Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya II Kipindi cha Kwaresima: Kung'ara kwa Yesu ni utimilifu wa Unabii na Sheria katika Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Pasaka! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya II Kipindi cha Kwaresima: Kung'ara kwa Yesu ni utimilifu wa Unabii na Sheria katika Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Pasaka! 

Liturujia Neno la Mungu: Kwaresima II: Kristo & Fumbo la Pasaka!

Kristo Yesu alipokuwa akisali sura ya uso wake ikageuka na mavazi yake yakawa meupe yakimetameta. Tendo hili la kugeuka sura kwa Yesu pamoja na matukio yote yaliyoambatana nalo: kutokea kwa Musa na Eliya pamoja na sauti kusikika kutoka katika wingu, yanatoa ufupisho utume wote wa Yesu tangu ubatizo hadi ufufuko wake. Huu ni muhtasari wa Habari Njema ya Wokovu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 2 ya Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mwa 15:5-12, 17-18) ni kutoka kitabu cha Mwanzo ambapo Mungu anathibitisha ahadi zake kwa Abramu kwa kufunga naye agano.  Katika somo hili mambo mawili yanajitokeza. La kwanza ni imani ya Abramu: Mungu alipomtoa nje na kumuonesha nyota za mbinguni na kumwambia kuwa uzao wake utakuwa mwingi kama nyota hizo, Abramu aliamini na somo linasema “naye Bwana akamhesabia jambo hili kuwa haki”. Tangu Mungu alipomwahidia Abramu mtoto (Rej. Mwa. 12:2, 7) ilikuwa imeshapita miaka mingi na hakuwa amepata mtoto. Umri wake ulikuwa umeenda na mkewe Sara alikuwa tasa. Ni katika mazingira hayo ambapo kibinadamu hakuna sababu ya kumfanya mtu aamini, hakuna uelekeo wowote wa kuamini anachoambiwa, yeye aliamini. Abramu anakuwa mfano na baba wa imani. Mtume Paulo katika waraka kwa Warumi na kwa Wagalatia anatumia kifungu hiki kuonesha imani ambayo kwayo mtu anahesabiwa haki na Mungu.

Jambo la pili katika somo hili ni kwamba Mungu anakubali kuweka agano na Abramu ili kuthibitisha ahadi zake. Agano hili analiweka katika namna iliyozoeleka katika utamaduni wa nyakati za Abramu; kwamba wale wanaowekeana agano wanapita katikati ya mnyama aliyepasuliwa vipande viwili ili yeyote asiyetimiza kiaminifu makubaliano ya agano apasuke vipande viwili kama myama huyo, yaani afe. Mungu anaweka agano kuthibitisha imani. Anatambua kuwa ombi la Abramu si kupata uthibitisho ili aamini kwa sababu tayari alishaamini. Abramu aliyekwisha amini katika neno la Mungu anajiweka tayari pia kuamini katika matendo ya Mungu kuhusiana na ahadi zake.

Somo la pili (Fil 3:17-4:1) ni waraka wa mtume Paulo kwa Wafilipi. Katika somo hili Paulo anajipambanua kama mmoja wa wale walio na imani kubwa sana kwa Kristo, na hasa kwa msalaba wa Kristo. Yeye ambaye utume wake ulianza alipotokewa na Kristo mfufuka katika ile njia ya Damasko, ufufuko wa Kristo ambao umeungana moja kwa moja na mateso na kifo chake msalabani ndio mzizi na msingi wa yote. Kwa hiyo kwanza anawaalika wafilipi wamfuate yeye, wamuige yeye na waenende katika mfano aliowapa kwa sababu yeye naye anaenenda kwa mfano alioupata kwa Kristo. Paulo kama kiongozi wa imani, haoni ni sawa kuwa tu hodari katika kuifafanua imani bali anajitahidi kuwa pia mfano wa imani hiyo katika maisha yake hivi kwamba kumuiga yeye kunakuwa sawia na kuishika imani.

Filipi lilikuwa ni koloni la dola ya kirumi ambao wenyeji wao walikuwa wamepewa hadhi ya kuwa pia raia wa Roma. Hiki kiliwafurahisha sana na waliona ni fahari kubwa sana kupata uraia wa dola iliyokuwa ikitawala dunia. Inawezekana ni kwa sababu hii wafilipi walianza kufuata mitindo ya maisha ya kipagani ya kirumi ili wajifananishe vizuri na raia wa Roma. Hapa Paulo anawatahadharisha akiwaambia kuwa “wenyeji wetu uko mbinguni” – uraia wa wakristo uko mbinguni. Na kwa sababu hiyo wao kama wakristo wajihadhari wasifuate mifano ya maisha iliyo kinyume na imani yao kwa Kristo na iliyo hasa adui wa msalaba wa Kristo, kushawishiwa kuwafuata ambao mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha na nia yao ni ya mambo ya kidunia kwa sababu mwisho wa yote hayo ni uharibifu.

Injili (Lk 9:28b-36) Injili ya leo, kadiri ya Mwinjili Luka, ni tukio la Yesu kugeuka sura. Yesu aliwatwaa wanafunzi wake watatu, Petro, Yohane na Yakobo kwenda mlimani kusali. Alipokuwa akisali sura ya uso wake ikageuka na mavazi yake yakawa meupe yakimetameta. Tendo hili la kugeuka sura kwa Yesu pamoja na matukio yote yaliyoambatana nalo: kutokea kwa Musa na Eliya pamoja na sauti kusikika kutoka katika wingu, yanatoa ufupisho wa utume wote wa Yesu tangu ubatizo hadi ufufuko wake. Maneno “huyu ni mwanangu mteule wangu msikieni yeye” ni yaleyale yaliyosikika wakati wa ubatizo wake mtoni Yordani; uwepo wa Musa na Eliya ni uwakilishi wa Torati na Manabii ambavyo Yesu amekuja kuvikamilisha. Musa na Eliya kuzungumza na Yesu ni kualika kurudi nyuma na kuona kuwa Torati na mafundisho yote ya manabii yalikuwa yakizungumza kuhusu Kristo na kuhusu ukombozi wa ulimwengu atakaoukamilisha Yerusalem kwa mateso, kifo na ufufuko wake.

