Cerca

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu ni Mwana mpendwa wa Mungu, Msikilizeni yeye! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya II ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu ni Mwana mpendwa wa Mungu, Msikilizeni yeye! 

Neno la Mungu, Jumapili II ya Kwaresima: Mwana wa Mungu

Kristo Yesu anang'ara mbele ya wafuasi wake, ili kuwaimarisha zaidi kuweza kulipokea Fumbo la Msalaba yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wake unaoleta ukombozi, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu! Ili kutekeleza dhamana na utume huu, wafuasi wake, wanapaswa kuwa wasikivu na watekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya kipindi cha kwaresma mwaka C wa Kanisa. Zimepita siku kumi na mbili tangu tuanze kipindi hiki cha majiundo yetu ya kiroho kwa kujikatalia na kujinyima yale tuyapendayo kwa ajili ya wengine ili tujipatanishe na Mungu. Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva la kukaidi maagizo na amri za Mungu, walipoteza neema ya utakaso, sura ya Mungu ndani mwao na mahusiano mazuri na Mungu Baba. Walichokipoteza Adamu na Eva ndicho tulipokipoteza nasi kwani ubinadamu wetu ulikuwa tayari kwao.

Hata hivyo Mungu kwa upendo wake hakuwaacha wapotee, mara nyingi na kwa namna mbalimbali kwa njia ya viongozi mbalimbali hasa Manabii ametuita kila mara tumrudie lakini hatukuwa wasikivu hatimaye akamtoa na kumleta mwanaye wa pekee ndiye Mkombozi wetu yesu Kristo aliyeteseka, akafa, akazikwa siku ya tatu akafufuka ili arudishe tena uhusiano wetu naye. Leo hii Mungu anamdhihirisha kwetu mlimani Tabor katika wingu akisema “Huyu ni mwanangu mteule wangu ninayependezwa naye, msikieni yeye”. Mungu anatutaka tuwe wasikivu kwa maongozi ya mwanaye mpendwa basi nasi tuvunjevunje roho ya ukaidi tuwe wasikivu ili tuweza kumpendeza Mungu kama wanawe wapendwa.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Katika somo la kwanza Mungu anafanya agano na Abrahamu baba wa imani. Alama na ishara ya agano hili ni moto uliopita juu ya nyama alizoziandaa Abrahamu. Moto huu ni alama wazi ya uwepo wa Mungu anayefunga Agano na Abrahamu naye hapaswi kulivunja agano hili. Katika somo la pili, Mtume Paulo anawaonya Wafilipi wajiadhari na wale wanaotaka kuwashurutisha washike torati ya Wayahudi ili wawe wakristo, wafuate mfano wake aliyeweka tumaini lake kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

Injili inatupa simulizi la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo mlimani wakati wa kusali akiwa pamoja na wanafunzi wake watatu; Petro, Yohane na Yakobo. Tukio hili lilitokea huko mlimani Tabor, baada ya ungamo la Petro kuwa Yesu ni mwana wa Mungu (Mk 8:29) na ni majuma machache tu kabla ya mateso. Katika tukio hili la kung’ara sura kwa Bwana wetu Yesu Kristo tujiulize maswali yafuatayo: Kwanini Yesu aliwachukua wanafunzi watatu tu na sio wote? Kwanini aligeuka sura mbele yao? Uwepo wa Musa na Eliya na baadae kutoweka maana yake ni nini?

Kwanini wanafunzi watatu? Wanafunzi hawa ndio walioshuhudia kufufuliwa kwa binti Jairo (Mk 5:37), na ndio watakao shuhudia mateso ya Yesu kule Gethsemane (Mk 14:13). Kabla ya tukio la kugeuka sura, Yesu alitoa utabiri juu ya Mateso yatakayompata. Wanafunzi hawakuelewa na walikwazika kiasi kwamba Petro akasema: Hasha Bwana hayo hayatakupata na Yesu anamkemea Petro na kumwambia rudi nyuma yangu shetani wewe maana unawaza ya binadamu sio ya Mungu (Mt. 16:22). Kwa hiyo Yesu kuwachukua hawa wanafunzi watatu alitaka aimarisha ndani yao mambo matatu yaani imani, matumaini, na mapendo. Petro akiwa papa wa kwanza alipaswa kuwa na imani dhabiti na imara.

Ndiyo maana baadaye alikuja kusema hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu wa watu tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake bali tulikuwa tumeona wenyewe ukuu wake (2Pt. 1:16…) Pili; Yakobo alikuwa wa kwanza kati ya mitume kuteswa na kufa shahidi kwa ajili ya Bwana hivyo alipaswa kuwa na matumaini makubwa ya maisha yajayo. Tatu; Yohane aliyeandikiwa kuwa mlinzi wa mama yetu Bikira Maria, alipaswa kuwa na mapendo makubwa na safi. Hivyo lengo ni kuwaimarisha kwa kuwaonesha utukufu wake ili wakati wa majaribu wasitetereke bali wawaimarishe mitume wenzao na kwamba wasipoteze imani, matumaini na mapendo kwa mwalimu wao.

Kwanini Mbele yao? Kuwafundisha kuwa utukufu unapatikana katika kuvumilia mateso. Lakini pia kwa mila na desturi za wayahudi, ushahidi wowote wa jambo kubwa na zito ili uweze kukubalika ilibidi utolewe na wanaume wawili na kuendelea (ushahidi wa wanawake na watoto haukuwa halali). Kwa hoja hii Yesu anapanda mlimani na mitume watatu. Ndiyo kusema tukio hili linakidhi vigezo vya sheria kwamba tukio hilo kweli lilitokea. Hivi hata sisi leo tusiwe na wasiwasi juu ya hili.

