Tafuta

Vatican News
Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania: Kauli mbiu "Kuyatakatifuza Malimwengu" Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania: Kauli mbiu "Kuyatakatifuza Malimwengu"  (AFP or licensors)

Jubilei ya Miaka 50 Halmashauri Walei Tanzania: 1969-2019

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yanaongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza Malimwengu”. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yalizinduliwa rasmi na Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hapo tarehe 16 Juni 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu “Harakati za Kitume” (Apostolicam actuositatem” wanatambua mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na hasa nyakati hizi za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Wanawataka waamini walei kutambua kwamba, wanashiriki kikamilifu huduma za Kristo za kikuhani, kinabii na kifalme na kwamba, wanapaswa kutimiza wajibu wao kadiri ya hali yao katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Waamini walei wanamahasishwa kushiriki kwa dhati kabisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Watambue haki na wajibu wao katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Wanayo dhamana ya kuinjilisha kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko na kwamba, wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu, kwani upendo wa Kristo unawawajibisha. Waamini walei wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Utume wao uonekane katika Jumuiya za Kikristo, katika familia na hata katika mazingira ya kijamii: kitaifa na kimataifa!

Jambo la msingi kwa walei kuhakikisha kwamba, wanashikamana na viongozi wao wa Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Halmashauri Walei Tanzania, tarehe 24 Juni 2019 inaadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969 na Hayati Askofu James Sangu aliyekuwa Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kumbe, kuanzishwa kwa Halmashauri Walei Tanzania ni matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Huo ukawa ni mwanzo wa Baraza la Walei ambalo baadaye mwaka 1983 lilifanyiwa marekebisho na kutambulikana kama Halmashauri ya Walei Tanzania.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yanaongozwa na kauli mbiu “Kuyatakatifuza Malimwengu”.  Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yalizinduliwa rasmi na Askofu Desiderius Rwoma, Mwenyekiti Idara ya Utume wa Walei, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hapo tarehe 16 Juni 2018. Katika mahojiano maalum na Vatican News, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania anapenda kukazia umuhimu wa walei kuyatakatifuza malimwengu kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu Rwoma anawahimiza waamini walei wawe mstari wa mbele kulitegemeza Kanisa mahalia kwa hali na mali. Watambue kwamba, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ni sehemu ya wajibu wao kwa Kanisa mahalia. Anazitaka familia ziwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata malezi, makuzi na elimu bora itakayowawezesha kuwa kweli ni Wakristo watakatifu na raia wema wa Tanzania. Wazazi na walezi wawafundishe na kuwarithisha watoto wao fadhila ya uchaji wa Mungu kwani Walatini wanasema, “Sapientia est timor Domini” yaani “watu wawe na hofu ya Mungu”, waogope kutenda dhambi na wawe na upendo kwa Mungu na jirani. Haya ni mambo makuu, yakitekelezwa kikamilifu, kwa hakika waamini walei watakuwa wametimiza wajibu na dhamana yao ya kuyatakatifuza malimwengu!

Jambo la pili, Askofu Rwoma anasema kwa uchungu mkubwa ni “POMBE”. Wataalam wanasema, pombe ni kama uhai wa mtu, ukinywa kwa kiasi! Waswahili wanaongeza chumvi kwa kusema, “Eti, maisha yafaa nini bila pombe?” Pombe imetengenezwa ili iwafurahishe watu! Kunywa pombe kwa wakati wake na kwa kiasi kwaleta burudani na shangwe moyoni”. Sasa hii ndiyo “habari ya Mujini”: LAKINI kunywa pombe kupita kiasi kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha. Ulevi huongeza hasira ya mpumbavu akajiumiza mwenyewe; humdhoofisha na kumwongezea majeraha! Askofu Rwoma anaendelea kudadavua kwa kusema, pombe imekuwa ni chanzo cha majanga mengi katika familia na jamii kwa ujumla! Pombe imekuwa ni chanzo cha magomvi, mafarakano hata mipasuko ya kifamilia na ni chanzo kikuu cha umaskini wa hali na kipato!

Kumbe, watu wanapaswa kuwa na kiasi na wale wasiotumia pombe, waheshimiwe na jamii na kuwa ni mfano bora wa kuigwa! Hakuna mtu ambaye amechelewa kuacha kunywa pombe, inawezekana kabisa, anza leo na wala usingoje kesho! Askofu Rwoma katika mahojiano na Vatican News anakaza kusema, waamini walei wanapaswa kuyatakatifuza malimwemgu kwa kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima yake! Wawe mstari wa mbele kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Waamini walei wawe mstari wa mbele kutoa haki pamoja na kutimiza wajibu! Katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na maendeleo ya teknolojia, waamini walei wawe ni madaraja na vyombo vya majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kweli Tanzania na jirani zake, ili paweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kujikita katika ujenzi wa: umoja, udugu, upendo na mshikamano!

Katika mahojiano haya, Mama Donesta Simon Byarugaba, Katibu msaidizi Halmashauri Taifa ambaye pia ni Mratibu mkuu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Tanzania anasema, maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania yawe ni kumbu kumbu endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni wakati kwa waamini kujiimarisha katika katekesi makini na endelevu kuhusu: Sakramenti za Kanisa, Maandiko Matakatifu pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, nyenzo msingi katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu! Kanuni maadili na utu wema ni mambo ambayo yanapaswa kupewa msukumo wa pekee kwa vijana, ili wasitumbukie katika utamaduni wa kifo na utumwa mamboleo unaofumbatwa katika matumizi haramu ya dawa za kulevya, ulevi na biashara ya ngono.

Mama Byarugaba anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni sehemu ya Injili ya mazingira, kielelezo makini cha umoja na mafungamano ya kijamii kati ya binadamu. Haya ni mafungamano yanayojikita katika mambo makuu matatu: Uhusiano na Mwenyezi Mungu; Uhusiano na Jirani na hatimaye, Uhusiano na dunia yenyewe. Mwanadamu amejeruhiwa kwa dhambi ya asili na matokeo yake yanayojionesha ardhini, majini, hewani na katika aina mbali mbali za mifumo ya maisha sanjari na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Changamoto hizi zinahitaji kwa namna ya pekee kabisa mageuzi kuhusu mtazamo wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, uratibu wa shughuli za kiuchumi pamoja na mitindo ya maisha. Mafundisho ya Kanisa kuhusu kazi ya uumbaji yanakazia kwamba, kama ulivyo uumbaji hata maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya, mwanadamu anaelemewa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kazi ya uumbaji ni hatua ya kwanza katika wito wa mwanadamu yaani: Uumbaji, Umwilisho na Ukombozi. Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania ni wakati muafaka wa kuenzi mazingira nyumba ya wote, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Wakati huo huo,  Thompson Mpanji kutoka Mbeya anasema, habari zaidi kutoka Jimbo kuu teule la Mbeya zinabainisha kwamba,  Padre Sirilo Mwalyoyo, Mkurugenzi wa Utume wa Walei Jimbo kuu teule la Mbeya, katika uzinduzi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Halmashauri Walei Tanzania, amewataka waamini kuwa na hofu ya Mungu kwa kumwilisha Amri za Mungu katika maisha na utume wao, ili ziwe kweli ni dira na mwongozo wa maisha! Ameonya tabia ya waamini kumezwa na malimwengu kwa kutopea katika dhambi na maovu. Wasome na kulitafakari Neno la Mungu; watambue kwamba, wao ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia, kumbe wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini wawe ni washiriki wazuri katika Jumuiya ya Ndogo ndogo za Kikristo, mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa Afrika Mashariki na Kati!

Walei Tanzania 50
13 March 2019, 11:39