Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Kwaresima: Toba na wongofu wa ndani ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Kipindi cha Kwaresima: Toba na wongofu wa ndani ili kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani!  (Vatican Media)

Tafakari Neno la Mungu: Jumapili IV Kwaresima: Huruma ya Mungu

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alisikika akisema, Kanisa linaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka! Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani ili kutembea katika haki na utakatifu wa maisha!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika dominika ya nne ya kipindi cha kwaresma mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa dominika hii ni kufanya maamuzi ya kuacha dhambi na kusema: Nitaondoka, nitakwenda kwa baba na kumwambia nimekosa ili nipate kufurahi tena. Katika wimbo wa mwanzo nabii Isaya (66: 10-11) anatualika tufurahi akisema, Furahi, Jerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake. Maneno haya yanaipa dominika hii jina la “Letare” yaani Dominika ya furaha. Tunaalikwa kufurahi kwa sababu Pasaka i karibu. Liturujuia ya dominika hii inaruhusu altare kupambwa kwa maua, rangi ya mavazi ya Misa kuwa ya pinki badala ya zambarau pia ala za muziki zinaruhusiwa kupigwa.

Katika Dominika hii huadhimishwa takaso la pili la wakatukumeni watakaobatizwa siku ya Pasaka. Katika somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua, Mungu anawaondolea waisraeli aibu ya kuwa watumwa Misri, nao wakafanya sherehe wakala sikukuu ya Pasaka wakikumbuka makuu aliyowatendea Mungu wakaanza maisha mapya katika nchi ya Kanaani. Wakauonja wema wa Bwana kama mzaburi anavyotuambia katika wimbo wa katikati Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema ni mwaliko wa furaha. Katika somo la pili Mtume Paulo anawaeleza Wakorinto kuwa dhambi iliwatenganisha na Mungu lakini Mungu mwenyewe akiwa ndani ya Kristo aliupatanisha ulimwengu na nafsi yake ili asiwahesabie makosa yao.

Upatanisho huo unaendelezwa na wajumbe waliotumwa na Kristo nasi tunapaswa kufanya jitihadi za kujipatanisha na Mungu kwa njia Kristo yeye asiyejua dhambi lakini Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. Ni upendeleo wa hali ya juu sana tunaopewa na Mungu hivyo hatuna budi kuupokea kwa moyo wa shukrani na furaha. Maneno ya Paulo kuwa Kristo ambaye hakujua dhambi lakini Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye, Yesu mwenyewe katika injili anayaweka wazi katika simulizi la baba mwenye huruma kwa mwanae mpotevu, simulizi alilowapa mafarisayo na waandishi walipomnung¢unikia, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao kwa kuwa watoza ushuru na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia Yesu ili wamsikilize wapate faraja na neno la furaha kutoka kwake.

Simulizi hili linatuonyesha wazi huruma ya Mungu ilivyo kubwa kiasi kwamba tunapofanya toba ya kweli moyoni Mungu anatupokea mara moja, anatukumbatia, anatubusu sana, anatuvika mavazi mapya, anatufanyia sherehe kubwa, tunakuwa huru na kupewa hadhi ya kushiriki karamu ya Kristo, Ekaristi Takatifu ambayo ni kiini cha maisha yetu ya kikristo, nasi tunajaa furaha kubwa ndani mwetu, furaha isikifani na kuanza maisha mapya. Hii ndiyo furaha anayokuwa nayo mtu akifanya toba ya kweli na kuungama vyema dhambi zake, akizitaja waziwazi kwa ujasiri bila kuzimumunya wala kuficha chochote. Ni furaha ya ajabu isiyoelezeka, furaha inayotuondolea mawazo ya kukata tamaa na inayotupa matumaini na nguvu ya kusonga mbele katika maisha yetu. Sakramenti hii ya ya kitubio inatuondolea aibu ya dhambi na kutuweka huru tukiwa wenye furaha. 

