Tafuta

Vatican News
Jimbo Katoliki Geita, Tanzania limezindua ujenzi wa Hospitali na Sekondari ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Jimbo Katoliki Geita, Tanzania limezindua ujenzi wa Hospitali na Sekondari ya Mtakatifu Yohane Paulo II. 

Jimbo Katoliki Geita: Ujenzi wa Hospitali na Sekondari! Yaani...

Familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki Geita, Tanzania inaalikwa kuonesha ukarimu kwa Injili, ili kuweza kukamilisha ujenzi wa Hospitali na Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa wakati muafaka. Askofu Flavian Matindi Kassala anawatakia wote paji la elimu katika kudumisha afya na nguvu katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Na Padre Angelo Bartholomeo Shikombe, - Vatican.

Hivi karibuni Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alisikika akisema, kwa sasa kila kijiji nchini Tanzania kina shule ya msingi na ongezeko limefikia idadi ya shule za msingi 17,659 zikiwemo zilizo chini ya Kanisa Katoliki 204. Pia, kuna shule za sekondari katika kila kata, ambazo zipo 4,883 nchi nzima zikiwemo 266 zilizo chini ya Kanisa Katoliki. Idadi hiyo ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu katika ngazi mbalimbali nchini Tanzania!

Ikumbukwe kwamba, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vimekuwa ni vituo vya majadiliano ya kidini na kiekumene; mahali pa kurithisha imani, maadili na utu wema. Kutokana na dhamana hii, vijana wanapaswa kuwa kweli ni wadau wa uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yao adili. Jambo msingi kwa walimu, wazazi na walezi ni kutambua dhamana na utume wa shule za kikatoliki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuwajengea watoto na vijana msingi wa imani, maadili na utu wema. Hapa ni mahali pa kujenga na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani, ili wanafunzi wanaohitimu kutoka katika shule za Kikristo waweze kuwa kweli ni wadau katika kuyatakatifuza malimwengu.

Dunia inawahitaji vijana watakaotoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kwa kutambua kwamba, shule na taasisi hizi ni vyombo makini vya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho! Afya bora ni kati ya haki msingi za binadamu, lakini hadi leo hii, kuna maelfu ya watu ambao hayajabahatika kupata huduma bora ya afya katika maisha yao. Kumekuwepo na maboresho makubwa katika sekta ya afya na tiba, lakini juhudi hizi inazonekana kuwanufaisha watu wachache, wenye uwezo mkubwa kiuchumi. Hali bado ni tete kwa nchi changa zaidi duniani. Changamoto kubwa ni kutokana na umaskini, ujinga na imani potofu. Sekta ya afya kwa sasa inaonekana kujishikamanisha zaidi na watu wenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kwani hata baadhi ya wahudumu wa sekta ya afya wameifanya sekta ya afya kuwa ni mtaji unaoweza kuwaingizia faida kubwa. Sekta ya afya iwe ni mahali pa kujenga na kudumisha mshikamano unaoongozwa na kanuni ya auni kwa ajili ya maboresho ya maisha ya watu wengi duniani!

Ndugu msilkilizaji na msomaji tunakukaribisha na kukushirikisha maendeleo ya uenjilisha yanayofanywa na Kanisa Katoliki ulimwenguni. Leo, tunaelekea Tanzania katika Jimbo Katoliki la Geita lililoanzishwa kunako mwaka 1984. Jimbo Katoliki la Geita ni moja kati ya majimbo yanayojishughulisha na miradi endelevu ya ujenzi wa Hospitali na shule ya Sekondari chini ya usimamizi wa Mhashamu Askofu Flavian Matindi Kassala. Huu ni ujenzi unaofanywa na familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Geita kama sehemu ya ukarimu wa kila binadamu muhitaji katika mazingira mbali mbali. Huu ni mwaliko pia kwa watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na kusikiliza kilio cha maskini, tayari kukipatia majibu kwa mwanga wa Injili!

