Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anashawishiwa na Ibilisi Jangwani! Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anashawishiwa na Ibilisi Jangwani! 

Tafakari Neno la Mungu: Jumapili 1 Kwaresima: Vishawishi

Ibilisi, Shetani alimjaribu Kristo Yesu Jangwani, akataka kumpotosha ili asitimize utume ambao alikuwa amekabidhiwa na Baba yake wa milele yaani kumwokoa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti pamoja na kuzivunjilia mbali nguvu za Ibilisi, Shetani. "Usitutie katika kishawishi". Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafafanua vyema tafsiri hii. KKK 2846. Chungulia zaidi hapa!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha jumapili ya kwanza ya kwaresima. Tunaona katika masomo yetu kuwa Yesu anashawishiwa. Mara moja twaona kuwa hata sisi tuko katika hatari ya kushawishika. Yesu anashawishiwa ila anashinda. Ushindi huu wa Yesu ni uhakika kuwa hata sisi tunaweza kushinda kishawishi. Hatuna budi kujua kuwa mwanadamu na hali yake huangukia dhambi. Mtakatifu Yohane Chrysostom anasema lipo janga moja tu, nalo ni dhambi. Kipindi cha Kwaresima huanza tangu Jumatano ya majivu. Mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya haya tunayasikia/tumeyasikia kila tunapopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima. Ni mwaliko ili tuongoke, tuanze maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.

Wakati Leonardo da Vinci, mchoraji maarufu alipokuwa anatengeneza sanamu ya ‘Karamu ya Mwisho’ alitafuta mtu mwenye sura kama ya Kristo. Akazunguka jijini Roma na mwisho akakutana na mtu mwenye sura mfanano aitwaye Pietro Bandinelli. Huyu alikuwa mwimba kwaya kanisani. Ilichukua muda mrefu kukamilisha ile sanamu. Mitume wote walishatengenezwa isipokuwa Yuda Iskarioti. Leonardo akaanza tena safari ya kuzunguka jijini Roma ili kumpata mtu mwenye sura iliyopigika na kuangamizwa na dhambi, kama alivyoangamizwa Yuda Iskarioti. Hatimaye akakutana na omba omba maarufu aliyechakaa mno na kumweleza hitaji lake. Yule ombaomba akamkubalia. Alipokuwa anamalizia mchoro akamwuliza jina lake. Akamjibu kuwa anaitwa Pietro Bandinelli na akamkumbusha kuwa ni yeye aliyekuwa na sura mfanano wa Yesu. Hali hii ilimhuzunisha sana Da Vinci. Hali hii ilimtafakarisha sana Da Vinci kuhusu ubaya wa dhambi. Dhambi iliharibu kabisa sura yake ya mwili na roho.

Katika Kitabu cha Waebrania, Ebr. 2:17-18, tunaona kuwa Yesu alishawishiwa. Hali hii inamfanya atusaidie zaidi. Alifanana na ndugu zake ili awe mwenye huruma na mwaminifu kwa Mungu Baba, kwa ajili yetu. Alijua hali yetu na ndiyo maana ni mwaminifu. Katika fundisho hili twaona kuwa Yesu alichukua mwili ili ashiriki mateso yetu. Tunakumbushwa kuwa kishawishi ni kipimo cha uhuru wa mtu na kwamba mateso huwa ni kipimo cha jinsi ya kufanya maamuzi.  Mtu huru hufanya uamuzi sahihi na baada ya uamuzi sahihi hufuata majukumu. Mtumwa hushurutishwa. Akili, uhuru, utashi na neema ya Mungu vikitumika vizuri kinachofuata ni majukumu. Tumeona Yesu akisimamia hilo.

Neno la Mungu jumapili hii linatupatia changamoto ya matumizi sahihi ya akili, uhuru, utashi na neema yake Mungu. Ni katika uhuru huu, tunabeba majukumu. Katika Ebr. 4:15, tunasoma – ‘maana hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuonea huruma udhaifu wetu, kwani yeye alijaribiwa kama sisi katika mambo yote, ila hakutenda dhambi’. Katika kitabu cha Mwanzo sura ya 3, twaona jinsi mwanadamu anavyoweza kutumia vibaya hivyo vipaji. Matumizi yakiwa mabaya, basi dhambi hutendeka. Yale makubaliano kati ya Eva na nyoka yameleta majanga kwao na kwa kizazi kilichofuata. Eva anaacha kuongea na Mungu. Anatumia muda wake kuongea na nyoka na wanafikia muafaka kwenda kinyume na Mungu. Hapa twaona matumizi mabaya kabisa ya akili, uhuru, utashi na neema ya Mungu. Wao lakini (Eva na Adamu) walipata bahati kwani Mwenyezi Mungu aliwatafuta hata baada ya kosa lao. Lakini baada ya kuwahoji juu ya kosa lao na wao kusema kosa walilolifanya, anawawajibisha. Twaambiwa kuwa dhamiri hutuonya kama rafiki, lakini hutuhumu kama hakimu.

Katika Somo la Kwanza, tunaona muondoko wa taifa la Israeli toka Misri kwenda nchi ya ahadi – toka utumwa kwenda uhuru wa watoto wa Mungu. Yote yanawezekana kwa mkono wa nguvu wa Mungu. Ndicho anachofanya Yesu katika Injili, anashinda kishawishi na anaonesha uwezekano wa kushinda dhambi, toka utumwa kwenda uhuru wa watoto wa Mungu. Mwandishi wa barua kwa Waebrania 4:14 anasema ‘basi kwa kuwa tuna kuhani mkuu aliyekwisha penya mbingu, ndiye Yesu, Mwana wa Mungu, tuyashikilie maungamo yetu’.

Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha toba katika Kanisa Katoliki cha siku zipatazo 40 tangu Jumatano ya majivu mpaka siku kabla ya siku 3 kuu zinazotangulia Jumapili ya Pasaka au Jumapili ya ufufuko wa Bwana. Tunapofunga tunatakiwa kuzuia vilema vyetu na kuviacha kabisa, tunaomba kujaliwa moyo wa toba, tunainua mioyo yetu na tunaomba Mungu atujalie nguvu na tuzo. Haitoshi tu kukiri makosa yetu bali tunahimizwa kuungama na kutubu hayo makosa na kuwa tayari kuanza upya.

Nasi hatuna budi kujiangalia tena tunapoingia kwenye kipindi kingine cha Kwaresima. Je, ni yupi Ibilisi wako anayekuamrisha umpigie magoti? Ni mambo yapi tunayaamini mno na kuona kuwa ya maana zaidi na kuyapigia magoti ingawa yanapingana na mapenzi ya Mungu? Je, tunafanya matumizi mazuri ya akili, uhuru, utashi na neema aliyotujalia Mwenyezi Mungu? Tuombe sana neema na baraka yake Mungu ili kipindi hiki cha toba na mwito tena wa kuiamini Injili kizae matunda ya kimungu katika maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

07 March 2019, 16:04