Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Jitihada za kushinda vishawishi na majaribu! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima: Jitihada za kushinda vishawishi na majaribu! 

Tafakari ya Neno la Mungu: Shindeni vishawishi na majaribu!

Katika mazingira ya upweke Shetani anamjaribu na kumshawishi Yesu avunje uhusiano wake na Mungu katika mpango mzima wa ukombozi. Vishawishi alivyopambana navyo Yesu kwanza ni kutafuta heshima au sifa. Pili ni ukuu au utawala-nitakupa mali hii kama ukiniabudu, na tatu mamlaka-amuru jiwe hili liwe mkate. Hivi ndivyo vinavyotutenga na kutuweka mbali na Mungu wetu!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika kipindi cha kwaresima mwaka C wa Kanisa. Leo tunaadhimisha dominika ya kwanza ya kwaresma katika kipindi hiki cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi maalum cha mapambano ya kiroho dhidi ya mapungufu na madhaifu yetu ya kibinadamu licha ya kuwa mapambano haya ni ya kila wakati lakini katika kipindi hiki cha kwaresma yanapewa nafasi ya pekee zaidi.

Ni kipindi cha kukuza fadhila mbalimbali kama vile haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga muunganiko na Mungu wetu mtakatifu katika kuwatumikia ndugu zetu waliodhaifu na wahitaji yaani kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kuwasaidia maskini zaidi. Kipindi hiki cha Kwaresima ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi. Kwa hiyo kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi tulichokianza siku ya Jumatano ya Majivu tulipopakwa majivu katika paji la uso, tendo ambalo kimsingi ni la kiroho na ishara ya toba ya kweli. Tendo hilo linatufanya tutambue ya kuwa sisi ni jumuiya ya wakosaji tunaohitaji kufanya toba ya kweli, kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu ndani ya kanisa.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kishawishi ni mvuto au msukumo kutoka ndani yetu au nje. Tunavutwa au kusukumwa kutenda jambo zuri au baya. Vishawishi, mara nyingi hutujia katika namna mbili: Kwanza, tunasukumwa na vionjo vya miili yetu. Miili yetu inawaka tamaa mbalimbali kama vile kula, kunywa, kuvuta, kupenda, kupendwa, au kufanya chochote kile ambacho mwili unadai ufanye na kukusukuma kutoa uamuzi. Pili, tunashawishiwa na kuvutwa na watu wengine kutenda jambo fulani. Ushauri huo unaweza kuwa mzuri au mbaya.

Yesu baada ya Ubatizo wake, anaongozwa na Roho Mtakatifu mpaka jangwani, kama Waisraeli walipotolewa katika utumwa wa Misri walivyopita jangwani kuelekea nchi ya ahadi, anafunga kwa siku 40, kuwakumbusha Waisraeli walivyokaa jangwani miaka 40, Musa alivyokaa mlimani siku 40, gharika ilivyochukua siku 40, Waninawi walivyofunga siku 40 ikimaanisha kipindi cha kutosha cha kufanya maandalizi kwa ajili ya jambo zito litakalotukia na kupokelewa. Huko jangwani Yesu anafunga na kusali ili kujipatia nguvu ya kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi.

Katika mazingira hayo ya upweke Shetani anamjaribu na kumshawishi Yesu avunje uhusiano wake na Mungu katika mpango mzima wa ukombozi. Vishawishi alivyopambana navyo Yesu kwanza ni kutafuta heshima au sifa – jitupe chini toka hapa hutaumia maana imeandikwa atakutumia malaika zake wakulinde usijejikwaa, pili ni ukuu au utawala-nitakupa mali hii kama ukiniabudu, na tatu mamlaka-amuru jiwe hili liwe mkate. Hivi ndivyo vinavyotutenga na kutuweka mbali na Mungu wetu mtakatifu. Yesu alivishinda vishawishi hivi na majaribu hayo akasonga mbele na kazi ya kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso nasi tunafurahia ushindi huo.

