Tafuta

Vatican News
Nguzo msingi za Kipindi cha Kwaresima: Fumbo la Msalaba; Kufunga, Neno la Mungu; Sala na Matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji! Nguzo msingi za Kipindi cha Kwaresima: Fumbo la Msalaba; Kufunga, Neno la Mungu; Sala na Matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji!  (ANSA)

Nguzo msingi za Kipindi cha Kwaresima na ukuu wake katika maisha!

Mama Kanisa kila mwaka anawajalia watoto wake kipindi cha siku arobaini za toba na wongofu wa ndani; kipindi cha kusali ili kujenga uhusiano wa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu; kipindi cha kufunga na kujinyima kama sehemu ya ushuhuda wa Injili ya huruma na upendo. Hii ni nafasi pia ya kutafakari ukuu wa Fumbo la Msalaba katika maisha na utume wa Kanisa! Unyenyekevu!

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. - Roma.

Siku hizi watu wengi wanapenda sana kwenda Gym na kufanya mazoezi magumu ya viungo. Neno gym linatokana na kigiriki gymnasion lenye maana ya pahala pa wazi palipotengwa rasmi kufanyia mazoezi ya riadha kwa muda maalumu. Kufanya mazoezi gym kuna faida kwa afya ya mwili na akili pia. Kumbe kanisa limetenga wakati rasmi wa kufanya gym ya kimwili, kiakili na kiroho. Gym  yetu rasmi imetengwa kufanywa kwa siku arobaini mfululizo. Aidha lengo kuu la mazoezi hayo ni kujiandaa kuadhimisha mafumbo makuu ya Pasaka. Mazoezi hayo yamejikita kwenye mfungo, sala na kutenda mema. Ukiyaangalia juu juu mazoezi hayo utashtuka na kuyaona kuwa ni mateso na msalaba mzito. Kumbe ukiingia gym na kuyafanya utagundua  jinsi yalivyojaa utamu wa kiroho, kiakili na kimwili. Kabla ya kuuona uhondo uliojificha katika mazoezi hayo, tuangalie kwanza utamu uliojificha katika mateso yaani msalaba.

UTAKATIFU NA UKUU WA FUMBO LA MSALABA:

Kwa kawaida busu linapigwa kwa mtu umpendaye sana au kwa vitu vya pekee.  Busu ni alama ya upendo mkubwa kwa kitu kilicho kizuri, chema au kilichokupatia ushindi na mafanikio katika maisha. Kwa vyovyote mtu au kitu kinachokuokoa huna budi kukisujudu na kukibusu. Mathalani wachezaji wanabusu mpira, au kikombe cha ushindi wa michezo. Wakati mwingine mchezaji akifunga goli la ushindi, wanatimu wenzake wanamrukia kwa furaha na kumpongeza kwani amewapatia ushindi. Katika ibada ya Ijumaa kuu Wakristu tunabusu na kuabudu Msalaba. Kulikoni?

Ndugu zangu, mateso ya msalaba siyo mchezo. Kwanza kabisa tukitafakari ukatili ulio katika Msalaba huwezi kuwa na hamu ya kuthubutu kusema eti katika msalaba kuna tija au kitu fulani chanya. Hata siku ya Ijumaa kuu tunapoubusu Msalaba tunatikisa vichwa, na kumwonea Yesu huruma. Tunajihisi vibaya kwani ndiyo tuliomsaliti kwa dhambi zetu na kumsababishia kusulubiwa Msalabani. Kifo cha msalaba ni moja ya mateso ya aibu sana yenye karaha na fedheha hapa duniani.

