Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III Kipindi cha Kwaresima: Mapenzi ya Mungu, toba na wongofu wa ndani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III Kipindi cha Kwaresima: Mapenzi ya Mungu, toba na wongofu wa ndani! 

Kwaresima: Jumapili III: Musa anaitwa na kutumwa kuwakomboa watu

Katika sura hii ya tatu ya Kitabu cha Kutoka tunaona ufunuo wa Mungu, tangazo la mpango wa ukombozi na wito wa Musa. Ujio huu unaonesha hali ya Mungu katika tendo la ukombozi. Musa lakini anapata wasiwasi – kazi hii ni ngumu ila bahati yake ni kuwa Mungu anajifunua! Huu ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa njia ya utakatifu wa maisha!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma

Mtu mmoja alimwuliza padre ni jinsi gani ajitolee maisha yake yote kwa Mungu au jinsi gani afanye ili apate kuongoka. Yule padre alitoa karatasi nyeupe isiyoandikwa cho chote na kumwambia inatosha kuandika jina lako na kuweka saini chini/sehemu ya chini ya karatasi na kumwachia Mungu ajaze mapenzi yake sehemu iliyobaki wazi. Nasi pia hatuna budi kumwachia Mungu aandike upya ukurasa wa maisha yetu. Hilo ndilo dai mojawapo la maisha mapya ya kwaresima la kukesha na kuongoka. Kumwacha Mungu aandike upya ukurasa wa maisha yetu.

Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima. Katika tafakari yetu dominika ya pili, tulialikwa kuyatambua mapenzi ya Mungu na utukufu wake. Tuliona jinsi Mungu anavyotimiza ahadi yake na jinsi anavyoonekana katika sura yake halisi mbele ya wafuasi wake. Nasi tukaalikwa kuangalia sura ya imani yetu, ufuasi wetu na maisha yetu kama yanabeba sura ya kimungu. Hiyo sura mpya ya Mungu tunayopaswa kuwa nayo kipindi hiki cha kwaresima, huo ufahamu ambao unawekwa mbele yetu leo hii twaalikwa kuuwajibikia au kuufanyia kazi. Na ndiyo wito wa neno la Mungu dominika hii ya leo.

Katika Neno la Mungu dominika hii tunaona haja ya kukesha na kuongoka. Katika somo la kwanza leo, tunaona ufunuo wa Mungu kwa Musa na tangazo la mpango wa Mungu wa kuwakomboa Waisraeli toka utumwani. Mungu anajifunua kwa Musa, hata kutaja jina lake. Tukio hili linafanyika chini ya mlima Sinai, mahali walipoitwa Waisraeli. Musa anaishi maisha ya jangwani na Mungu anamtumia katika mazingira yake hayo kwa kazi ya baadaye. Katika sura hii ya tatu ya Kitabu cha Kutoka tunaona ufunuo wa Mungu, tangazo la mpango wa ukombozi na wito wa Musa. Ujio huu unaonesha hali ya Mungu katika tendo la ukombozi. Musa lakini anapata wasiwasi – kazi hii ni ngumu ila bahati yake ni kuwa Mungu anajifunua

Katika somo la pili tunaona mtume Paulo anatumia mfano wa historia ya Kutoka kuwaonya wakristo Wakorintho juu ya maisha yao ya kikristo. Mtume Paulo anasema haitoshi tu kusema naamini katika Kristo, hatuna budi kumfuata, kuwa wafuasi kweli. Katika somo la Injili tunaona mwito wa mwinjili Luka wa kubadilika. Sehemu hii ya maandiko matakatifu imeandikwa na mwinjili Luka tu. Tukio hili lilitokea wakati Wagalilaya walipokuja Yerusalemu kutoa sadaka na wakauawa na majeshi ya Pilato. Pia habari ya wale 18 waliouawa halipo katika injili nyingine isipokuwa katika Luka tu. Mnara wa Siloam ulikuwa katika kona ya kusini na mashariki ya mji. Ulivunjika wakati Pilato akiimarisha kuta ili kuongeza kiwango cha maji huko Yerusalemu.

