Tafuta

Vatican News
Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima: Ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya Shetani, Ibilisi Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kwaresima: Ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya Shetani, Ibilisi 

Neno la Mungu, Jumapili Kwanza ya Kwaresima: Kristo Yesu

Injili inamwonesha Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu. Pili Kristo anaakisi katika nafsi yake yale taifa la Mungu lililoyapitia katika historia ya ukombozi: mafungo ya siku 40 aliyoyafanya nyikani yanaakisi miaka 40 waliyokaa jangwani; mkate unaakisi mikate ambayo waisraeli walikuwa wakimdai Musa jangwani. Tatu, majibizano kati ya Yesu na ibilisi yanaonesha mapambano yaliyopo!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 1 ya Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Hiki ni kipindi cha kukua na kuimarika katika imani, matumaini na mapendo, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu unaoleta wokovu!

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Kum 26,4-10) ni kutoka kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Linaleta sala aliyokuwa akiisali myahudi alipokwenda kumtolea Mungu shukrani ya mavuno yake ya kwanza. Sala hiyo ilikuwa ni kanuni ya imani. Kanuni ya imani ya Myahudi ilikuwa ilikuwa ni kupitia historia ya matukio makuu ya taifa lao kama wayahudi na katika historia hiyo kukiri mkono wa Mungu na uwepo wa Mungu ambao umeisindikiza na kuiunda historia hiyo. Ndiyo maana katika sala yake hiyo anaanza kutaja baba zake, bila hata kutaja majina tunaona wazi kwanza jinsi Abrahamu alivyotoka kuelekea nchi ya ahadi, jinsi Yakobo na wanawe walivyoingia Misri na  mateso yao yaliyofuata na mwishowe jinsi Bwana alivyowatoa utumwani Misri na kuwaingiza katika nchi ya ahadi.

Kwa jinsi hiyo, tendo la kumtolea Mungu mavuno ya kwanza kama shukrani lilikuwa ni tendo la kukuza imani kwa wayahudi. Liliwakumbusha ukuu wa Mungu na uwepo wake wenye nguvu katika historia ya maisha yao. Liliwaonesha kuwa Mungu hakubaki tu katika historia hiyo ya kale bali hadi sasa bado yupo nao. Aidha, tendo hilo la shukrani ya mavuno ya kwanza liliwafanya waone kuwa mavuno waliyoyapata ni ya Mungu na ni wajibu wao kumrudishia kwa shukrani. Mavuno hayo ni ya Mungu kwa sababu ni yeye aliyewaongoza kwa nguvu zake kufika katika ardhi hiyo na ni yeye aliyewapa ardhi hiyo. Somo hili linaletwa kwetu katika jumapili hii ya mwanzo ya Kwaresima kutuonesha nasi pia kuwa Kwaresima ni kipindi cha kukua katika imani. Ni kipindi cha kusogea karibu zaidi na Mungu na hasa ni kipindi cha kumuona Mungu katika maisha yetu.

Somo la pili (Rum 10:8-13) ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika Waraka huu, mojawapo ya mambo anayozungumzia kwa kirefu Mtume Paulo ni utofauti katika ya Torati ya Musa na Imani kwa Kristo. Dini ya kiyahudi ilikuwa imejengwa juu ya msingi wa Torati na hiyo waliishika kwelikweli. Paulo alilenga kuwaonesha kuwa Torati ni njema; iliwapatia haki ila haitoshi kumpatia mtu wokovu kwa sababu ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaanda kuupokea utimilifu wake kwa njia ya Kristo. Katika somo la leo, Paulo ananukuu na kutafsiri maneno ya Musa katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 30:12 kuonesha kuwa kuipata imani hii si kazi ngumu. Ananukuu “lile Neno li karibu nawe, katika kinywa chako na katika moyo wako” na kuonesha kuwa si kazi ngumu kwa kuwa Kristo yuko tayari ndani  mtu. Kazi ya yule anayetaka kuupata wokovu wake ni kumkiri kwa kinywa na kuiamini kwa moyo Habari Njema yaani katika Mateso yake, Kifo chake na Ufufuko wake uletao wokovu.

Injili (Lk 4:1-13). Injili ya leo, kadiri ya Mwinjili Luka, inaonesha Yesu anashinda katika  vishawishi. Kishawishi cha kwanza anachoshinda ni kile cha kutumia vibaya nafasi yake kama Mwana wa Mungu – kugeuza jiwe kuwa mkate. Kishawishi cha pili ni kile dhidi ya tamaa ya madaraka na ufahari – nitakupa enzi hii yote na fahari ukinisujudia. Kishawishi cha tatu ni dhidi ya kuziweka majaribuni ahadi zake Mungu – jitupe chini maana imeandikwa atakuagizia malaika wake wakulinde. Kristo anajionesha kama mfano wa kufuata katika kushinda majaribu na vishawishi maishani lakini hasa anajionesha kama msaada na nguvu kwamba kwa njia yake na pamoja naye, ubinadamu dhaifu unapata kushinda dhidi ya majaribu na vishawishi.