Mkosaji aliyeadhibiwa kufa msalabani hakuteseka tu kimya kimya, bali aligalagala na kujitikisa msalabani kwa maumivu makali yasiyoelezeka. Yalikuwa mateso ya kinyama na ya dharau kubwa kwa utu wa binadamu. Kwa kweli wale waliogundua aina hii ya adhabu walikuwa na unyama wa hali juu sana. Enzi hizo mateso ya msalaba yalifanywa kwa watumwa, kwa wahaini na maaduni wakubwa tu. Kwa maana hiyo wakristu wa zamani waliogopa sana kumwonesha Yesu akiwa katika msalaba. Aidha ilieleweka kwamba msalaba wa Yesu haukuwa tu kitu kibaya na cha kudhalilisha, bali pia ni ishara wazi ya kukataliwa na ya kushindwa kwake. Kwa hiyo kuna uzuri gani katika msalaba hadi ustahili kupigwa busu? Katika hali kama hii tunaweza bado kuzungumza juu ya utamu wa msalaba?Aidha kuna cha mno gani hadi tuuzungumzie Msalaba?

Ndugu zangu katika Msalaba kuna utamu na uzuri unaostahili kupewa muwaa ya nguvu!  Uzuri na utamu huo umelala katika kipengele cha kuokoa na cha kuletesha ushindi. Yesu ametukomboa kwa kuteseka na kufa msalabani. Fumbo kuu la mateso ya msalaba limelala hapo panapoonekana kwa Wagiriki kuwa ni upumbavu na kwa Wayahudi ni kikwazo, yaani palipo ubaya na ukatili hapo ndipo palipojikita fumbo linaloitwa: “Kosa lenye heri-Felix culpa”. Jambo hilo linawezekana tu kwa sababu katika Yesu msulibiwa, tunatafakari suala la uhakika mtupu kwamba Mungu anatupenda bila mipaka wala masharti. Tunao uhakika kwamba makosa yetu yote yamesamehewa kwa njia ya damu azizi ya Yesu. Tunao uhakika kwamba Yesu yuko nasi anatuonea huruma katika majaribu tunayokumbana nayo katika maisha. Tunatambua kuwa hata sisi ni shujaa na tunaoweza kutesekea kwa ajili yake. Aidha tunaweza kumwomba Mungu msamaha na kuwa na uhakika wa kuupata!.

Ukimwangalia Yesu Msalabani, ukiangalia nyundo na misumari zilizompigilia na taji la miiba kichwani, unakuwa na uhakika wote kwamba Mungu ametupenda kweli. Maana kama alimwacha hata Mtoto wake apigike kiasi hicho ili kutukingia sisi kifua, kwa vyovyote Mungu huyo hataweza kamwe kututupa tukikosea. Ama kweli  Mungu ameweka neema ya utakatifu mioyoni mwetu. Kwa hiyo Msalaba si tu nguvu yetu, bali pia ni ung’arao wa utukufu. Ndiyo maana katika Ibada ya Ijumaa kuu: “Tunauabudu Msalaba.”

Katika Jimbo kuu la Songea nchini Tanzania, kuna kanisa moja la parokia liitwalo “Msalaba Mkuu.” Kanisa hilo limewekwa chini ya ulinzi wa Msalaba wa Yesu. Ndani ya Kanisa hilo kumesimikwa Msalaba mrefu pembeni mwa altare. Katika msalaba huo kumetundikwa silaha na pembejeo zote zilizotumika kumsulubu Yesu. Kwa dhati yake vitu hivyo vilistahili kuitwa haramu, viuaji, vikatili na vitesaji. Lakini kumbe, vinaitwa vitakatifu. Tukianzia na Msalaba wenyewe ni Mtakatifu, Misumari mitakatifu, Nyundo takatifu, Taji takatifu, Mkuki mtakatifu, Kamba takatifu, Mijeledi mitakatifu, Mkoba wa pesa Mtakatifu  nk.

