Cerca

Vatican News
Mtakatifu Yosefu ni mfano wa baba mnyenyekevu, mpole, mkarimu, mvumilivu na mkimya aliyetambua kutii na kuamini kutunza mchumba wake na Mwana wa Mungu Mtakatifu Yosefu ni mfano wa baba mnyenyekevu, mpole, mkarimu, mvumilivu na mkimya,aliyetambua kutii na kuamini kutunza mchumba wake na Mwana wa Mungu 

Kila tarehe 19 Machi ni Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu mchumba wa Bikira Maria!

Mtakatifu Yosefu alibeba wito wa ubaba, alichukua fumbo kusaidia na kulinda.Lakini ni kwa njia ya ukimya katika kwa kazi yake hadi Mungu alipomwita kwake.Ni moja ya sifa ya tafakari ya baba Mtakatifu Francisko akitazama sura ya Mtakatifu Yosefu.Tunatazama sura hii tunapolekea tarehe 19 Machi ambapo Mama Kanisa anaadhimisha sikukuu yake

Na sr Angela Rwezaula - Vatican

Kila tarehe 19 Machi ya kila mwaka  ni Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu msimamizi na mchumba wa mama Bikira Maria ambapo pia anajulikana kama ni msimamizi wa  wafanyakazi, wa wanauchumi, walioachwa pekee pembezoni, walio karibu ya kufa, mababa na waandamizi wa mambo ya sheria. Kwa hakika ni mzao halisi, ni Mtakatifu Mkuu sana wa Kanisa anayesifiwa na kutolewa ibada, baada ya Bikira Maria Mama Mtakatifu.  Maisha yake yote yalibaki ndani bila kujulikana. Hakuna mwana historia aliweza kuandika kumbukumbu yake, lakini utakatifu wake na ushuhuda wake mzuri sana unapatikaka katika maandiko Matakatifu. Hiyo ni kuonesha kuwa Mungu alikuwa tayari amechagua kuwa mlinzi wa Mwokozi Yesu Kristo na  mlinzi wa mchumba wa Bikira Maria.

Tarehe 19 Machi Mama Katina linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu

Tunapokaribia katika kilele cha Sikukuu ya Mtakatifu Yosefu tarehe 19 Machi ambayo ni sambamba na sikukuu ya baba wote, kwa kawaida katika tamaduni nyingi za kikristo kwa mfano wa  wakristo wa nchi za Ulaya, watoto wa shule nyingi na waalimu wao kwa pamoja uwaandaliwa baba zao zawadi, ikiwa ni ishara ya upendo kwa kukumbuka na kuenzi sura hii ya Mtakatifu Yosefu,kwa maana hiyo  leo hii ndugu msomaji ebu tuitazame sura hii pamoja kwa kina.

Hawali ya yote  tunaweza kusema kuwa Mama Maria alimpata Yosefu kama msindikizaji mwaminifu wa maisha yake ambaye alimfariji na kumlinda. Ni kwa jinsi gani, vijana wengi wa kiume na wanaume wangeweza kuiga zaidi mfano huo? Katika dunia yetu ambamo, wasichana wengi na wanawake, wametelekezwa kufuatia na kupata ujauzito? Ndiyo kuna utofauti wa Bikira Maria na Yosefu, lakini kwa hakika katika upendo mkuu na uaminifu wa Mtakatifu Yosefu unajionesha, yeye aliweza alithubutu kwa imani na kukubali fumbo la ajabu.

Wasi wasi, utii na uaminifu wa Mtakatifu Yosefu

Injili inatuonesha wazi jinsi gani Mtakatifu Yosefu alikuwa amedhamilia kuweka pembeni zawadi kubwa ambayo Roho Mtakatifu alikuwa amemtendea Bikira Maria.  Hiyo ilitokana na kwamba kuwa mtu wa kawaida alipata mashaka makubwa juu ya fumbo la mchumba wake. Na kama nilivyokwisha kusema japokuwa alipata mashaka, lakini hayakumpelekea kuwa na mawazo mabaya, maana aliongozwa na upendo mkuu aliokuwa nao kwa mchuma wake Matakatifu na aliamua amwache kwa ukimya bila kumdhuru, kufuatia na tamaduni za kale ambazo zilikuwa ni ngumu kwa yule ambaye angebainika na ujauzito kabla ya ndoa, sheria ilikuwa ni kupigwa mawe bila huruma. Na wakati anaendelea  kufuata pendekezo lake kwa siri, ndipo  wakati huo Bwana alipendelea kumjia kwa kumtumia Malaika na mtumishi wake mwaminifu wa fumbo kubwa la aliyefanyika mwili. Kwa maana nyingine ni wakati ambao watu walikuwa wanatamani kuona  mwana wa Mungu, naye  akaja kuishi kati ya watu, na Mtakatifu Yosefu na Bikira Maria walikuwa wa kwanza kumwabudu mtoto wa Mungu

