Afrika Kusini:Tafakari ya vijana kuhusu Sinodi na ombi la siku ya vijana kikanda!
Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican
Vijana waliowakilisha nchi saba za Afrika ya kusini wameunganika kwa pamoja ili kutafakari juu ya hitimisho la Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika mwezi Oktoba 2018 iliyokuwa inahusu vijana, imani na manga’muzi ya miito. Na zaidi vijana waliweza kupata maelekezo ya dhati na ushauri kuhusu Mabaraza ya Maaskofu kwa sababu Sinodi inajikamilisha yenyewe katika jumuiya zao na katika Kanda nzima ya Afrika ya Kusini, kama ilivyo hata katika mabara mengine ya dunia baada ya Sinodi ya maaskofu mjini Roma.
Kushirikishana imani
Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 5-8 Machi 2019 kwa kuandaliwa na Kanda ya Baraza la Maaskofu wa Afrika ya Kusini (IMBISA) ambapo uliwaunganisha vijana kutoka Lesotho, Namibia, Musumbiji, Botswana, Swaziland, Afrika ya Kusini na Zimbabwe. Aliyeongoza shughuli hiyo ni Mike Greef mjumbe wa Chama cha Maristi. Katika majadiliano, yao ndipo ilijitokeza kuona njaa ya vijana ambao wanapenda kuwasiliana kati yao; wazo la kuu la kuweza kufanya siku ya vijana kikanda ambayo inafanana na ile ya duniani.Vile vile katika kujadiliana imewawezesha kila mmoja kutoa mchango ambao kwa pamoja wameonelea kuwa ni fursa ya kutengeneza jukwa la kushirikishana imani katika Kanda hiyo.
Vijana ni cheche za matumaini
Naye Askofu Sephamola Mopeli, OMI wa Qasha's Neck nchini Lesotho, ambaye ni mhusika wa Kitengo cha Kichungaji cha IMBISA amefuatilia majadiliano yao yote na hata meza za mduara. Mwisho wa wa mkutano wao aliemelezea shauku ya vijana katika Sinodi imeweza kuwa cheche za kweli za matumaini katika jumuia zote wanamoishi vijana. Vilevile ameonesha furaha yake ya kuona vijana wakatoliki na wenye akili wanayo ari kubwa ya kutaka kuendeleza shughuli na utume wa Kanisa.
Mikutano iliyotangulia
Hata hivyo IMBISA mwezi Julai mwaka jana, ilikuwa imeandaa Mkutano kabla ya Sinodi kwa ajili ya maaskofu, mapadre na vijana. Na zaidi baadhi ya vijana waliudhuria katika mkutano wa maandalizi kabla ya Sinodi uliofanyika mjini Roma mwezi Machi 2018 na ule ulioandaliwa na IMBISA na vijana wengine walikuwapo katika Sinodi mjini Roma, hata Siku ya Vijana Panama. Kutokana na ushuhuda huo wapo vijana ambao kwa sasa ni wenye uzoefu wa utume wa Kanisa na ambapo yapo matumaini kuwa nguvu hizi na shauku zinaweza kuwasaidia na kuwa mwafaka wa kupelekea mbele utume wa Kanisa endelevu. Vijana pia wameongozwa na tafakari kupitia Wosia wa Laudato si, ili waweze kuwa msitari wa mbele wa kutunza mazingira ambamo ni nyumba yetu ya pamoja.