Kwa hiyo tuupende Msalaba Mtakatifu, tusiuonee aibu na tujipige ishara ya Msalaba kila tunapoanza kusali, aidha tupende kusali mbele ya Msalaba. Tuibusu miguu ya Yesu, tuubusu uso wa msulibiwa. Kwa njia hiyo tutaangazika na kufarijiwa na fumbo la majeraha yake. Tutasoma kutoka kwenye Msalaba wake ubaya wa ukatili, na mng’aro wa upendo wa Mungu na wa utukufu wa mfufuka. Hayo yote yatakuwa ishara kwetu inayotuonesha kuwa hata misalaba yetu ya maisha inayotuumiza na kutukatisha tamaa inashiriki fumbo la ukombozi linalookoa ulimwengu. Tuutaje “Msalaba” siyo ya kumaanisha matatizo ya maisha, bali ni kwa sababu: Mungu alitupenda sana kiasi cha kutupatia Mwanae. Yesu anatupenda na amekufa Msalabani ili kutusamehe na kutufufua. Hii ndiyo picha na fikra unayotakiwa kuwa nayo unaposikia msalaba.

Pili: Ninaiangaliaje (ninaiona onaje) Misalaba ya ulimwengu huu? Yaani, tunapowaangalia maskini na fukara, wagonjwa na walioachwa, wakoma wa mwili na wa kiroho, wakimbizi na wasio na makao, waliokata tamaa, wafungwa. Je, ninaiona misalaba yao kama karaha, maudhi, kichefuchefu na kuiona kwa dharau na chuki au kwa upendo na ninataka kuwaauni na kushiriki mateso yao. Utamu wa Msalaba, umelala katika kutambua kuwa hiyo ni njia ya ukombozi kwa wote. Wakati wa Kwaresima ni vyema kuangalia kwa dhati karaha iliyoko katika msalaba. Mara nyingi tumezoea kuiona misalaba yetu juu juu tu. Tunabaki kujifikiria na kujionea huruma sisi wenyewe tu basi. Hapo unajisikia kusulibiwa na ni adhabu na mateso ya aibu umwonapo msulibiwa pale msalabani, siyo tu anateseka vibaya, bali anagalagala na kujinyonganyonga kwa maumivu makali.

Ni mateso yanayokuacha mdomo wazi kwa mshangao. Kumbe katika Msalaba huo unaotisha na ulio wa kipagani na wa upumbavu na upuuzi ndipo palipojaa utamu wa  Fumbo takatifu: Ukuu na unyenyekevu wa Mungu! Fumbo la Msalaba linaonekana katika Sikukuu ya kung’ara sura Yesu, unamwona Musa na Eliya wanaongea juu ya kuondoka kwa Yesu. Kuondoka maana yake ni kwenda kuteswa na kufa. Yesu atahitimisha safari yake ya hapa duniani huko Yerusalemu atakakokufa Msalabani. Kwa hiyo kung’ara ni utangulizi wa ufufuko (mng’aro mkuu) unaoanza kwa mateso na kifo chake msalabani. Kwa hiyo utukufu wa Yesu hautenganishwi na Msalaba wake.

Mtumishi wa Mungu Bernadeta Mbawala akiwa hoi anagalagala kwa maumivu makali kitandani alisema: “Mang’amuzi yangu ya kwanza kabisa ya nguvu ya kimungu yanatoka katika Msalaba wa Kristo.” Mtakatifu Paulo mtume anasema: “Neno la Msalaba kwa wanaokombolewa nalo ni nguvu ya Mungu”. Kadhalika alisema: “Sijivunii kitu kingine isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu”. Kwa hiyo tunaweza kuzungumza juu ya “nguvu ya Msalaba; utukufu wa Msalaba; faida ya Msalaba na utamu wa Msalaba” kwa sababu katika Yesu msulibiwa tunao uhakika kwako: Mosi, Mungu anatupenda bila masharti wala mipaka. Pili, makosa na madhambi yetu yote yanasamehewa. Tatu, Yesu yuko karibu nasi anatuonea huruma na kutufariji katika majaribu yetu yote ya maisha na tunapata nguvu ya kuteseka kwa ajili yake.

