Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anageuka sura: Ufunuo wa utukufu wa Mungu na mwaliko wa kuisikiliza sauti yake! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu anageuka sura: Ufunuo wa utukufu wa Mungu na mwaliko wa kuisikiliza sauti yake! 

Neno la Mungu, Jumapili II ya Kwaresima: Utukufu wa Mungu!

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima inamwonesha Kristo Yesu akigeuka sura mbele ya wanafunzi wake watatu na wanasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, "Huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikilizeni yeye kwani ni utimilifu wa Unabii na Sheria kutoka Agano la Kale. Utukufu wa Mungu umefumbatwa kwenye Fumbo la Msalaba!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mwanafalsafa Emmanuel Levinas alihuzunika sana baada ya kuona madhara ya unazi na dhuluma kwa utu wa mtu. Katika tafakari yake na akitaka kutoa jibu la suluhu ili jambo au hali hiyo isiendelee alialika watu wawe na uwezo wa kutazamana usoni/machoni. Aliaamini kwamba ubinafsi na kutokuthamini utu wa mtu ulikuwa ndiyo chanzo cha ukatili huo. Aliona kuwa kila mtu anajitazama peke yake, tena mtu akitaka kujiridhisha sura yake kama yuko safi hutumia kioo. Akaalika watu waache kujitazama wakitumia vioo kwani kioo hutumika kujiridhisha kwa jinsi utakavyo, kioo hakisemi na kualika watu wawe na ujasiri wa kutazamana usoni/machoni ili wawe na uwezo wa kuambiana ukweli, kujengana na kukosoana. Hatuna budi kujiuliza sana leo hii kama kweli tunafahamiana vizuri sura zetu?

Katika Injili ya leo tunaona Bwana wetu Yesu Kristo akibadilika sura. Anafunua utukufu wa kimungu mbele ya wafuasi wake. Bwana wetu anataka sisi ndugu zake tuwe au tuvae sura ya Mungu. Sura ya utukufu, sura ya uzima wa milele. Kadiri ya Biblia, mwili ni sehemu muhimu kwa mwanadamu. Mtu ni mwili pia. Mwili uliumbwa na Mungu, ukamwilishwa na kutakatifuzwa na Roho Mtakatifu katika ubatizo. Mtu wa biblia ametawazwa na utukufu huu wa kimwili. Katika Zab. 139:13.. tunasoma haya; maana wewe umeuumba mtima wangu, umeniunga tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa kuwa nimefanywa kwa namna ya ajabu ya kutisha. Mwili na roho vitakuwa na utukufu sawa. Mtu mmoja Charles Pequy anasema, siku ya mwisho, mwili na roho; au itakuwa mikono miwili iliyofungwa pamoja katika utukufu au viganja viwili vilivyofungwa pamoja utumwani.

Ndugu zangu, ukristo au niseme kuwa Kanisa Katoliki linafundisha wokovu wa mwili na si wokovu toka mwili kama walivyofundisha wafuasi wa mafundisho potofu kama “Manicheans” na “Gnostics” au baadhi ya dini nyingine au hata baadhi ya madhehebu ya wakati wetu huu. Wao huongea tu kuhusu roho na kudharau mwili. Sisi tunatafuta wokovu wa mwili na roho na si wokovu wa roho tu. Huku kugeuka sura Yesu ni dhihirisho wazi la hilo. Thamani ya tendo hili ni kwamba miili yetu iliyoharibika kwa dhambi itang’arishwa katika utukufu wake Bwana. Mwenyezi Mungu anampatia daima mwanadamu nafasi ya kumwona vizuri zaidi. Na katika kumwona Mungu, mwanadamu anapata uzima mpya. Mt. Ireneo anasema wazi, uzima wa kweli wa mtu uu katika kumwona Mungu.

Tukirudi katika masomo yetu katika somo letu la kwanza tunaona kuwa Mungu alipomwita Abrahamu toka nchi ya Baba zake, alimwahidi jina kubwa na uzao mkubwa. Wito huu wa Abrahamu ulifanyika katika sura ya 12:1-3. Sasa baada ya miaka kadhaa bado hana cho chote, yaani hana jina wala uzao, lakini bado anamwamini Mungu. Hapa tena nafasi ya Mungu inaonekana. Mungu hasahau ahadi aliyotoa. Daima Mungu anachukua jukumu kama ulivyo upendo wake – anaingilia kati. Na anapoingilia kati huwa anatoa wokovu na hapa kwa njia ya ahadi.

Katika sura ya hii ya 15 ya Kitabu cha Mwanzo tunaona jinsi Mungu anavyorudia ahadi yake kwa Abrahamu. Ila Abrahamu hana mrithi wala jina bado, hivyo anataka uhakika fulani ili kuonesha kuwa ahadi hizo zitatokea kweli. Mungu anamwonesha hilo kupitia ibada ya kuchoma wanyama. Kinachoonekana hapa na kuhitajika, kwa Abrahamu na kwetu (wakristo) ni imani kuwa Mungu hutimiza ahadi zake. Nabii Yer. 34:18 - anaonesha haja ya kuheshimu kiapo na kuwa waaminifu katika maagano yao, kushindwa kufanya hivyo tutagawanywa vipande vipande kama wale wanyama. Jamii mbalimbali za kiafrika hutimiza ahadi zao kwa maagano. Wako hata tayari kujitakia kila aina ya balaa iwapo hawatatimiza hayo – Zab. 7: 3-5, 137:5-6. Kwa kifupi katika sura hii tunaona habari juu ya ahadi na agano.