Askofu Kassala katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, changamoto hii inaongozwa na kauli mbiu “Elimu na afya, nguvu yetu ya Uinjilishaji Geita”. Kwa hakika, huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa na chapa ya kudumu katika utekelezaji wa Injili ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika huduma makini na matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo cha imani tendaji! Hii itakuwa ni Hospitali ya Mtakatifu Yohane Paulo II na Shule ya Sekondari ya Yohane Paulo II, Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa, kutembelea Tanzania na kuwakutanisha waamini wanaounda Jimbo kuu la Mwanza, kilimani Kawekamo, Jimbo kuu la Mwanza kunako mwaka 1990. Papa Yohane Paulo II akabariki Jiwe la Msingi la Kanisa kuu Jimbo Katoliki la Geita; akabariki pia Jiwe la Msingi la Seminari ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Sengerema.

Miradi hii mikubwa imezinduliwa mnamo tarehe 4 Machi, 2019 mjini Geita na Baba Askofu Flavian Kassala ikiwa na malengo ya kumhudumia mwanadamu kimwili na kiroho.  Miradi hii inatarajiwa kughalimu kiasi cha fedha za kitanzania kisichopungua bililioni 2. 9 hadi kukamilika. Katika uzinduzi huu, kiasi cha shilingi milioni 17 zilikusanywa kama kielelezo cha ukarimu wa Kiinjili kutoka kwa familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Geita. Wazo la Kujenga Sekondari ya Wasichana na Wavulana, kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, likiambatana na ujenzi wa Kituo cha Afya (kwa wakati huo), lilianzishwa mnamo miaka kumi iliyopita na Mhasham Askofu Damian Dallu, akiwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita. Mnamo mwaka 2008, Mhashamu Askofu Damian Dallu aliliona hitaji hili la msingi linalotokana na msukumo wa ndani wa utume wa kimisionari unaotambua mahitaji msingi na ya lazima ya kijamii yanayohitaji suluhu.

Aidha, Askofu Dallu alianza kuomba kiwanja cha kujenga shule hiyo katika ofisi za Ardhi hapo Geita. Wazo likiwa ni kujenga shule na kituo cha Afya katika maeneo ya Buhalahala. Hivyo alianza kutafuta pesa za kuanza ujenzi huo kwa kutafuta wafadhili huko Marekani kwa kushirikiana na Padre Mathew Bulala aliyekuwa masoni USA. Mnamo mwaka 2011 ofisi ya ardhi Geita iliweza kulipatia Jimbo katoliki eneo la ekari 80 katika eneo la Bombambili na mchakato wa kupima eneo ulianza na kukamilika 2013. Wazo la Askofu Dallu kujenga shule ya Sekondari lilikuwa ni pamoja na kuwatayarishia watoto yatima toka kituo cha Moyo wa Huruma kinachomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo katoliki la Geita kuanza kutayarisha Sekondari ya kwenda baada ya kuhitimu Darasa la Saba. Toka mwaka 2013 Jimbo liliweza kupata misaada kidogo kidogo ya pesa toka USA ambayo ilisaidia upimaji wa viwanja, na hatua mbali mbali hadi kupata hati Miliki ya eneo lote.

Baada ya Askofu Damian Dallu kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea hapo mwaka 2014, mpango mzima ulisimama ili kusubiria Askofu mwandamizi. Kwa bahati nzuri mnamon mwaka 2015, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Geita aliyeteuliwa kusimamia Jimbo, Askofu Renatus Nkwande, alishauri wazo la ujenzi wa Sekondari liendelee.  Msimamizi wa kitume akishirikiana na Idara ya Maendeleo Jimbo aliweza kupata msaada kidogo toka Canada wa kupanua Zahanati ili iwe ni Kituo cha Afya, lengo likiwa ni kuwasaidia kwa karibu zaidi wanafunzi, yatima, na wananchi wanaokaa katika maenneo ya Bombambili-Geita.