Katika jaribu la kubadili jiwe kuwa mkate, shetani anamshawishi Yesu abadili mwelekeo wa kazi yake ya kumkomboa mwandamu kutoka utumwa wa dhambi, kuelekea zaidi katika utumwa wa mahitaji ya kimwili kwa kumwambia afanye muujiza wa kubadili jiwe kuwa mkate ambao ndio mahitaji ya kila siku. Ni wazi hakuna maisha bila chakula cha kimwili. Lakini Yesu anatufahamisha kuwa binadamu si mwili tu ana roho ndani mwake na roho ndiyo itiayo uzima, hivyo hatuishi kwa mkate tu, yaani mahitaji yetu ya kimwili peke yake bali tunahitaji pia chakula cha kiroho tunachokipata kwa kufanya anayotuamuru Mungu, ndiyo maana Yesu anasema; “chakula changu ni kuyafanya mapezi ya Mungu”. Jaribu hili la miujiza limetushika kwelikweli wakristo wa sasa.

Kama Wana wa Israeli walivyamjaribu Mungu walipokuwa jangwani wakihitaji ishara na miujiza toka juu, kizazi chetu cha sasa kinalilia miujiza. Fikiri madhehebu na vikundi vya wana maombi vinavyoibuka na kudai wanafanya miujiza ya uponyaji wa magonjwa, kuvunja mti wa ukoo, kutoa ugumba au kupata mtoto baada ya kuharibu vizazi kwa utoaji mimba na madawa ya kuzuia mimba, na usipopona unahama kwenda dhehebu lingine ambapo ukidhani Mungu atakusikiliza. Tunalilia miujiza ya kupata kazi na mafanikio bila kufanya kazi, kufaulu mitihani hata bila kusoma, tunahitaji muuujiza wa kupanda cheo hata ukiwa na elimu ndogo, kupandishwa mshahara wakati vigezo hauna, wakati huo vyeo vyao hawa wanamiujiza havijulikani, wanasahau hata Kristo mwenyewe wanaotumia jina lake hakuwaponya wenye pepo na kuwatakasa wakoma wote wakati wake na hawajiulizi ni kwanini?

Lakini cha ajabu hawawezi kwenda kwenye vituo vya walemavu, wakoma, viwete na viziwi wawaonee huruma, wakawaponye ili waondokane na mateso hayo. Huku ni kumpa Mungu nafsi ya pili, Yesu Kristo masharti ya kumfuata na kumwamini tunamwambia kama wataka niwe mfuasi wako fanya muujiza. Kwaresima hii tufanye mabadiliko, tumrudie Mungu, tufanye toba ya kweli, tutapata Baraka na kibali machoni pa Bwana Mungu wetu. Jaribu la kutafuta mamlaka, kupenda vitu kuliko kumpenda Mungu. Kule jangwani wana wa Israel walichoka kumwabudu Mungu wakajitengenezea mungu wao, ndama wa dhahabu. Yesu hakudhubutu kuabudu miungu mingine, wala mamlaka za kisiasa au utajiri na mali alizoahidiwa na shetani.

Kristo Yesu alibaki mwaminifu kwa sauti na maelekezo ya Mungu Baba, akiwa mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na mtiifu kwa Mungu, rafiki wa watoto, maskini na wanyonge, na sasa anafurahi milele yote mbinguni. Je kizazi chetu sasa kikoje. Kinatafuta mamlaka, ufahari, na nguvu kwa kila namna hata kwa nguvu za giza na mauaji ya watu wasio na hatia. Kwaresima hii tusali na tufunge kwa ajili ya dhambi za mauaji ya kinyama kwa binadamu hasa wasio na hatia yanayofanyika kwa majina ya vita, uharamia, ugaidi, uenezaji wa dini kwa kujitoa muhanga, tusali na kufunga kwa ajili ya wanaojitenga na Kanisa kwa kudai wanakarama hasa za kunena kwa lugha na uponyaji.

