Cerca

Vatican News
Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa. Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa mwaka 2019 lina jumla ya Parokia 114: Lengo ni huduma ya uinjilishaji! Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa: Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa mwaka 2019 lina jumla ya Parokia 114: Lengo ni huduma ya uinjilishaji!  (ANSA)

Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Parokia sasa ni 114: Huduma zaidi!

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salam, kwa kusoma alama za nyakati na kwa kuangalia mahitaji ya shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho ya watu waami, ameamua kuipandisha hadhi Parokia teule ya Mtakatifu Yuda Thadei, iliyoko Mpiji Magoe, kuwa Parokia kamili na itahudumiwa na Mapadre Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosmini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana kwa mwaka 2018 wamekazia umuhimu wa Kanisa kupyaisha maisha na utume wa Parokia, ili kuleta mvuto na mashiko kwa vijana wa kizazi kipya pamoja na waamini katika ujumla wao, ili hatimaye, kujenga familia ya Mungu inayowajibikiana katika: imani, matumaini na mapendo. Mama Kanisa anasema, adhimisho la  Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa ni kiini cha Parokia. Kimsingi, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa siku ya Bwana yaani Jumapili. Hii ni siku ambayo Jumuiya ya waamini inapata nafasi ya: kusoma, kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu na hatimaye, kutumwa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao, kama kielelezo cha imani tendaji!

Kumbe, Parokia ni mahali pa kujenga na kudumisha ujirani  na kwamba, Parokia ni kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali pa kufundishia watu kweli na tunu za Kiinjili; kuinjilisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili; huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salam, kwa kusoma alama za nyakati na kwa kuangalia mahitaji ya shughuli za kichungaji na maisha ya kiroho ya waamini, ameamua kuipandisha hadhi Parokia teule ya Mtakatifu Yuda Thadei, iliyoko Mpiji Magoe, kuwa Parokia kamili na itahudumiwa na Mapadre Shirika la Mapendo, maarufu kama Warosmini. Mapadre hawa pia wanafanya utume wao Parokiani Msakuzi.

Hadi kufikia, tarehe 19 Machi 2019, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Msimamizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Padre Frank Mtavangu, Katibu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo lina Parokia 114. Kardinali Polycarp Pengo, kwa kusukumwa na mahitaji ya maisha ya kiroho, ameamua kukipandisha hadhi Kigango cha Mtakatifu Salome, kilichoko kwenye Parokia ya Kilungule kuwa Parokia teule itakayosimamiwa na Mapadre wa Shirika la Marian Hill. Mapadre hawa pia wanatoa huduma ya kichungaji Parokia ya Kimara Mtoni! Wakati huo huo, Parokia ya Mtakatifu Veronica, Mwanagati, imekabidhiwa kwa Mapadre wa “Shirika la Heralds of Good News” (HGN) ambao wanafanya pia utume wao katika Parokia ya Mbweni, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Katika mabadiliko haya, Kardinali Pengo amemteua Padre Cletus Mzeru kuwa Padre wa kiroho (chaplain) wa Hospitali ya Jimbo ya Kardinali Rugambwa, Ukonga na ataendelea pia kuwa ni Paroko Msaidizi Parokia ya Ukonga!

Kardinali Pengo

 

21 March 2019, 16:23