Huzuni mwingi kwa tendo la  kuangamiza watoto wa Bethlehemu

Hata hivyo katika historia ya Mtakatifu Yosefu japokuwa ni fupi inaonesha ni huzuni gani uliosikika wakati mfalme wa Yudea anaamuru watoto wote wa Bethlehemu  waliokuwa chini ya umri wa miaka 2 wauwawe bila kubagua, kwa lengo la kutaka muua hata Yesu ambaye alikuwa anasikika masikioni kama mfala wa wayahudi. Mtakatifu Yosefu kwa mara nyingine tena, Malaika alimtokea na kumjulisha hatari hiyo. Kwa utayari kabisa  akamchukua Maria na mtoto wakakimbilia Misri. Baada ya kifo cha Erode, Injili inatuonesha kwa mara nyingine tana  kwamba Mtakatifu Yosefu kwa ndoto tena Malaika alimwambia arudi kwao kutoka Misri  yeye kwa ukarimu na upole alianza safari ya kurudi na familia yake. Lakini kwa kuogopa mfalme mwingine mtoto wa Erode, kwa njia ya ndoto tena aliambiwa hasiwenda huko bali aweze kuishi huko Galilaya. Walikwenda wakaishi katika mji mdogo wa Nazareti mahali ambapo aliwatunza Mtoto Yesu na Maria mchumba wake.

Injili inathibitisha pia Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mwanaseremala

Ndugu msomaji ni vema kabisa kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yosefu mwaminifu wa Mungu.  Tunatambua kuwa Mtakatifu Yosefu katika Injili anaitwa mwanaseremala na ndiyo maana ni msimamizi wa wafanyakazi wote. Hii ni katika Injili isemayo kuwa “watu Wa Nazareti waliposikia Yesu anafundisha katika Sinagogi, walisema; hivi si mwana wa yule seremala?”, Wakiwa na maana ya Mtoto wa Yosefu. Na wakati mwingine walitoa maneno hayo kwa mshangao na hata kwa dharau, “hivi si yule mselamala?”

Hakuna shaka kuwa Mtakatifu Yosefu hakuwa mfanyakazi kweli, mwanaume anayejua kazi na ugumu.Yeye alikuwa ni mseremala, aliyetambua kushika zana zote za kutendea  kazi ya mikono kwa kutumia  chuma na mbao. Aliweza kushika msumeno, misumari na kila aina ya zana ya ufundi seremala kuaznia asubgu hadi jioni , kwa maisha yake yote. Ni mara ngapo tunaona picha ya Mtakatifu Yosefu akiwa meza ya kufanyika kazi na msumeno? Alikuwa ni mwanaume mwenye haki , na alitambua kudfanya kazi  ambayo ni sheria kwa wote. Hakuwa mgumu na wali kulalamikia kazi yake.  Alifanya kazi kwa bidii na kwa utashi kwa ajili ya wema na juhudi zake kwa wale ambao walimkabidhi kazi yao.

Alipenda kazi na kwa unyenyevu kwani kama alikuwa anatoka  katika ukoo wa mfalme Daud angejidai na zaidi kuwa mchumba wa Mama wa Mungu, msimamizi wa Mungu aliyejifanya binadamu. Licha ya hayo tunapatambua kwamba ni kwa unyenyekevu wa kibaba kama zoezi la kazi yake kila siku na ugumu alifanya hivyo. Aliacha kazi yake wakati wa kwenda kusali kama utamaduni na mapenzi ya Mungu  ambayo ilimsaidia katika hija yake ya maisha. Tunaona wazi kwamba Mtakatifu Yosefu hakutaka kamwe kujifurahisha binafsi kwa faida yake na utajiri. Alitambua kuwa mwenye furaha na mtu wa imani kubwa ambayo aliichota kila siku katika shughuli zake na hata katika magumu.