Tusali na kufunga kwa ajili ya wanaharakati wa ndoa za njinsia moja, ushoga na usagaji, huku wakidai haki ya kuasili watoto, tusali na kufunga kwa ajili ya makahaba ili wamrudie Mungu kwani Yesu anatuambia pepo wa namna hii hawatoki isipokuwa kwa kusali na kufunga. Tusali na kufunga kwa ajili ya wanaotafuta mali kwa njia zisizo halali ambao Yakobo katika waraka wake kwa watu wote 5:2-4 anawakemea kwa ukali sana akisema: “Basi sikilizeni, ninyi matajiri mliojikusanyia mali ambazo ninyi wenyewe hamwezi kuzimaliza, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo.

Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itakuwa ushuhuda dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu kama vile ya dawa za kulevya, dawa za kuzuia na kutoa mimba chini ya mwavuli wa uzazi wa mpango, makasino, madanguro, na mengine kama hayo) mliowanyonya kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji (ambao ni maskini, watoto, wajane, yatima, vijana hasa wa kike ambao ni wahanga wa kwanza wa biashara haramu ya binadamu mnaowafanyisha kazi za kuwadhalilisha katika mashamba hayo tuliyoyataja) vimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha kwa karamu zenu kama ndama wa Mediani.

Mmewahukumu na kuwauwa watu wenye haki, ambao walikuwa hawapingani nanyi bali na mwovu shetani lieni na kuomboleza, mrudieni Mungu kwa mioyo yenu yote mkizingatia haki na kutenda mema. Na hii ndiyo kwaresma yenyewe ambayo Jumatano ya majivu nabii Yoeli alituasa tuifanye toba ya kweli kwa kurarua mioyo yetu wala si mavazi yetu kwa kufunga na kuomboleza. Majaribu ya Yesu ni kielelezo cha majaribu yote tunayokutana nayo kila siku katika safari yetu ya kuelekea mbinguni. Hakuna hata mmoja kati yetu atakayemaliza maisha ya hapa duniani bila magumu au majaribu yoyote. Udhaifu wetu wa kimwili kama njaa, kiu, uchovu, wivu au tamaa ni majaribu ambayo yanatupatia mahangaiko, huzuni na ugomvi mkubwa kati yetu.

Vipawa tulivyo navyo kama elimu, uwezo wa kuongea, cheo, au kuponya hutufanya tuwe na majivuno na kusababisha masengenyo, utengano na mauaji makubwa. Hivi kutokana na uwezo au nafasi tulizonazo katika maisha wengine tunajiona ni wa maana sana kuliko wengine na hivyo tutananyanyasa na kuwakatilia mbali kabisa. Hayo yote hutokana na vishawishi vya mali, heshima na mamlaka. Tunapoanza mfungo wetu wa kwaresma tutambue kuwa tunakabiliwa na vishawishi vingi vya kila aina. Tunaalikwa leo kuvitambua vishawishi hivyo na tuwe tayari kukabiliana navyo. Kiongozi wetu Kristo aliyashinda majaribu yote. Nasi tukimtegemea Mungu tutashinda hayo yote pia.

Tunaweza kuepuka vishawishi endapo tunasali daima, tunafunga, tunatenda matendo ya huruma, tunatenga muda wa kuongea na Mungu, tunashiriki Misa Takatifu na kupokea Sakramenti hasa kitubio na Ekaristi pasipo unafiki na kufuru. Basi tuendelee kujiweka chini ya maongozi ya Mungu tukiomba neema na msaada wake ili tudumu katika imani yetu ili Kristo atakapofufuka tufufuke naye tutoke katika makaburi ya dhambi zetu tuuridhi ufalme wa mbinguni tuliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Tumsifu Yesu Kristo.

Kwaresima J1

 

07 March 2019, 16:36