Kugeuka sura kwa Yesu ni tukio ambalo pia lililenga kuwaongezea wanafunzi imani na kwa imani hiyo kuwaimarisha. Somo linaonesha kuwa wakati Yesu akisali mitume walikuwa wamelala. Kulala ni tendo linalohusishwa na kukosa imani, kunakuwa ni kinyume na kukesha na kusali ambayo ni matendo yanayoonesha uwepo wa imani. Ni katika upungufu huo wa imani Petro anapendekeza kujengwa vibanda vitatu. Kwa wayahudi vibanda vilikuwa ni kumbukumbu ya kukombolewa kutoka utumwani Misri na kila mwaka walifanya sherehe ya vibanda au makambi kukumbuka pia maisha yao jangwani walipokuwa wakisafiri kuelekea nchi ya ahadi. Hoja ya Petro haikuwa mbaya tena ilikuwa ni ya kidini na yenye msingi katika Agano la Kale. Pamoja na hayo hoja yake haikuwa na nguvu kwa sababu katika Agano Jipya kuna ukombozi mkubwa zaidi kuliko ule wa Misri ambapo Kristo anaukomboa ulimwengu mzima kwa Msalaba wake na hivyo vibanda havina nafasi tena. Ndiyo maana sauti inasikika ikisema “huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni yeye”. Kiini na msingi wa yote sasa ni Kristo.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, mfungo wa Kwaresima pamoja na mazoezi yote ya kiroho yanayoambatana nao, yaani tafakari ya kina kuhusu hali yetu ya dhambi na udhaifu, kukuza fadhila za kimungu na za kibinadamu, sala na matendo mema, vyote hivi hutusaidia kuona ni wapi tulipo na ni wapi tunaelekea. Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya pili ya Kwaresima yanaendeleza dhamira kuhusu imani, dhamira ambayo tulianza kuitafakari katika dominika iliyopita. Masomo ya leo yanaleta mbele yetu picha ya Abramu na mahangaiko yake ya kupata mtoto na yanaleta picha ya Kristo anayegeuka sura akisali mlimani. Kwa Abramu tunauona mwanzo, tunaiona hali yetu ya sasa na kwa Kristo anayegeuka sura tunauona mwisho, tunaiona hali yetu ya mwisho itakavyokuwa pale tutakapoufikia utukufu wa ufufuko wetu.

Picha ya Abramu na mahangaiko yake ya kupata mtoto ndiyo inayoonesha hali yetu nasi ya sasa. Hali ambayo ubinadamu wetu unasongwa na mahitaji mengi na ya msingi, mahitaji ambayo tunajitahidi kuyaweka daima mbele ya mwenyezi Mungu tukitumainia msaada na wema wake. Picha ya kugeuka sura kwa Yesu kunaonesha mwisho wetu ambao tunapaswa kuuangalia kwa matumaini na kuuandaa katika maisha yetu ya kila siku. Katikati ya mwanzo na mwisho wetu ipo njia inayoongoza nayo si nyingine ni njia ya imani kama ile ile aliyokuwa nayo Abramu, imani ambayo si tu kusema ndiyo naamini, bali ni kujikabidhi katika nguvu na uwezo ulio mkubwa zaidi kuliko ufahamu wetu na kuliko uwezo na utashi wetu.

Simulizi la Abramu katika somo la kwanza linaanza Mungu anapomwambia Abram atoke nje atazame juu angani kuona nyota. Naye alitoka akaona akaamini. Hii ni lugha ya Kibiblia ambayo inatualika hata sisi kutambua kuwa wakati mwingine ili kuamini inatuhitaji tutoke nje – tutoke nje ya namna zetu za kufikiri, namna za kuona na kupima mambo katika mwono wa kibinadamu na kutazama juu ulipo uwezo wa Mungu. Picha hii ndiyo inayoonekana katika tukio lenyewe la kugeuka sura ambapo Yesu anawatwaa wafuasi wake na kupanda nao mlimani, kutoka katika ukawaida wa maisha na kukwea ili kukutana na Mungu katika sala.

Katika tukio lenyewe la kuguka sura, uso wa Kristo na mavazi yake yalimetameta si kwa sababu ya mwanga uliotoka nje, bali ni kwa sababu ya mwanga uliotoka ndani, naye ndio Mwanga huo uliokuja ulimwenguni kuuangazia ulimwengu ili tusitembee tena katika giza. Mwanga huo ni mwanga wa imani. Tunapongojea nasi kuufikia utukufu wetu, ni mwanga ulio ndani yetu ndio utakaotung’arisha, ni imani iliyo ndani yetu ndiyo itakayotung’arisha kwa mwanga wake. Imani yetu kwa Kristo siyo tu njia ya kutufikisha katika utukufu bali imani hiyo ndiyo utukufu wenyewe wa Kristo unaong’aa katika maisha yetu. Mungu ajalie ili mfungo wetu wa Kwaresima uwe kipindi cha kung’aa mioyoni kwetu kwa mwanga wa imani yetu ambaye ni Kristo Bwana wetu.

Liturujia J2 Kwaresima
15 March 2019, 12:21