Cerca

Vatican News
Haki ya kupata maji safi na salama ni changamoto inayohitaji majibu ya haraka Haki ya kupata maji safi na salama ni changamoto inayohitaji majibu ya haraka  (ANSA)

Haki ya maji safi na salama: Changamoto inayohitaji majibu!

Kuna watu zaidi ya bilioni mbili ambao hawana uhakika wa maji safi na salama. Ukame wa kutisha ni chanzo kinachowapelekea watu kuzikimbia nchi na familia zao. Uchafuzi wa vyanzo vya maji na ukosefu wa uhakika wa maji safi na salama ni changamoto pevu hasa katika nchi changa zaidi duniani. Uhakika wa maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maji safi na salama ni kielelezo makini cha upendo uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu kwa binadamu wote! Hii ni haki msingi  inayopaswa kulindwa na kudumishwa na jamii ya binadamu. Maji yasipoheshimiwa yanageuka kuwa ni chanzo cha magonjwa na maafa makubwa kwa mamilioni ya watu duniani. Kumbe, hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, watu wanajenga tabia ya kulinda na kuhifadhi mazingira, kwa ajili ya ustawi na mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho!

Maji safi na salama; chakula na lishe bora ni mambo yanayofungamana kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu! Leo hii kutokana na ukame wa kutisha na uharibifu wa mazingira, kuna uhaba mkubwa wa maji safi na salama; chakula na lishe bora na matokeo yake kuna watoto wanaopoteza maisha kutokana na utapiamlo wa kutisha. Tatizo la maji safi na salama ambayo ni sehemu ya haki msingi ya binadamu bado ni changamoto kubwa sana sehemu mbali mbali za dunia!

Hii ni sehemu ya hotuba elekezi iliyotolewa hivi karibuni na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, kwenye mkutano wa ishirini na mbili wa Ekaristi Takatifu kiuchumi, ambao kwa mwaka huu umejikita zaidi katika kuonesha uhusiano uliopo kati ya rasilimali maji na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Ukosefu wa maji safi na salama na hatimaye, ukame wa kutisha ni hatari sana kwa maisha ya watu kwani maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Leo hii, kuna watu zaidi ya bilioni mbili ambao hawana uhakika wa maji safi na salama. Ukame wa kutisha ni chanzo kinachowapelekea watu kuzikimbia nchi na familia zao. Uchafuzi wa vyanzo vya maji na ukosefu wa uhakika wa maji safi na salama ni changamoto pevu hasa katika nchi changa zaidi duniani. Uhakika wa maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu, inayopaswa kudumishwa na wala haina mjadala.

Maji ni rasilimali kwa ajili ya ustawi,  maendeleo na mafao ya wengi na kamwe haipaswi kubinafsishwa. Maji kadiri ya mapokeo ya kisiasa, kijamii, kifalsafa na kidini ni alama yenye nguvu katika maisha ya watu! Kwa maneno machache, maji ni uhai! Kumbe, dini mbali mbali zinaweza kusaidia katika mchakato wa kulinda na kudumisha vyanzo vya maji sehemu mbali mbali za dunia! Rasilimali maji isipolindwa, ikatunzwa na kuendelezwa, inaweza kuwa ni chanzo kikuu cha mipasuko ya kijamii kwa siku za usoni anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Maboresho haya yanakwenda sanjari na umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema; umuhimu wa kutekeleza dhamana na wajibu katika kulinda vyanzo vya maji, ili jamii iweze kupata maji safi na salama, chachu muhimu sana ya kupambana na magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu! Afya ni haki ya binadamu wote, kumbe, utunzaji bora wa mazingira unaofumbatwa katika ukusanyaji na hifadhi ya taka ni muhimu sana, ili kuboresha mazingira wanamoishi binadamu! Leo hii anasema kuna watu wamekumbwa na magonjwa makubwa makubwa kutokana na uchafuzi wa mazingira, vyanzo vya maji na makazi ya watu hasa kwenye majiji na miji mikubwa zaidi duniani!

Haki Maji Safi & Salama
13 February 2019, 10:44