Kwanini Musa na Eliya? Hawa ni watu muhimu sana katika Agano la Kale. Musa anawakilisha Torati ama sheria, na Eliya anawakilsha manabii. Torati na manabii kwa pamoja zinajenga msingi wa utabiri wa ujio wa masiha Yesu Kristo.  Bila ufunuo huu wa torati na manabii katika Agano la Kale Yesu angekuwa fumbo lisiloweza kufumbulika. Ndiyo maana baada ya ufufuko wake ili kuwafanya wanafunzi wawili wa Emmaus waelewe maana ya kifo na ufufuko wake atahitaji kuelezea Agano la Kale: akianzia na Musa kama kiongozi na nabii wa kwanza na manabii wote akawaeleza katika Maandiko mambo yote yaliyo mhusu yeye mwenyewe (Lk 24:27).

Pia wingu jeupe kutokea juu ya mlima ambako ndiko ilikotoka sauti ikisema huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye inaashiri uwepo wa Mungu kwani katika Agano la Kale wingu lilimaanisha uwepo wa mwenyezi Mungu. Baada ya maneno hayo kumalizika, Musa na Eliya walitoweka. Nini maana ya kutoweka kwa Musa na Eliya? Hapa Mungu anataka kutuambia kwamba wakati wa kuwasiliana naye kwa njia yao, yaani Musa na Eliya kama viongozi na manabii umekwisha. Na sasa anataka tuongee naye moja kwa moja kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo.

Petro alipoona sura mpya ya Bwana wake alipata msisimko mkubwa hata ukamfanya atake kujenga vibanda vitatu; kimoja cha Musa cha pili cha Eliya na cha tatu cha Yesu. Wazo la Petro nasi tunaalikwa kulifanyia kazi yaani tujenge vibanda vitatu leo. Tujenge kibanda cha Musa: Kwa kuiga mfano wa nabii Musa aliyekuwa rafiki wa Mungu, nabii mkuu mwombezi na mtetezi wa taifa la Mungu nasi tuwe marafiki wa Mungu.Yatupasa tumpende Mungu kwa moyo wetu wote kwa akili yetu yote na kwa nguvu zetu zote kama Musa alivyompenda. Na kama Musa tuwe watetezi na waombezi wa wakosefu na wanyonge mbele za Mungu.

Tujenge kibanda cha Eliya: Tuige mfano wa nabii Eliya aliyekuwa kiongozi mzuri mwenye kuliongoza taifa bila kuwaogopa wafalme waliokuwa na mioyo migumu na mwenendo mbaya. Hata sisi leo katika jumuia zetu kuna wenzetu walio na kiburi, majivuno na mioyo migumu. Bila woga tuwaambie na kuwaonya ili hasira ya Mungu isije ikawaangukia. Tuwahimize wasali wamwamini Mungu na wasimsahau muumba wao. Bila woga tuwatete wanyonge hasa Watoto wanaonyanyaswa na kuteseka bila hatia.

Kuhusu kibanda cha Yesu, Sisi tusikijenge bali tufungue mioyo yetu ili aweze kufanya makao yake ndani yetu tuishi naye siku zote, wakati wote na mahali popote. Katika dominika hii ya kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo tunahimizwa kumsikiliza yeye aliye mwana mpendwa wa Mungu Baba. Neno kugeuka maana yake kuwa na hali nyingine. Kiroho kugeuka ni kutoka katika hali mbaya ya dhambi, kufanya toba ya kweli, ni kuanza maisha ya utakatifu, kuacha kabisa matendo maovu na sio kwenda likizo ya dhambi, sio kuahirisha kutenda dhambi ni kubali kabisa mwenendo, kuwa mtu mpya, kuanza maisha mapya ya kumsikiliza mwana wa Mungu na kuishi kadiri ya amri za Mungu.

Dominika hii kila mmoja wetu katika hali yake ajiulize amebadilika katika lipi? Kama wewe ni mvivu mseng’enyaji, mkaidi, mtukutu, domokaya, mpiga majungu, mwongo, mwizi, mlafi, mchoyo, mgomvi, tapeli, mchafu, mlevi, umeacha nini na umegeuka katika lipi tangu kwaresma ianze kama bado tukio la Kristo kugeuka sura lituimarishe tufanye juhudi za makusudi kabisa kumgeukia Mungu kwa kuacha na kupigana kabisa dhidi ya madhaifu yetu. Katika kujaribiwa kwa taabu na mateso mbalimbali, tusitafute ufumbuzi wa shida zetu katika dhambi. Bali tuungane na Yesu, tuendelee kumpenda na kutafuta ufumbuzi kwa namna ilio adili.

Iwapo taabu zetu zimezidi kuwa kubwa, kwa sala zetu tutolee mateso yetu kwa Yesu. Na hii itakuwa nafasi ya heri kwetu, kwani tutakuwa tumeshiriki mateso ya Yesu mwenyewe. Tutakuwa tumevumilia mabaya kwa ajili ya Injili na kwa ajili ya imani yetu. Na katika kufanya hayo, nasi tutajaliwa kuona ule mng’aro wa utukufu wa Mungu. Tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus.

Kwaresima J2
14 March 2019, 15:06