Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma ya Mungu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima: Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma ya Mungu!  (AFP or licensors)

Tafakari ya Neno la Mungu: Kwaresima: Toba na Upatanisho!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anawaalika waamini kutafakari kuhusu Injili ya huruma ya Mungu, kwa mfano wa Baba mwenye huruma, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia na kuambata Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani! Hii ni tiba ya maisha ya kiroho!

Na Padre Reginald Mrosso - Dodoma.

Ndugu zangu karibuni tena katika tafakari ya Neno la Mungu dominika hii ya nne ya Kipindi cha Kwaresima. Tumesikia juma lililotangulia juu ya wito wa Mungu kwetu sisi wa kuwa tayari kumtumikia. Musa anaitwa na anaambia avue viatu vyake. Atoke katika mazingira yake aende apeleke habari ya ukombozi kwa taifa lake. Sisi nasi tukaalikwa kutoka katika mazingira yetu na kuwa tayari kumtumikia Mungu. Wito uliwekwa wazi na somo la Injili ukitualika kutubu na kuongoka, kuwa tayari kuvua: utu wetu wa kale; hali zetu za kibinadamu na kuvaa viatu vya Mungu na kuwa tayari kumtumikia katika ukweli, haki na utakatifu wa maisha!

Leo tunasikia kuhusu kukubali au kukiri kosa ili kupata msamaha. Si jambo rahisi kibinadamu ingawa inawezekana. Tumepata bahati wakati wetu huu kushuhudia uwezekano huo. Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini aliunda kamati ya haki, amani na maridhiano kitaifa. Mbele ya wengi ilionekana kitu kigumu na hatari lakini mwishoni ilitoa mafanikio makubwa. Ni mahali hapa mtenda maovu na aliyetendewa maovu walipata nafasi ya kukutana uso kwa uso, kukaa pamoja, mmoja akakiri kosa lake dhidi ya mtendewa, kuomba msamaha na msamaha kufikiwa.

Tunaambiwa kuwa katika kamati hii, mama mmoja alikutana na askari wa kibaguzi aliyemuua mume wake na mtoto wake. Baada ya yule jamaa kujieleza na kuomba msamaha ilifika wakati wa mtendewa kutoa msamaha. Kila mmoja katika kamati hakujua yule mama atadai kitu gani. Wakati huo yule mkosaji alikuwa kifungoni gerezani. Yule mama alisimama na akaanza kueleza uchungu uliompata, jinsi mume wake na mtoto wake walivyouawa na yule askari mbele ya macho yake. Pia akaeleza jinsi alivyompenda mume wake na mtoto wake. Akaeleza pia furaha aliyokuwa nayo akiwapikia chakula na machungu aliyonayo kwa kukosa mtu wa kumpikia chakula. Akaomba kamati imruhusu kama njia ya msamaha kupika chakula na kumpelekea yule askari mfungwa gerezani kila siku mpaka mwisho wa maisha yake kama alama ya kumkumbuka mume wake na mtoto wake. Watu wote kwenye kamati walibaki vinywa wazi na furaha ya msamaha ikatawala ukumbi wote. Ukweli na uwazi ukazaa msamaha na hali mpya ya maisha.

Sote twafahamu kuwa tendo la upatanisho ni jambo gumu sana kwani hata mtenda jema aweza kuonekana tishio mbele ya baadhi ya watu. Angalia Injili ya leo – linaanza shitaka –  huyu hula na wenye dhambi. Jibu la Yesu ni kuwa Mungu humpokea bado mdhambi na kumpa nafasi ya kutubu dhambi na hatimaye, kumwongokea Kupatana na adui ni kitu kigumu sana kwa mwanadamu. Tunaona jinsi watu wanavyohangaika kulipa kisasi kwa waliowakosea. Au jinsi mtu anavyohangaika kutafuta haki ikiwa amekosewa. Lakini kutafuta haki huku hupelekea pia hata kumdhuru mwingine. Hutokea pia hata hilo hitaji la kutafuta haki likaongeza uadui zaidi. Katika somo la kwanza tunaona jinsi watu wanavyohangaika kulipa kisasi.

Mtoto mmoja mdogo alisikika akisali hivi – utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wale waliokufa dhidi yetu. Tunaambiwa kuwa msamaha wa kweli huanza toka ndani. Mtume Petro alipomwendea Yesu na kuuliza habari ya msamaha anatufundisha jambo kubwa sana. Tukisoma Mt. 18:21 – kuhusu kusameheana – kisha Petro akamwendea, akasema, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Mtume Petro hakusema aliyenikosea aniombe msamaha mara ngapi Kadiri ya mafundisho na mapenzi yake Mungu, tiba sahihi ya ugomvi ni upatanisho, pamoja na ugumu wake ulivyo. Mungu ametaka upatanisho nasi na kati yetu wenyewe.