Hata katika hali hii ya wasiwasi, Abrahamu anaendelea kuamini katika Mungu ambalo ndilo jibu la kwanza na kinachotegemewa toka kwa mwanadamu. Mwitiko huu unabeba kukubali, kujitoa kwa Mungu anayeahidi na hapa imani kuu yahitajika. Katika Gal. 3:6-9 na Rom. 4:1-25, Mt. Paulo daima katika maisha yake aliishangaa imani hii kuu, ya namna hii ya Abrahamu. Wanyama kukatwa vipande viwili, kwaonesha kugawanyika kwetu ikiwa tutakiuka ukubali huo. Kule kupita katikati ya vipande vya wanyama, kwaonesha ukubali na kuratibisha agano. Hapa tunaona kama kawaida, Mungu anajiweka katika mstari wa wokovu. Anatuokoa, tukiitikia. Hilo giza kuu, lengo ni kuonesha Mungu anataka kufanya jambo kubwa kwa watu wake. Mungu anakuja kwetu. Ni vigumu kwetu kuelewa jambo hili ingawa twatakiwa kusema mapenzi yako yatimie hata katika wasiwasi na hofu zilizo mbele yetu – Ayu. 4:13-14.

Katika somo la pili tunaona jinsi Mtakatifu Paulo anavyokazia umuhimu wa hali ijayo kwa wale wanaomwamini Kristo. Paulo hasiti kusema niigeni mimi kwa vile yeye amemwiga Kristo ipasavyo. Anatualika kukumbuka kuwa sisi ni raia wa mbinguni. Anasisitiza juu ya haki ya kweli na hamu ya kuwa na Kristo. Huu ni mwaliko wa kuwa na imani thabiti huku tukitumainia ukamilfu wa mapenzi ya Mungu. Katika somo la Injili tunaona na kusikia juu ya utukufu wa Mungu – Yesu anageuka sura. Baada ya kuwaeleza juu ya kujikana na kuchukua Msalaba, anageuka sura. Ni ajabu kidogo kwani Yesu anaonesha kuushinda ulimwengu kwa kufa msalabani. Anageuka sura baada ya kuwaeleza masharti juu ya ufuasi – lazima kujikana, kuchukua msalaba na ikiwa hivyo basi uhakika wa kufika mbinguni unawekwa wazi.

Somo la Injili la leo linatupatia changamoto kubwa pia. Kina Petro wanashikwa na mshangao mkubwa, hawakuelewa. Mungu anaonesha utukufu wake, ila mwanadamu anashindwa kuulewa. Wao walilala usingizi, ila sauti ya Mungu inasikika. Kile kile kilichotokea wakati wa ubatizo wake Bwana – Lk. 3:22, ndicho kinajirudia tena hapa. Mungu anamweka wazi Yesu hadharani. Hapa imani yetu inaguswa tena leo. Ni kwa jinsi gani tunasikia sauti ya Mungu. Je tuko macho au usingizini? Je, sura zetu zikoje? Je, kipindi hiki cha Kwaresima sura zetu zitageuka?

Mtume Paulo katika Efe. 3:14-21 – anazungumzia uwepo wa mwaliko, uwezo wa kufahamu na kupenda fumbo hilo la Mungu ili Kwaresima hii izae matunda na hatimaye tuufikie uzima wa milele katika ufufuko na Kristo, yaani Pasaka ya mbinguni. Kwa sababu ya kukosa imani, Mtume Paulo analia juu ya maadui wa msalaba – wanaong’ang’ania mambo yao na mambo ya dunia. Mtume Paulo anataja sana fadhila za imani, matumaini na mapendo ingawa katika mfululizo tofauti. Paulo anasisitiza imani bila matendo ni bure na hakuna wokovu – Rum. 1:16 – Kristo amekufa bure kama mmoja angejiokoa kwa matendo yake mwenyewe. Baada ya kupata uaadilifu kwa imani ya Kristo, imani hiyo ni lazima izae matendo mema ya mapendo – 1Thes:1:3, Gal. 5:6. Ndiyo sababu kila mmoja atahakumiwa kwa kadiri ya matendo hayo ya mapendo – Rum. 2:6.

Maisha ya mkristo ni maisha ya imani, yenye msingi wake katika Neno la Mungu – na anayelishwa na Neno la Mungu anao uzima wa milele. Njia kuu ya kushinda vishawishi na dhambi ni kusikiliza Neno la Mungu – ili kuwa na uwezo wa kukataa vishawishi vya shetani. Ufahamu huu ndiyo mwanzo wa kugeuka sura na kuanza upya. Mhimili wa Kwaresima ni  kusikiliza Neno la Mungu = neno la ukweli, kuishi, kusema na kutenda ukweli na kukataa uongo ambao ni sumu kali inayoharibu ubinadamu wetu, sura zetu na mahusiano yetu na Mungu na wenzetu na ambao pia ni mlango wa dhambi zote. Tumsifu Yesu Kristo.

13 March 2019, 14:48