Kwa kutazama Baba Mtakatifu Francisko anavyo mwelezea Mtakatifu Yosefu

Ndugu msomaji tukiendelea kutafakari kuhusu sura hii ya Mtakatifu Yosefu tunapoelekea katika sikukuu yake, ebu tusaidiwe hata  Baba Mtakatifu Francisko, kwa miaka hii ambayo ameweze kumtumia sana, katika mahubiri yake na kutoa mifano  mingi kwa ajili yake akikazia kumwinga kama sura muhimu katika maisha yetu ya kikristo. “Ni zaidi ya miaka 40 ninasali kwa Mtakatifu Yosefu na hajawahi kuniambia hapana. Tunatakiwa kuwa na ujasiri huo. Utume wake unajionseha kwa dhati katika  karama ambayo inajikita kwenye maisha na wazo la huduma kama alivyoishi Mtakatifu Yosefu.Ni kuanzia kuiga mtindo wake wa kijasiri,  unyenyekevu na kufanya kazi kwa juhudi. Yeye aliishi kwa uaminifu na urahisi kuanzia wito wake wa kumlinda Maria na Moto Yesu. Alikuwa karibu sana na mchumba wake katika kipindi cha furaha  hata kile kigumu na kwake yeye aliweza kuwa na msimamo wa ajabu wa familia. Macho yake yalikuwa daima yakimtazama Yesu”.

Hii ni moja ya hotuba aliyotoa Baba Mtakatifu Francisko tarehe 31 Agosti 2018 wakati alipokutana na wajumbe wa Mkutano mkuu wa XVII wa Shirika la Kitawa la Waoblati wa Mtakatifu Yosefu. Akitazama karama yao hasa ya kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu alisema: shughuli yao katika dunia ni ile ya kuwa mashuhuda wa ujumbe wa faraja wa habari njema, yaani wa Mungu ambaye anasaidia wote na zaidi kupendelea walio wadogo na wadhaifu ili kupanda na kukuza Ufalme wake dunia kama ilivyo mbinguni. Umakini wa Kanisa ni kwa vijana, wazee na wale wanyenyekevu ambao wanaweza daima kuwa mihuri ya wito wa Kanisa kwa mfano wa Mtakatifu Yosefu.

Mtakatifu Yosefu anatambua kutembea gizani, kusikiliza sauti ya Mungu na kwenda mbele kwa ukimya

Aidha Baba Mtakatifu francisko wakati wa mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Marta kunako tarehe 18 Desemba 2017 anasimulia juu ya Mtakatifu Yosefu  alivyo mkuu sana, kwamba anatambua namna ya kutambea katika giza, kwa jinsi gani ya kusikiliza sauti ya Mungu, kwa jinsi gani ya kwenda mbele kwa ukimya. Kwa mujibu wa Baba Mtakatifu anaelezea historia ya Mtakatitu Yosefu hasa alipoona ujauzito wa Mama Maria unaanza kukua na kuonekana yaani ishara ya umama. Na kama mtu aliweza kuwa na mashaka, uchungu na mateso yake kutokanana watu wa kijijini kuanza maneno mengi. Ndiyo, anaongeza  Yeye hakuwa na utambuzi nini kimetokea kwa maana ni  mwanadamu, lakini alikuwa anajua kuwa Maria alikuwa ni Mama wa Mungu. Na ndipo aliamua amwache kwa siri bila kumwaibisha hadharani, lakini Bwana anaingilia kati kwa njia ya Malaika kwenye ndoto ambapo aliambiwa kwamba kiumbe kitakachozaliwa ni kwa njia ya Roho Mtakatifu. Na kwa maana hiyo yeye aliamini na kutii.

Mtakatifu Yosefu alikuwa amebeba wito huo wa ubaba alithibitisha Baba Mtakatifu na kuongeza kusema Mtakatifu Yosefu alikuwa anachukua fumbo hili na kusaidia. Lakini ni kwa njia ya  ukimya tu na kwa kazi yake hadi Mungu alipo mwita kwake. Mwanaume huyo kwa hakika alichukua majukumu ya ubaba na fumbo, ambapo wanasema lilikuwa ni kivuli cha Baba. Kivuli cha Mungu Baba. Na kama Yesu binadamu alijifunza neno la kusema Baba, yaani Baba yake aliyekuwa anamjua kama Mungu, alijifunza kutokana na maisha, na ushuhuda wa Mtakatifu Yosefu. Mtu ambaye alikuwa ni msimamizi, mtu aliye mfanya akue, mtu aliyepeleka mbele kila hatua ya ubaba, kila fumbo lakini hakubeba chochote kilicho chake binafsi zaidi ya fumbo hili takatifu.

Mtakatifu Yosefu ni mlinzi wa wadhaifu na wadhambi pia

Kadhalika Mtakatifu Yosefu ni mwota ndoto na mwenye uwezo wa kukubali ahadi ya Mungu na kuipeleka mbele kwa ukimya wa nguvu, anaipeleka mbele ili kile ambacho Mungu anapende kitimilizike. Alithibitisha hayo katika mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican kunako tarehe 20 Machi 2017. Kwa kufafanua juu ya Mtakatifu Yosefu anasema, ni kama mtu ambaye hazungumzi lakini anatii, mtu wa upendo, mtu mwenye uwezo wa kupeleka utume wake  hadi unakuwa  imara na uhakika; mtu anaye hakikisha msimamo wa Ufalme wa Mungu, ubaba wa Mungu, utoto wetu na kama mwana wa Mungu.

