni kati ya mafundisho makuu yaliyotolewa na Yesu mwenyewe na huu ni mwaliko endelevu unaotolewa na Mama Kanisa kwa watoto wake kila wakati lakini kwa namna ya pekee, Kipindi cha Kwaresima. Pamoja na mwaliko wote huu, lakini bado Wakristo wengi hawajaweza kumwilisha ujumbe huu katika uhalisia na undani wa maisha yao. Ujumbe huu unagusa dhamiri, kwani dhana ya dhambi inaonekana kutoweka kwa wengi.

Wongofu unawawajibisha hata watakakatifu ili wasirudie tena nafasi za dhambi na hatimaye kutenda dhambi. Wongofu wa ndani unawasaidia waamini kuwa tayari kubadilika na kuchuchumilia mambo makubwa na dumifu katika ujenzi wa mahusiano mema na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao. Lengo ni kukoleza fadhila ya upendo, unyenyekevu, kiasi na amani ya ndani. Baada ya toba, waamini wawe wepesi kwenda kuungama dhambi zao, ili waweze kupokea maondoleo ya dhambi, huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!

Kwaresima ni kipindi kinachowahamasisha waamini kudumu katika sala yaani: sala binafsi, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa sala katika familia, ushiriki mkamilifu katika sala na Ibada za Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo na katika Parokia. Kwaresima ni kipindi cha kutakasa nyoyo, kwa kusaidiwa kuondokana na vikwazo vya maisha ya kiroho, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu unaoleta wokovu kwa moyo mweupe kama “tui la nazi”. Na kwa njia hii, wataweza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kutangaza na kushuhudia ile furaha ya Injili!

Kwaresima ni wakati wa kujitoa sadaka, kufunga na kujinyima, ili kurekebisha vilema na kunyenyekesha miili, kwa kushinda vishawishi, nafasi ya dhambi na hatimaye dhambi zenyewe. Haya ni mapambano ya maisha ya kiroho. Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2019 anawaalika waamini kufunga na kusali, utajiri na amana inayowawezesha waamini kumfahamu Mwenyezi Mungu, kutoka katika undani wa maisha yao.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema, kufunga na kusali si upendeleo kwa wateule wachache ndani ya Kanisa, bali ni tendo la Kanisa zima, linalopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu: kiroho na kimwili. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anawakumbusha waamini kwamba, mtu asitafute faida yake mwenyewe, bali ya wenzake! (Rej. 1Kor.10:24) Ustawi na mafao ya jirani katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili ndiyo changamoto kubwa inayopaswa kumwilishwa katika Kipindi cha Kwaresima.

Ikumbukwe kwamba, kufunga na kusali kunawawezesha waamini kuvuta msaada na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili waweze kutakaswa na kuondolewa dhambi zao, tayari kuweza kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka. Huu ni mwaliko wa kuondokana na uchoyo na ubinafsi, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa kusimama thabiti katika imani, matumaini na mapendo, na kamwe wasiwe tena chini ya kongwa la utumwa! Uhuru wa kweli unawawezesha waamini kushirikishana tunu na mema ya mbinguni kama ushuhuda wa imani tendaji.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaendelea kufafanua kwamba, hakuna mtu anayeweza kujitosheleza katika mambo yote, kwani watu wanasaidiana, wanategemezana na kukamilishana katika hija ya maisha yao hapa duniani! Huu ndio uhuru wa kweli unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu kama anavyosema Mtakatifu Paulo, lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. (Rej. 1Th. 5:18). Uhuru wa kweli unajikita katika kanuni ya umoja, upendo na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali tabia ya migawanyiko na mipasuko katika jamii.

Kufunga ni ibada inayotakiwa kutekelezwa kwa moyo mnyoofu na kwa furaha, kama sehemu ya ushiriki wa mwamini katika mateso ya Kristo Yesu. Waamini wajibidishe kushiriki sala na ibada mbali mbali katika Kipindi hiki cha Kwaresima, wakiwa na matumaini ya kushiriki katika Pasaka ya milele. Kumbe, Kipindi cha Kwaresima, iwe ni nafasi muafaka ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi, na kuomba neema ya kudumu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kuwasaidia maskini: kiroho na kimwili. Kwa njia ya kutubu na kuongoka; kufunga na kusali; kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, waamini watakuwa wamejiandaa kikamilifu kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Patriaki Bartolomeo: Kwaresima 2019
18 March 2019, 09:00