Kwa hiyo Msalaba ni kitu kitukufu, kinachong’ara na kinachotuweka sawa katika maisha yetu. Kwa hiyo, tuubusu msalaba, tuibusu misumari iliyompigilia Msalabani, tulibusu taji la miba, tuibusu nyundo, tuibusu mikono, miguu, ubavu na uso wa Yesu msulibiwa. Kwa kufanya hivyo tutaangazwa na kutulizwa kwa fumbo la majeraha yake. Aidha tutasoma kutoka ubaya na ukatili wa msalabani kuwa ndiyo mng’aro wa upendo wa Mungu na wa utukufu wa Mfufuka. Hayo yote yatakuwa kama matokeo ambayo hata mateso ya misalaba yetu midogo kwa mikubwa inayotukatisha tamaa, tutaweza kuichukulia kuwa kama namna yetu ya kushiriki fumbo la ukombozi wa ulimwengu. Ama kweli tunajivunia msalaba mtamu. “Fahari yetu ni Msalaba”.

UMUHIMU WA KUFUNGA NA KUJINYIMA: KUDHIBITI VILEMA

Aina hii ya gym ya kiroho ni ngumu sana. Ukiwaona wanaofanya mfungo wa kidini unakosa hamu ya kufunga. Maana utamwona mtu amesinyaa na kukosa raha kabisa. Mwingine anashinda anatema-tema mate ovyo akichelea kufungua mfungo. Wengine wanawavaa wanaokula chakula mbele yao. Hapo mfungo unageuka kuwa mateso. Ama kweli mfungo hauna utamu wowote ndani yake. Aidha, tunapata kigagasi fulani kinapokaribia kipindi cha Kwaresima. Basi tujiulize kama zoezi hili la mfungo bado hai au ni zoezi hewa lililopitwa na wakati. Aidha, tujiulize kama kuna utamu wowote ule katika zoezi hili. Kuhusu mfungo wa Kwaresima Mtakatifu Ambrosi anasema: “Inatujia sikukuu na ambayo tayari imeshakaribia (Kwaresima)… Ushindi wetu ni Msalaba wa Kristo, na Fahari yetu ni Pasaka ya Bwana Yesu. Awali ya yote Kristu alipigania kupata ushindi, lakini siyo kwa ajili yake, bali kwa ajili ya kutufundisha jinsi ya kupigana. Hata Yesu mwenyewe alifunga. Akaweka kipao mbele mfungo ili kuvivunja vifungo vya mshawishi shetani. Kwa hiyo mapambano yetu ni kufunga.”

Ili kuupatia umaana zaidi uasheta wa kikristo Mtakatifu Ambrosi alisema: “Mfungo una nguvu ya ajabu kwa sababu hata Yesu mwenyewe alifunga. Aidha mfungo ni mzuri kwa sababu humwinua binadamu na kumpeleka hadi juu mbinguni. Mfungo ni zoezi mwafaka la kukarabati roho na mwili. Aidha mfungo ni chakula cha kiroho, ni maisha ya kimalaika, ni kifo cha dhambi, mwisho wa uhalifu, ni njia ya ukombozi, ni  chanzo cha neema na msingi wa usafi wa moyo.” Kwa hiyo yatubidi tutambue kuwa mfungo  ni nidhamu inayotakiwa kufuatwa na watu wote kwa manufaa ya jamii. Yaani kufunga kwa ajili ya wenye njaa, fukara. Kadhalika kufunga kwa ajili ya ulimwengu uliojaa matatizo na kukitiri maovu ya kila aina. Kwa hiyo, faida kuu ya mfungo kijamii unayo maana sana tena inayolenga hadhi ya binadamu.  Lakini kwetu sisi wakristo, yatubidi tupate maana ya mfungo inayotufaa zaidi. Maana ya kiasheta ya kutubu na majuto kwa ajili ya utakatifu na kwa maisha ya kiroho.

Katika mfungo wa kawaida wa kimwili kuna vipengele vingi vinavyoonekana kirahisi katika maisha yetu ya kila siku. Kwa mfano, kufunga chakula au kufunga kuongea. Unaweza ukafunga kula aina fulani ya chakula, au ukapunguza kula chakula unachokipenda sana. Kwa mfano kama unayo mazoea ya kunywa pombe au unavuta sana tumbako, nk. Mafaa yake kiroho, kama ukifunga hutaumia, hasa ukikumbuka kuwa unafuata nyayo za Yesu anayesafiri kuelekea Kalvarini (Msalabani) na kwenye Pasaka.

