Tafuta

Askofu mkuu Cristobal Lòpez Romero: Utambulisho wa Kanisa: Majadiliano ya kidini; Uekumene wa huduma ya upendo; Ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! Askofu mkuu Cristobal Lòpez Romero: Utambulisho wa Kanisa: Majadiliano ya kidini; Uekumene wa huduma ya upendo; Ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake! 

Hija ya Papa Francisko Morocco: Utambulisho wa Kanisa Morocco

Papa anakutana na Kanisa ambalo limeotesha mizizi yake Morocco; Kanisa ambalo linajikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na haki: Kanisa la Morocco linajipambanua pia kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kwamba, hili ni Kanisa ambalo ni daraja kati ya Wakristo na Waislam, Kati ya Bara la Afrika na Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Cristobal Lopez Romero wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kitume nchini Morocco kuanzia tarehe 30-31- Machi 2019 ni fursa ya kumkutanisha na mashuhuda wa Kristo Yesu; anakutana na Kanisa ambalo limeotesha mizizi yake nchini Morocco; Kanisa ambalo linajikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na haki: Kanisa la Morocco linajipambanua pia kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene na kwamba, hili ni Kanisa ambalo ni daraja kati ya Wakristo na Waislam, Kati ya Bara la Afrika na Ulaya na kwamba, huu ndio wito wa Kanisa nchini Morocco!

Askofu mkuu Lopez anasema, Wakristo ambao kwa sasa idadi yao inafikia 30, 000 ni alama na vyombo vya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hawa ni waamini wanaotoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni amana na utajiri unaofumbatwa katika umoja na utofauti. Sera na mikakati shughuli za kichungaji nchini Morocco kwa mwaka 2018-2019 zinaongozwa na kauli mbiu “Ujenzi wa umoja, na kuishi katika umoja” miongoni mwa watu wote wa Mungu nchini Morocco. Umoja huu unajikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; ukweli na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; mshikamano na upendo wa dhati.

Waamini wote wanashirikiana na kushikamana kama Kanisa kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, huduma makini kwa watu wa Mungu na mashuhuda wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Hii ni huduma inayotolewa katika sekta ya elimu na afya; ustawi na maendeleo ya wananchi wa Morocco katika ujumla wake. Kwa njia hii, waamini hawa wamekuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na mshikamano wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hili ni Kanisa linalojikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika ukweli na haki; amani, urafiki na maridhiano, ili hatimaye, kushikamana zaidi katika huduma kwa binadamu hasa katika masuala ya elimu, afya, haki msingi za binadamu, maendeleo na ustawi wa wanawake.

Mwelekeo huu wa maisha unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za maisha ya kiroho; sala na imani inayomwilishwa katika matendo! Waalimu wanafundisha katika shule 15 zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Morocco ni: Wakristo na Waislam, wanaowahudumia wanafunzi zaidi ya 12, 000, wote wakiwa ni watoto wanaotoka katika familia za waamini wa dini ya Kiislam. Hili ni Kanisa ambalo limesimikwa katika msingi wa kiekumene kwa kushirikiana kwa karibu sana na “Taasisi ya Kiekumene ya Al Mowafaqa” iliyoko mjini Rabat, ambayo ilizinduliwa kunako mwaka 2012. Tafsiri ya Taasisi hii kwa Kiswahili ni “Muafaka”. Hapa wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanapata mafunzo ya kitaalimungu; wanapata fursa ya kusali na kutafakari Neno la Mungu kwa pamoja.

Hili ni Kanisa linalosimikwa katika Injili ya Msamaria mwema, kwa ajili ya maskini, wakimbizi na wahamiaji, ili kuwawashia tena cheche za matumaini. Hii ni huduma inayosimikwa katika mambo makuu manne kama yanavyotiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapatia hisani. Wote hawa wanahudumiwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Morocco, Caritas Morocco.

Askofu mkuu Cristobal Lopez Romero wa Jimbo kuu la Rabat, Morocco anahitimisha kwa kusema, Kanisa nchini Morocco ni daraja kati ya Afrika na Ulaya. Ni Daraja la Majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, huu ndio wito wa Kanisa nchini Morocco. Kanisa nchini Morocco linataka kuendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha furaha ya Injili! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko ni fursa makini kwa Kanisa nchini Morocco kuweza kufahamika zaidi na zaidi hasa kuhusu maisha na utume wake!

Kanisa Morocco 2019
30 March 2019, 12:00