Masomo yetu ya leo yaonesha mapenzi ya Mungu juu ya upatanisho. Kinachoonekana wazi ni kuwa ili upatanisho utokee ni lazima Mungu aingilie kati. Sisi tunaalikwa kushiriki katika tendo hili. Hili liko wazi katika somo la kwanza na la pili. Mtume Paulo anasema mpatanishwe na Mungu. Na anasema kwa vile sisi ni watu wake Bwana, sisi ni viumbe vipya. Tendo halisi la upatanisho hutoka kwa Mungu, kwa njia ya mwanawe na katika mstari wa 18 wa somo hili la pili tunasoma kuwa naye anatupa sisi huduma ya upatanisho. Mtakatifu Fransisko wa Assi husali katika sala zake ‘Ee Bwana unifanya chombo cha amani yako”. Hivyo huu unakuwa ni wajibu na si hiari. Katika somo la kwanza tumeona kuwa Mungu yuko daima na anawakumbusha watu wasahau ile hali ya utumwa na waishi kama watu huru. Tendo la upatanisho lina asili yake ndani ya Mungu na sisi watoto wake tunapaswa kuwa watu wa upatanisho. Mtume Paulo anasisitiza haja ya mwanadamu kuupokea huu upatanisho.

Abraham Lincoln, Rais wa 16 wa Marekani anatupata uwezekano wa kuishi msamaha na upatanisho. Wakati akifanya kampeni alitokea mpinzani aliyefanya kila aina ya mbinu ili kuharibu jina na sifa yake. Huyu aliitwa Edwin McMasters Stanton. Alikuwa tayari kufanya lo lote ili Lincoln asipate nafasi ya kushinda uchaguzi wa urais. Hata hivyo Lincoln alishinda na alipokuwa anaandaa baraza la mawaziri jina la Stanton likawepo. Wasaidizi wa rais walifanya juhudi kubwa ila bila mafanikio kumweleza rais chuki ya Stanton dhidi yake. Rais alionekana kuzijua wazi mbinu mbaya za Stanton dhidi yake wakati wa kampeni. Rais akasema huyu ananichukia mimi ila siyo Marekani. Huyu ana sifa za kuongoza Marekani na  watu wake. Akamfanya waziri wa ulinzi na akaifanya kazi ile kwa weledi mkubwa. Lincoln aliuawa. Wakati wa maziko yake Stanton alisema hakika huyu asingeondoa chuki yake dhidi yangu, leo hii angezikwa akiacha adui duniani. Lakini kwa vile roho yake ilikuwa tofauti na yangu ameacha rafiki duniani.

Habari ya Baba mwenye huruma katika somo la Injili nayo yatupa changamoto kubwa. Lakini kubwa zaidi ni ile roho ya yule mtoto kutambua na kukiri kosa. Anaamua kufunga safari ya kurudi kwa baba na kuomba msamaha. Huyu anajitambua na kukiri kosa lake. Wengi wetu hatuwezi kufikia hali hii ya juu kabisa ya kiroho. Ilitokea siku moja mfalme mmoja alitaka kutoa msamaha kwa mmoja kati ya wafungwa katika gereza.. Yeye alitaka kutoa msamaha kwa mfungwa atakayezungumza wazi kile kilichomsibu. Kila mfungwa alidai kuwa ameonewa na hakutendewa haki kuwa pale gerezani. Mwishoni kabisa akatokea mfungwa mmoja aliyetamka wazi kosa lake na kukubali kuwa kuwepo kwake pale gerezani ilikuwa sawa kabisa. Huyu alikiri kosa lake. Mfalme akamwamuru bwana jela kumfungua pingu yule mfungwa na kumwacha huru kwa vile alikiri kosa lake. Wengi wetu hatufikii hatua hii ya kukiri na kukubali makosa.

Na hii inagharimu sana maisha yetu na mahusiano kati yetu na Mungu. Habari ya kaka anayechukia kurudi kwa ndugu yake inasikitisha sana. Pengine anawakilisha hali zetu sisi ambao hatuko tayari kutoa msamaha. Kwake huyu ndugu yake alikuwa tayari adui. Tunakumbushwa kuwa hatuna budi kuwa tayari kuukubali msamaha wa baba kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine.

26 March 2019, 15:22