Maaskofu Katoliki DRC: Wanasema, kipaumbele cha kwanza: Ulinzi na usalama; fursa za ajira, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi & wahamiaji Maaskofu Katoliki DRC: Wanasema, kipaumbele cha kwanza: Ulinzi na usalama; fursa za ajira, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi & wahamiaji 

Maaskofu Katoliki DRC: Vipumbele: Usalama, rushwa & wakimbizi

Maaskofu DRC wanasema, bado hali ya usalama na amani ni tete; kuna wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum katika Ukanda wa Kisangani. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma, ni saratani inayoendelea kusigina haki msingi za binadamu nchini DRC na kwamba, ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na ajira ni tishio la amani na mafungamano ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC linasema, bado hali ya usalama na amani inatia shaka; kuna wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum katika Ukanda wa Kisangani. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma, ni saratani inayoendelea kusigina haki msingi za binadamu nchini DRC na kwamba, ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na ajira ni tishio la amani na mafungamano ya kijamii!

Hii ni sehemu ya taarifa iliyotolewa na Maaskofu Katoliki Ukanda wa Kisangani baada ya mkutano wao uliofanyika kuanzia tarehe 5- 7 Machi 2019. Maaskofu wanasema, bado kuna vikundi vya watu wenye silaha vinavyotishia, usalama, amani na haki msingi za wananchi wa DRC. Kuna makundi makubwa ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kutoka Sudan ya Kusini pamoja na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, CAR. Bado kuna Jeshi la Waasi wa Uganda, “Lord’s Resistance Army” ambalo linaendelea kusababisha hujuma kwa wananchi wa DRC pamoja na wanajeshi kutoka Libya wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo!

Migogoro kati ya wakulima na wafugaji Kaskazini Mashariki mwa DRC, inahatarisha ustawi, maendeleo, mafao na mafungamano ya kijamii katika eneo hili. Kumbe, kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama vinawahakikishia wananchi ulinzi na usalama wa maisha na mali zao. Maaskofu Katoliki nchini DRC wanasema, matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 30 Desemba 2018 nchini DRC umewavuruga wananchi wengi na hiki ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha rushwa na ufisadi.

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linasema, litaendelea kukemea vitendo vya kutoa na kupokea rushwa nchini humo kwani vinasigina utu, heshima na haki msingi za binadamu! Maaskofu wanasikitika kuona bado DRC imegawanyika na kwamba, kuna ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na fursa za ajira. Hii ni changamoto ya kichungaji, ambayo Maaskofu wanasema, wanapaswa kuivalia njuga, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Kanisa litaendelea kuwekeza katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, ugonjwa wa Ebola bado ni tishio kwa maisha na usalama wa wananchi wengi wa DRC.

Maaskofu DRC
15 March 2019, 11:45