Askofu Renatus Nkwande alitafuta wachoraji wa ramani ya Skondari na Zahanati ili viende kwa pamoja. Mchakato wa kuchora ramani ya Sekondari na Kituo cha Afya uliendelea, na kuliundwa Kamati ya Ujenzi hapo mwaka 2016. Kazi ya matayarisho ya ujenzi iliendelea na hapo tarehe 25 Februari, 2016 Askofu Renatus Nkwandwe alilibariki eneo lote. Baada ya Askofu Flavian Matindi Kassala, kukabidhiwa Jimbo mnamo terehe 12, Juni 2016, aliikuta kazi ya ujenzi ikiwa katika hatua hii na kuanza mara moja usimamizi akishirikiana na Idara ya Maendeleao, na Kamati ya ujenzi. Mhashamu Baba Askofu Kassala baada ya kuona kuwa Hospitali ya Sengerema inayohudumia wananchi wa Wilaya ya Sengerema na wengine wengi kutoka Mkoa wa Geita inazidi kuelemewa,  aliomba  mchoro wa kituo cha Afya upandishwe hadhi ya Hospitali. Wachoraji ramani walirekebisha tena michoro yao kuwa ya Hospitali.

Wakati huohuo, Kamati ya ujenzi ilianza kutafuta mbinu za kupata pesa. Kufikia mwaka 2017, Baba Askofu Kassala aliwaomba wana jimbo la Geita wote waanze kutoa ukarimu wao kwa kuchangia miradi hii. Waamini wa Jimbo la Geita waliipokea miradi hii miwili kwa furaha na upendo mkubwa na kila mmoja alianza kutoa ukarimu wa hali na mali. Ni mwaka huo huo 2017 Waamini wa jimbo la Geita wakiwemo Mapadre na Walei waliomba kuanza na ujenzi wa Hospitali kwa awamu ya kwanza na awamu ya pili kuendelea na ujenzi wa Sekondari. Kamati ya ujenzi ilipokea wazo hilo, na kuanza kwanza kutafuta kibali cha kujenga Hospitali.  Mwaka mzima wa 2018 ulikuwa ni mwaka wa kukamilisha uchoraji ramani ya Hospitali, kukamilisha vibali vya Serkali husani ujenzi ikiwemo na kibali cha NEMC., pamoja na kupata mkandarasi.

Baada ya yote kukamilika, Baba Askofu Kassala alipanga tarehe 4 Machi 2019 iwe siku ya kuzindua na shughuli za ujenzi kuanza mara moja. Hospitali hii ina malengo ya kujibu hitaji la Nyongeza ya Tiba za Afya katika mji wa Geita na Majirani zake ikiwa na mpango wa kuleta vifaa vya kisasa ili watu wasisumbuke kwenda mbali kwa ajili ya utafiti na uchunguzi wa magonjwa Hospitali hii itafanya kazi sambamba na Hospitali yetu Teule ya Sengerema, kwa kushirikiana na Serkali kwenye kitengo cha Afya. Itashirikiana na Asasi zingine zisizo za kiserikali zinazotoa huduma hapa Geita ili kumkomboa Mwanadamu katika mahangaiko ya matibabu sahihi. Katika kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua hii iliyofikiwa Kanisa Katoliki Geita linawaalika watu wote wenye mapenzi mema kuliunga mkono katika shughuli hii ya huduma ili liweze kufikia malengo yake ya kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili bila kubagua dini, kabila, jinsia wala utaifa.

Ni matumaini makubwa ya Askofu Flavian Matindi Kassala kwamba, huduma makini na endelevu ya elimu na afya itasaidia kuimarisha mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kuweza kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu. Hii ni fursa ya kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kujibu kilio cha maskini kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki Geita inaalikwa kuonesha ukarimu kwa Injili, ili kuweza kukamilisha ujenzi wa Hospitali na Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwa wakati muafaka. Askofu Kassala anawatakia wote paji la elimu katika kudumisha afya na nguvu katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Jimbo Katoliki Geita 2019

 

16 March 2019, 12:09