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Waisraeli walipekwa utumwani Misri kwa sababu ya dhambi na mwana mpotevu alipelekwa kwenye banda la nguruwe kwa sababu ya dhambi baada ya kula mali ya baba yake na makahaba. Nasi pia inawezekana dhambi imetupeleka utumwani au kwenye banda la nguruwe. Tunapaswa kutafakari na kuzingatia mioyoni mwetu kujiulize “Misri yangu ni wapi?” na “banda langu la nguruwe ni lipi?” Je, ni kitu gani kimenipeleka huko? Je, ni ukahaba, uasherati, nyumba ndogo, ulevi, utoaji mimba, madawa ya kuzuia mimba, uchawi na ushirikina, uzembe, ubinafsi, masengàenyo, umbea, uongo, ulafi, kiburi, marafiki wabaya, madawa ya kulevya, wizi, ujambazi, rushwa, ukaidi, kiburi, kutokufunga, kutokusali, kutokuwasaidia wahitaji au ni nini?

Ni wakati wa kutafakari na kuzingatia moyoni na kamua leo na kusema “inatosha, ninaondoka na kuachana na umisri au ubanda wa nguruwe. Usiogope rudi kwa Baba ukaungame na kumwambia nimekosa nihurumie. Mama Kanisa anatufundisha kuwa dhambi inaondolewa kwa njia ya sakaramenti ya ungamo la Dhambi, Sakramenti ya toba, Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya maungamo, Sakramenti ya msamaha, Sakramenti ya Upatanisho. Kuungama ni ile hali ya mdhambi aliyetayari kutubu kwa kujishutumu mwenyewe kutokana na dhambi alizozitenda mbele ya mhudumu halali wa kanisa ili kujipatanisha na Mungu. Mungu tuliyemkosea ndiye anayeanzisha upatanisho nasi. Anafanya hili kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana Yesu Kristo. Mwaliko tunaoupewa leo wa kufurahi kwa sababu pasaka i karibu, unatudai tuondoke, tuende kwa Baba, tukaungame, tukamwambie tumekosa.

Hiki ndicho alichokifanya Mwana mpotevu lakini ni baada ya kutafakari na kuzingatia moyoni mwake ndipo akaondoka, akaenda na kumwambia Baba, nimekosa nihurumie, nasi tunapaswa kufanya vivyo hivo. Hivyo kitubio ndio mwanzo wa amani binafsi na ya jumuia. Lakini kuondoka na kwenda si rahisi. Inahitaji ujasiri na neema ya Mungu, kila mmoja katika hali yake anahitaji ujasiri na kusema sasa imetosha, nitaondoka na nitakwenda. Kamwe tusikubali ukubwa wa dhambi utukatishe tamaa ya kupata msamaha, kwani jinsi dhambi ilivyo kubwa ndivyo nguvu ya huruma ya Mungu ilivyo kuu zaidi. Bwana ni mwema na mwenye huruma, hapendi wadhambi wapotee na si mwepesi wa hasira ni mwingi wa huruma Zab. 130.

Tunapaswa kumrudia Mungu kwa kusema kama Mfalme Daudi; "Unihurumie, Ee Mungu, kulingana na pendo lako kuu, kwa wingi wa huruma yako kuu uniondolee dhambi zangu" Zab. 51. Lakini tujue wazi kuna wapo watakaochukiza na maamuzi yetu kama mafarisayo na waandishi walivyomnungàunikia Yesu au kama kaka wa mwana mpotevu, nasi wale tuliozoea kuishi nao Misri na katika banda la nguruwe watachukizwa na pengine watatusema vibaya, tusiogope kwani furaha tutakayoipata ni kubwa na ya maana zaidi kuliko kuendelea kubaki misri na kuishi ndani ya banda la nguruwe, yaani kubaki katika dhambi kwani madhara yake ni mabaya zaidi. Kila dhambi inaadhiri akili, inadhoofisha utashi.