Inasemekana kuwa habari hii ilitajwa ili kumtaka Yesu awake hasira dhidi ya Pilato ili wapate sababu ya kumshitaki. Aidha Yesu anatumia nafasi hii ili kuonesha haja ya kukesha na kuongoka. Na Yesu anathibitisha fundisho lake akitaja hali ya mtini usiozaa matunda n.k. Hakika hatuna budi leo kukagua mpango wetu wa kwaresima na kuona kama unaendelea vizuri. Tukumbuke kuwa kipindi cha Kwaresima huanza kwa kupakwa majivu utosini au kwenye paji la uso. Maana yake nini? Alama hii yatukumbusha kuwa mwili wa mwanadamu u katika hali ya uharibifu na ukomo – alama hii ikituelekeza kwenye matumaini makuu. Tunaishi tukitambua kuwa sisi si kitu na ulimwengu huu ni mahali pa kupita tu. Tunakiri na kukubali waziwazi mbele ya Mungu Baba Muumba wetu na mbele ya wenzetu kuwa sisi tumepungukiwa. Ni majivu tu. Lakini huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tunakiri dhambi zetu.

Mtu mmoja anafanya tafakari hii: majivu ni masalio ya moto, makazi yake jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya kuwa nyeupe pe. Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya majivu. Majivu yatufanye tuwe weupe. Pia mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya haya tunayasikia/tumeyasikia kila tunapopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima, ni mwaliko wa kuelekeza matumaini yetu katika neno la Mungu, ni mwaliko ili tuongoke, tuanze maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.

Leo twaona tena Yesu akiongea habari ya jambo lililo kati yetu. Yohanie alikuwa akiongea juu ya jambo lijalo. Na zaidi sana, tunakumbushwa kile tulichotamka siku tunaanza kipindi cha Kwaresima, tubuni na kuiamini injili – Mk.1:15. Huu ni mwaliko wa uzima, wa kutaka kuanza upya. Sote twajua kuwa ni vigumu kuacha mazaoea yetu lakini daima twaona jinsi anavyotuhimiza kufanya mabadilko ya ndani – Lk. 9:23 – kujikana nafsi na kuchukua msalaba, Lk. 16:16 – habari juu ya sheria ya Musa na sheria mpya ambayo hatuna budi kutumia nguvu kuingia ndani.

Ndugu zangu, wito wa Mungu kwetu sisi ni kuwa tayari kumtumikia. Musa anaitwa na anaambia avue viatu vyake. Atoke katika mazingira yake aende apeleke habari ya ukombozi kwa taifa lake. Sisi nasi tunaalikwa kutoka katika mazingira yetu na kuwa tayari kumtumikia Mungu. Wito umewekwa wazi na somo la injili ukitualika kubadilika na kuongoka, kuwa tayari kuvua hali zetu za kibinadamu na kuvaa viatu vya Mungu na kuwa tayari kumtumikia. Maisha ya mkristo ni maisha ya imani, yenye msingi wake katika Neno la Mungu – na anayelishwa na Neno la Mungu anao uzima wa milele. Njia kuu ya kushinda vishawishi na dhambi ni kusikiliza Neno la Mungu – ili kuwa na uwezo wa kukataa vishawishi vya shetani.

Tukumbuke kuwa hatuwi wakristo kwa hiari yetu bali ni neema ya Mungu inayofanya kazi. Hata maendeleo yetu ya ukristo hayategemei nguvu zetu wenyewe. Ni upendo wa Mungu unaotujalia nguvu. Somo la kwanza laeleza wazi jambo hili. Twasikia habari juu ya Mungu aliye kati yetu. Uwepo unaofanya mageuzi na uongofu uwezekane kila siku. Sisi nafasi yetu ni kusikia sauti ya Mungu na kutimiza mapenzi yake. Katika kipindi cha kwaresima wakristo wanaalikwa kutafakari sana fumbo la wokovu wa Kristo na kuishi ubatizo wao kwa undani kabisa. Ni siku 40  za utakaso. Tumsifu Yesu Kristo.

21 March 2019, 16:57