Pamoja na fundisho hili, mwendo wa silimulizi la Injili ya leo unalenga pia kumtambulisha Kristo. Kuonesha Kristo ni nani na nafasi yake ni ipi katika maisha ya wanaomwamini. Kwanza kabisa Injili inamwonesha Kristo kuwa ni Mwana wa Mungu, na ndiyo maana jaribio lake la kwanza linalenga kuvunja kiri hiyo; “ukiwa ndiwe mwana wa Mungu…” Pili Kristo anaakisi katika nafsi yake yale taifa la Mungu lililoyapitia katika historia ya ukombozi: mafungo ya siku 40 aliyoyafanya nyikani yanaakisi miaka 40 waliyokaa waisraeli jangwani wakielekea nchi ya ahadi; mkate alioshawishiwa kuutengeneza kimiujiza unaakisi mikate ambayo waisraeli walikuwa wakimdai Mungu na Musa jangwani. Tatu, majibizano kati ya Yesu na ibilisi yanalenga kuonesha mapambano yaliyopo kati ya ufalme wa Mungu aliokuja kuujenga Kristo na ufalme wa shetani unaotaka kuuweka ulimwengu mateka.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tangu Jumatano ya Majivu tumeingia katika kipindi cha Kwaresima. Kipindi cha siku arobaini za toba, kufunga, sadaka na matendo ya huruma kujiandaa kuyaadhimisha mafumbo makuu ya wokovu wetu, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.  Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya kwanza yanatuonesha kuwa mwaliko huu wa Kwaresima ni mwaliko pia wa kukua katika imani. Na kitu kinachokuza imani ni matendo ya imani. Somo la kwanza limetuonesha mojawapo ya matendo ya imani ni ibada na limeonesha uhusiano uliopo kati ya ibada ya shukrani ya mavuno ya kwanza ya wayahudi na kiri yao ya imani.

Kwa Wayahudi kila ibada ilitafsiri sehemu fulani ya maisha yao, kwa jinsi hii ibada haikuwa kitu tofauti na maisha bali ibada ilikuwa ni maisha yenyewe yanayoelekezwa kwa Mungu na kurudishwa kwa Mungu kama shukrani. Ibada za kanisa zimechota tunu hii. Tunapoziangalia kwa ukaribu ibada zetu, ndani yake tunayaona maisha yetu katika ujumla wa hali zake na hivi ibada hatuzifanyi hivi hivi tu bali pamoja na kumtukuza Mungu na kututakatifuza, zinakuwa pia ni mwaliko wa kuyainua maisha yetu yafanane nazo. Kipindi hiki cha Kwaresima ni kipindi cha kushiriki kwa wingi ibada ili kukuza imani. Pamoja na adhimisiho la Misa, zipo ibada mahsusi za Kwaresima kama vile Njia ya Msalaba, Hija na Maungamo na tafakari ya Mateso ya Bwana ambazo hukuza imani yetu katika kipindi hiki cha Kwaresima.

Leo pia tumeona juu ya uwepo wa mapambano yaliyopo kati ya nguvu za ufalme wa Mungu na nguvu za utawala wa shetani. Ni mapambano ambayo shetani hukusudia kutuangusha katika dhambi na kutumiliki kwa njia ya majaribu na vishawishi mbalimbali ili kututoa katika ufalme wa Mungu. Mwaliko wa dominika hii ya kwanza ya Kwaresima ni kutambua udhaifu wetu wa kibinadamu katika kupambana na majaribu na vishawishi mbalimbali ili kumtazama na kumtumainia daima Yeye aliyeshinda vishawishi ili kwa njia yake nasi tuvishinde na kuingia katika ufalme wake. Kumwomba Yeye Roho ya upembuzi na nguvu ili tuiache njia inayotuingiza katika makucha ya shetani na tuielekee njia inayotuingiza katika ufalme wa Mungu. Ndivyo tunavyokusudia kuupokea mwaliko wa mfungo wa siku 40 za Kwaresima: kuomba neema ya kukua katika imani na nguvu ya kushinda vishawishi wa shetani katika maisha yetu.

Liturujia J1 Kwaresima
09 March 2019, 16:41