Halafu kipengele muhimu kwa afya ya kiroho ni kufunga macho na maruyaruya kichwani. Huu ni mfungo nyeti kwani unapiga vita homa iliyojikita sana katika jamii. Homa kubwa ya sasa katika jamii ni ya kutegemea mno vyombo vya mawasiliano. Ikiwa ni pamoja na matumizi tegemezi ya simu za mkononi, intenet, ipad, computer, luninga au televisheni nk. Huu ni ugonjwa wenye mvuto mkali sana na wenye kuacha maruyaruya kichwani yanayokukosesha. Mapato yake hata unakosa utulivu wa roho na wa mwili. Tukifanikiwa kufunga na kukiepa kishawishi hiki tutaona mapato yake katika maisha yetu, katika familia na jumuiya zetu, hata katika sala zetu. Yaani tutaona mabadiliko mazuri katika akili zetu na mwili wetu unavyofanya kazi kiutu.

Aidha utaufaidi zaidi mfungo ikiwa mwenyewe utajiongeza kidogo kwa kutenga muda wako binafsi wa upweke kwa kusali na kuyatafakari maisha yako. Kwa kufanya hivyo, utagundua polepole jinsi ya kujenga nidhamu ya kiroho ambayo ni fursa mwafaka kwa maisha ya kiroho.  Lengo kuu la sisi sote pamoja na kanisa zima ni kusafiri na Yesu hadi Pasaka. Kwa hiyo gym hii italeta maana kubwa zaidi kiroho hasa katika matendo yetu ya upendo. Aidga mazoezi hayo yatakuwa na tija na yatatusaidia kuruka vihunzi vinavyokinaisha, na kutuchosha, kwa sababu tutaibua nidhamu ya ndani iliyoundwa kwa juhudi na ustahimilifu. Mama Maria atusaidie kulifanya zoezi hili kwa siku 40. “Maisha safari tuende hodari, yapita taabu, yadumu thawabu.”

UMUHIMU WA NENO LA MUNGU KAMA DIRA YA MISHA YA KIROHO

Wakati wa Misa Takatifu, Padre au Shemasi anabusu ukurasa wa Injili aliousoma. Biblia ni Maandishi ya kale, ya wakati ulio mbali sana na uhalisia wa maisha ya ulimwenguni wa sasa. Sana sana Biblia ni maandishi yaliyosheheni ujumbe na alama za utamaduni wa kigeni. Hivi Biblia ni maandishi magumu kwetu kuyaelewa. Kwa hiyo kuna utamu gani katika Biblia hadi kuibusu? Kwa hiyo hatuna budi tujipange sawasawa tunapotaka kuzungumzia juu ya utamu wa Biblia. Aidha yabidi kujiuliza kama Biblia ina maneno matamu yanayovutia; aidha ni utamu aina gani tunaoweza kuuonja?

Kusoma Neno la Mungu wakati huu ni gym au mazoezi yenye makuzi ya kiakili na kiroho. Utamu wa kuisoma Biblia inaonja zaidi akili na roho. Kwanza kabisa hasa kutokana na uandishi wake mahili wa kiufundi na kiufasihi mkubwa. Uandishi wa Biblia ni kielelezo kikuu cha lugha iliyo wazi, lugha yenye ushawishi wa kubadili au hata kugeuza kabisa tabia ya msomaji. Yaani, Biblia ni kitabu chenye nguvu na mvuto wa kumfanya mtu ageuze mwenendo wake wa maisha. Kwa hiyo tunaweza kusema kwamba katika kila sura ya Maandiko Matakatifu, kunaakisi nguvu na uzuri wa kimungu. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alisema: “Kila ninaposoma kitabu au maandishi yoyote yale hata yale, ninajisikia kuchoka sana. Ninapoona hali hiyo ninaacha kusoma kitabu hicho maana naona kinajaza kichwa na kufukarisha moyo wangu. Badala yake nachukua Biblia na kuanza kusoma Neno Takatifu la Mungu. Hapo sasa mara moja ninaona kila kitu kinang’ara. Ninaligundua Neno hilo linalouamsha na kuupanua moyo wangu”.