Dhambi inaua dhamiri na kupoteza dira ya mdhambi. Dhambi inampumbaza mtu, inampa mtu mawazo na kumwambia nafasi hii ya dhambi ni ya leo tu usiogope hakuna shida. Kila unapotenda dhambi unapunguza uwezo wa dhamiri kugonga/kuuma/kukusuta. Hisia zinavurugika na hivyo kupoteza mizani ya maadili. Mdhambi anakuwa na chuki kwa Mungu kimoyomoyo pia anapoteza imani ya uwepo wa Mungu. Dhambi inadhuru afya kwani humfanya mtu kuwa na hasira na chuki ndani mwake hivyo yaweza kusababisha vidonda vya tumbo au ugonjwa wa moyo (BP) kwani dhambi iko moyoni ndani kabisa. Magonjwa haya ni matokeo ya hasira, chuki na uchu wa kulipiza kisasi vinavyopambani ndani moyoni. Hata magonjwa ya akili yanachangiwa na dhambi hasa dhambi za mauaji.

Dhambi inaharibu lengo la jumuia/jamii ya wakristo wote katika safari ya kumfikia Mungu (Mt. 5:48) pia inaharibu mwili wa fumbo wa Kristo (1Wakor. 12:26). Dhambi inafanya roho ya mkosaji kukosa amani na zaidi sana Neema ya Utakaso. Mtu akikosa dhamani ya Mungu lengo la maisha yake na dhamani ya maisha yake inapotea na hivyo anaanza kuwayawaya kuhangaika haoni cha maana na hivyo linalobaki kwake ni dhamiri iliyojaa mawazo maovu tu kwani upendo, amani, furaha, msamaha kwake ni mwiko. Kumbe ni vyema sasa tufanye maamzi ya mwana mpotevu, tuamue kujinasua kutoka dhambini. Tuweke nia kali ya kujikosoa kwa unyofu, kutojihusisha na dhambi na kutubu kweli.

Tuseme kwa dhati leo, imetosha, nitaondoka, nitakwenda na kumwambia Baba nimekosa. Leo hii dhambi hii naiacha! Uamuzi wa kwanza ni juu ya tamaa yako na uamuzi wa pili ni kuijongea sakramenti ya kitubio. Kitubio kinatuzoeza kunyenyekea na kujikubali kuwa tu wanyonge mbele ya Mungu na kinatustahilisha kupokea Ekaristi, chakula cha kiroho kinachoimarisha imani na fadhila nyingine. Tuepukane na Komunyo za mashaka na kufuru kwani huko ni kuila hukumu yetu wenyewe. Tunapaswa kujibidisha siku zote na kusogelea mara nyingi Sakramenti hii na kutofanya hivyo ni kukaribisha maanguko. Kuungama mara nyingi kunatupa fadhila ya unyenyekevu - kujijua na kujikubali kuwa tu dhaifu 1Yn. 1:8-9.

Tusikate tamaa tunapoungama mara nyingi. Njia ya Msalaba ni ndefu na yenye maanguko mengi: Kila dhambi ni mpya tuanze upya kwa kuungama dhambi zetu tukisema kwa ujasiri bila kuogopa "Mimi ni mwenye dhambi" - Lk. 5:8. "Ole wangu kwa sababu, mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami nakaa kati ya watu wenye midomo michafu" Isa. 6:5 kama Mtume Petro ondoka kwangu ee Bwana kwa kuwa mimi ni mdhambi naye Yesu anamwambia, "Usiogope tokea sasa utakuwa unavua watu" (Lk. 5:10). Tumwombe Mungu atujalie neema tuguswe na huruma yake. Tuchukie dhambi na kuamua leo kuwa ‘nitaondoka na kurudi kwa Baba. Yeye ni mwenye huruma atatupokea na kutuandalia karamu ya Pasaka. Tumsifu Yesu Kristo.

Kwaresima J4

 

27 March 2019, 12:27