Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu Umoja wa Falme za Kiarabu inamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa kuguswa na mahitaji ya ndugu zake kiroho! Familia ya Mungu Umoja wa Falme za Kiarabu inamshukuru na kumpongeza Papa Francisko kwa kuguswa na mahitaji ya ndugu zake kiroho!  (Vatican Media)

Familia ya Mungu Umoja wa Falme za Kiarabu inamshukuru Papa!

Baba Mtakatifu Francisko, kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi naye amefika katika nchi ya Kiislam kama alivyofanya Mtakatifu Francisko kunako mwaka 1219, kwa kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu Ukristo wao kwa kukazia mambo msingi ya maisha ya kiroho! Hakuna sababu za malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko! Hapa ni ushuhuda wa imani tu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Paul Hinder, Msimamizi wa Kitume huko Umoja wa Falme za Kiarabu, Oman na Yemen kwa niaba ya familia ya Mungu iliyojumuika tarehe 5 Februari 2019 kuadhimisha mafumbo ya Kanisa pamoja na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Uwanja wa Uwanja wa Michezo wa Zayed huko Abu Dhabi,  pamoja na mamilioni ya watu walioshiriki kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, amemshukuru kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu kwa kujali na kuguswa na mahitaji ya kichungaji ya Wakristo huko Umoja wa Falme za Kiarabu, wanaotoka sehemu mbali mbali za dunia.

Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, naye amekuja ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Wanapenda kumhakikishia sala na uaminifu wao kwake. Imegota miaka 800 tangu Mtakatifu Francisko wa Assisi alipokutana na Sultan Malik Al Kamili huko Misri. Huu ni mkutano ulioshuhudia umuhimu wa kuheshimiana na kuthaminiana! Baba Mtakatifu kwa kufuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi naye amefika katika nchi ya Kiislam kama alivyofanya Mtakatifu Francisko kunako mwaka 1219, kwa kuhakikisha kwamba, wanaishi kikamilifu Ukristo wao kwa kukazia mambo msingi ya maisha ya kiroho!

Hakuna sababu msingi ya kuanzisha malumbano yasiyokuwa na tija wala mvuto, jambo la msingi ni kutambua tu kwamba, wao ni Wakristo. Askofu Paul Hinder, amemshukuru kwa namna ya pekee kabisa, Mfalme mrithi  Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan aliyehakikisha kwamba, hija hii ya kitume inafanikiwa katika kiwango cha hali ya juu kabisa. Ndiye yeye aliyetoa kibali cha kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu uwanjani hapa. Amewashuruku waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliojisadaka kuhakikisha kwamba, matukio yote haya yanafanikiwa! Mwishoni, amemwomba Baba Mtakatifu Francisko kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema baraka zake za kitume!

Askofu Hinder: Shukrani
05 February 2019, 13:52