Ili kupata zaidi utamu uliosheheni katika Biblia, yatubidi kila tunaposoma tujiulize: “Fasuli hii inasema nini?” Mara nyingi hatujiulizi swali hili kwa sababu pengine fasuli hii tulishaisikia hivi tunafikiri tunaifahamu tayari. Kumbe utakaporudia kuisoma tena kwa uangalifu unagundua utamu uliomo. Inabidi kujiuliza tena: “Aya hii inaniambia nini mimi?” Wakati mwingine utagundua kwamba aya hiyo inakulenga moja kwa moja. Yaani, inazungumza juu ya kile unachokihitaji na inakupa suluhisho la vurugu na giza linalofunika moyo na akili yako. Yawezekana pia kwamba kipengele hicho kinasuta mwenendo wako wa maisha, au kinakutuliza, au kinakupa msamaha na amani nk. Hapo unagundua kuwa Biblia ni mvuvio wa Roho mtakatifu unaomwangaza na kumwongoza kila mmoja wetu ndani mwake.

Tusisahau pia kujiuliza ni sehemu au ukurasa upi wa Injili unaonipendeza zaidi, au ni sehemu ipi inanifaa mimi. Kwa kufanya hivyo tutaona kwamba inawezekana kupita kutoka kurasa zile unazoziona ngumu na hadi zile rahisi, kwa kuzilinganisha. Ama kweli Neno la Mungu ni tamu. Hii ndiyo pamba ya kufaa njiani katika msafara wetu wa siku hizi arobaini za gym yetu ya kiroho.

UTAMU WA SALA KATIKA MAISHA NA UTUME WA MWAMINI

Tumeutafakari utamu wa Msalaba, wa Mfungo na wa Biblia. Sasa tuuone utamu uliolala kwenye sala. Aidha sala nayo ni gym yenye mazoezi ya kimwili na kiroho, kwa vile katika kusali unatumia akili, mtima na midomo na miguu kwa kusimama, kuketi au kupiga magoti.  Kwa kweli kusali hakunogi yaani ni kitu kikavu kama vile kutembea jangwani. Mapato yake unasikia wengine wanalalamika na kusema kwamba sala inachosha, hasa zala zile zinazojirudiarudia kama ilivyo sala ya rosaziri, litania au njia ya msalaba nk. Wangine wanasema, kwamba katika kusali inatakiwa kutumia nguvu, yadai uvumilivu na kung’ang’ana kusali. Wengine wanasema: “Sala inakatisha tamaa, ninasali lakini hakuna kinachobadilika, kwa hiyo ni afadhali kuacha tu kusali kwenyewe.”  Kwa hiyo tunaweza kujihoji endapo katika sala kuna utamu wowote? Aidha mimi ninafaidika kitu chochote kile katika kusali?

Katika tafakari yetu tutajikita katika vipengele vifuatavyo: Mosi, tutajihoji: “Kama kweli sala ni tamu? Pili, kwa nini sala ni tamu? Tatu, “Tunawezaje kuonja utamu wa sala?” Ili kukupatia hamasa ya utamu ulioko katika sala ninakualika kukifuatilia kwanza kile kituko cha kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristu: “Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo akapanda mlimani kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta” (Lk 9:28b-29). Aya hizi zinabaini waziwazi kuwa wakati Yesu alipokuwa anasali alibadilika sura yake na mavazi yake yakawa meupe, Pe! Yaani Yesu alikuwa mzuri, anang’ara sura na kumeremeta wakati anasali. Kumbe sala inapendezesha, inang’arisha na kukufanya umeremete. Hapa unaona mahusiano haya ya sala na kung’ara ni vipengele viwili tunavyoweza kuvitafakari kwa kina.