Aidha aliongeza kusema,anapendelea kumfikiria Mtakatifu Yosefu kama msimamizi wa wadhaifu, mwenye uwezo wa kuzaliwa kwa mambo mengi mazuri kutokana na udhaifu wetu na dhambi zetu pia! Mtakatifu Yosefu ni mfano na baba anayesali ili Bwana awapatie sisi sote kuwa na uwezo wa kuota ndoto kwa sababu tunapoota ndoto ya mambo makubwa, mambo madogo tunakaribia ile ndoto ya Mungu ya mambo Mungu abayoota juu yetu. Na ili vijana waweze kuwa na uwezo wa kuota, kuthubutu na kuchukua majukumu magumu ambayo wanaona katika ndoto zao. Na ili atujalie hata sisi uaminifu wa ambao kwa ujumla ni kuwa na mtindo wa haki, kwani yeye alikuwa ni mwenye haki, kukua katika kimya na kuwa wenye maneno machache, alikuwa ni mwenye uwezo  wa kulinda udhaifu wetu, hata wa wengine.

Kujifunza kutafuta nafasi kusaidia, kukaa kimya na kuota ndoto

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Marta mjini Vatican tarehe 18 Desemba 2018 anasimulia juu ya Mtakatifu Yosefu kwamba anatafuta nafasi, ili mtoto apate kuzaliwa, anamlea na kumtunza, anamsaidia akue; alimfundisha kusali, namara nyingi katika ukimya. Kamwe hakumliki kama mtoto wake, alimwacha akue katika ukimya. Kuacha ukue katika ukimya ndiyo lingekuwa neno linalofaa katika nyakati zetu, ambazo kwa asili tunapenda kuweka pia kwa kila kitu, hasa katika maisha ya wengine na kuanza domo kaya. Lakini Mtakatifu Yosefu anamwacha mtoto akue, anamlinda, anamsaidia lakini kwa ukimya.

Mtakatifu Yosefu anaota ndoto lakini siyo kichwa cha mwota ndoto hewani. Na ndoto ni sehemu mwafaka ya kutafuta ukweli, kwa sababu katika ndoto hatujilindi dhidi ya ukweli. Na Mungu anazungumza katika ndoto. Kwa bahati mbaya mara nyingi hatutambui kuafsi ndoto hizi anasema, japokuwa mara nyingi Mungu alichagua kuzungumza katika ndoto, na mtakatifu Yosefu hakuwa mwota ndoto tu za kubuni, kwani ndoto za kubuni ni tofauti maana  zipo katika hewa na wala hazina msimamo.

Kwa kuhitimisha na makala hii tukumbuke kuwa ni Papa Pio IX alimtangaza Mtakatifu Yosefu kuwa ni msimamizi wa Kanisa la ulimwengu.  Na kwa maana hiyo tusali pamoja:  

Ee Mt. Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya Mchumba wako Mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu Mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza Mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema sie tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako. Ee Mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu. Ee Baba uliyetupenda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa Mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa, na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida yote; mtunze daima kila mmoja wetu, tufwate mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata mbinguni makao ya raha milele. Amina.

Tuwajibike wakina baba kwa kuiga mfano wa Mtakatifu Yosefu msimamizi wa familia takatifu

Ninawatakakia sikukuu njema ya Mtakatifu Yosefu msimamizi wa familia takatifu ya Nazareti, hasa kwa mababa wote duniani, tuwakumbuke kwa sala, kuwaenzi wote na kuwapongeza. Lakini kwa  wale ambao katika maisha yao au hata sasa katika maisha yao, hawakutenda/ watendi hawawajibiki ipasavyo kwa kuiga  mfano wa Mtakatifu Yosefu,siku hiii iwe  fursa kubwa kwao kujirudi, kutubu, kuwajibika, bado hawajachelewa, kuna fursa kubwa. Na zaidi tukiwa katika kipindi cha Kwaresima ambacho kwa siku ya tarehe 19 Machi, kinatulizwa na sura hii angavu ya unyenyekevu, ya upendo ya upole, wema unyenyekevu, uvumilivu, bidii, utashi, na msimamo thabiti, wanaweza kweli kumrudia Mungu ili kwa mfano wa Mtakatifu Yosefu waweze kuwa mababa hai wa kutekeleza wajibu wao!

MTAKATIFU YOSEFU

 

18 March 2019, 14:45