 Mt. Theresia wa Avila, Mwalimu wa Kanisa ameandika vuzuri kuhusu utamu na uzuri wa sala. Anasema kwamba sala ni kitendo cha urafiki, ni kitendo cha upendo. Kigezo kikuu cha utamu wa sala ni kwamba sala inatubadilisha. Ukweli huu tumeuona tayari katika aya ya kung’ara sura Bwana Yesu. Yesu aling’ara sura wakati anasali. Uzuri na utamu mwingine wa sala unaweza kukielezea kuwa ni tendo lililo bora kwa mtu aliye na imani, yaani kwa mtu anayejitoa kwa Neno la Mungu. Aidha, kila neno au kila sala tunayoitamka kutoka moyoni hata kama kwa namna ya kutawanyika mawazo inajenga daraja kati ya dunia na mbingu, kati ya usasa na umilele. Kwa hiyo sala ni nzuri kwa sababu, inajenga daraja. Kila unaposali unaweza kudhani unazunguza na ukuta usio na masikio. La sivyo, kwa sababu sala inaenda kwenye umilele, kwenye uhalisia unaodumu. Yaani maneno ya sala yanadumu milele. Hii ndiyo hatima ya maneno tunayoweza kuiona kwenye sala peke yake. Kwa hiyo sala si kitu haba.  Kinyume chake maneno mengi tunayobwabwata mitaani yanapita na kuishia humohumo vijiweni.

Kwa hiyo, kama sala ni kitu kizuri, tunaweza kufaidi utamu wake, yaani tunaweza kuona uzuri wake wakati nyeti hasa ule wa kukata tamaa. Mtakatifu Teresa wa mtoto Yesu ndiye mwalimu mzuri wa sala na aliyeonja utamu uliolala katika sala, alisema: “Kama mnafurahi mnaweza kumtafakuri mfufuka, mumwonapo anapotoka kaburini, hapo furaha yenu itaongezeka. We kunoga! Ni maajabu! Ni ukuu! Aidha kama mnadhulumiwa, mmebanwa na matatizo, hapo mnaweza kumtafakari Yesu akiwa kwenye bustani ya mizeituni kule Gestemani”.

Unaweza kuendelea kufanya gym hii ya sala peke yako, kwa kutafakari maswali yafuatayo: Je, kwangu mimi sala ni kitu rahisi au kigumu? Ingefaa kushirikishana mang’amuzi juu ya urahisi na ugumu huo wa sala. Je, ni kitu gani kinachonisaidia mimi kusali kirahisi? Je, kuna watu fulani au kitu fulani kilichonisaidia na kinachoweza kuwasaidia pia wengine? Je, kuna ulinganifu gani katika sala ya liturjia na sala ya binafsi? Kipengele hiki kinahusu aina yoyote ile ya sala, hasahasa sala ya Ekaristi ambayo ni Misa iliyo sala rasmi ya Kanisa.

Paulo anawaandikia Wakristo wake wa Watesalonike kwamba “Furahini daima, na msali daima”. Kitu cha kushangaza katika barua hii ya kale kupita nyaraka zote za vitabu ya Agano jipya, Paulo anahitimisha kwa kutoa tahadhari kishairi: “Furahini daima” “Salini daima” (I Watessa. 5:16-17). Hapa yaonekana Paulo anataka kusema wazi kwamba, Sala na Furaha zinategemezana. Yaani, ni kama vile anataka kutuambia: “Mnataka kufurahi daima, basi salini daima.” Haya ndiyo mapato mazuri ya sala kwamba inakuzidishia furaha. Vinginevyo, utakuwa mtu wa kununa nuna tu. Kwa hiyo kusali kunakung’arisha na kukujaza furaha. Huu ndiyo utamu wa gym ya kiroho.

14 March 2019, 06:46