Tafuta

Vatican News
tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Mwaka C wa Kanisa: Wito na Utume wa Unabii tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Mwaka C wa Kanisa: Wito na Utume wa Unabii  (AFP or licensors)

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Mwaka: Kristo Nabii!

Kristo Yesu ndiye nabii mkuu, ndiye utimilifu wa unabii, ni kwa ajili yake walipata kuwapo manabii wote wa Agano la Kale na ni kwa jina lake kanisa linapata utume wake wa kinabii. Kristo ndiye unabii kwa sababu unabii linaoutekeleza Kanisa ni kufundisha ukweli kama ulivyofunuliwa na Kristo mwenyewe.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 4 ya Mwaka C wa Kanisa. ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Yer 1:4-5, 17-19) ni kutoka katika kitabu cha nabii Yeremia na linazungumzia mwito wake kwa kazi ya unabii. Ni mwito ambao kama ulivyo mwito mwingine wowote wa kitume unaanza kwa kumkutanisha Yeremia na uwepo wa kimungu. Uwepo huu kwa Yeremia unakuwa ni kwa njia ya Neno la Bwana. Mungu anajitambulisha kwake kwa Neno.

Wito wa Yeremia ni uchaguzi wa moja kwa moja wa Mungu na wala si kwa chochote alichofanya Yeremia. Mungu alimjua kabla hajazaliwa na alimtakasa akingali tumboni mwa mama yake akamuweka nabii wa mataifa. Yeremia alizaliwa awe nabii. Na kumbe katika mipango hiyo ya Mungu Yeremia asingeweza kuepuka kuwa nabii na hata baada ya kuupokea unabii hana nafasi ya kuuacha tena, wito wake umeungana moja kwa moja na maisha yake. Yeremia anapoitwa anaambiwa ajifunge viuno. Anaalikwa kufanya maandalizi binafsi, ajiandae kikamilifu na aweke jitihada binafsi kuyakabili majukumu ya wito alioitiwa. Neema ya Mungu inayomjia mtu katika wito inahitaji mazingira mazuri ndani ya anayeipokea. Na mwisho Mungu anamhakikishia ulinzi na uangalizi wake katika kazi yote ya unabii anayomwitia.

Somo la pili (1Kor 12:31-13:13) ni Waraka kwa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorintho. Ni somo linalojikita katika upendo na linatoa mwaliko huo kwa utenzi ambao kwa hakika tumekwishausikia mara nyingi. Mazingira ya Paulo kuleta fundisho hili kuu kuhusu upendo ni yaleyale ya mgawanyiko na mpasuko katika jumuiya ya wakristo wa Korintho. Paulo alianza kwanza kwa kuwakemea wasiendekeze utengano bali wajenge umoja, wasiseme huyu ni wa Paulo, huyu ni wa Kefa na kadhalika kwa sababu Kristo hajagawanyika. Na katika dominika iliyopita aliwaletea mfano wa mwili mmoja ulio na viungo vingi, bado kukazia suala hilo hilo la umoja akiwaasa kutumia vema karama walizopewa na Mungu si kwa faida binafsi bali kwa manufaa ya jumuiya. Kama mwendelezo na kilele cha mausia yote hayo, Paulo analeteta fundisho leo juu ya upendo.

Anaanza na kunena kwa lugha; kitu ambacho wakorintho walikionea fahari kama alama ya juu kabisa ya ukamilifu, na anawaambia kunena huko ni bure kama anenaye hana upendo. Anagusia unabii na ujuzi wa elimu na maarifa. Walikuwapo manabii wa miungu ya kigiriki lakini hata kati ya wakristo walikuwapo wajuzi waliobobea katika elimu ya falsafa ya kigiriki. Yote hayo anasema yakifanyika bila upendo si kitu. Na hatimaye anataja wanaojipatia umaarufu kwa matendo ya imani kama miujiza ya kushangaza, kuhamisha milima na wale wanaojipatia umaarufu kwa ukarimu wa kujionesha – kuwalisha masikini na mengineyo – kuwa yote hayo si kitu bila upendo. Yataendelea kugawa jumuiya tu hata kama machoni pa watu yanaonekana ni mambo ya kuvutia na ya fahari.

Katika hatua ya pili Paulo anaonesha ni yepi sasa yaliyo matendo ya upendo. Anataja uvumilivu, fadhili, kutokuwa na husuda, kutojivuna na orodha inaendelea. Mwisho anaulinganisha upendo na fadhila nyingina na kuonesha kuwa fadhila nyingine mtu akiwa nazo zinaweza kufika mahala zikakoma ila upendo hapana. Ndio unaoziunganisha fadhila zote na ndio kama kiungo kinachozipa ladha fadhila nyingine zote njema za kikristo. Upendo unadumu.

Injili (Lk 4:21-30) Injili ya leo inaturudisha katika siku ya kwanza Yesu alipoanza utume wake wa hadhara kadiri ya mwinjili Luka. Siku alipoingia katika sinagogi akasoma andiko la Nabii Isaya “Roho wa Bwana yu juu yangu”. Injili ya leo inaanza kwa maneno ya Yesu baada ya kusoma andiko la Nabii Isaya, anasema “leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu”. Pamoja na kuonesha kuwa yote yaliyoandikwa na manabii yanatimia katika nafsi yake, Yesu anawaambia wayahudi kuwa muda wa kumsubiria masiya umekwisha, masiya amekwishafika. Na kimsingi anawaambia yeye ndiye huyo masiya waliyekuwa wakimsubiri.

Kinachotokea ni kwamba watu hawaamini na zaidi ya hapo wanamdhihaki “huyu si mwana wa Yusufu… tabibu jiponye mwenyewe..” lakini Yesu anawakumbusha mifano ya kilichotokea enzi ya nabii Eliya na enzi za nabii Elisha. Na kilichotokea kipindi hicho ni kwamba waliowapokea manabii hao na kunufaika na nguvu ya Mungu iliyokuwa inafanya kazi ndani yao hawakuwa waisraeli. Anawataja mjane wa Serepta katika nchi ya Sidoni na Naamani mtu wa Shamu. Waisraeli hapana. Na hivi anawatahadharisha kuwa wao nao waangalie wasiingie katika mkumbo huo. Mkumbo wa kuruhusu ugumu wa mioyo yao ufunge milango ya kupokea ukombozi kutoka kwake. Anawaonesha kuwa kazi ya Mwenyezi Mungu haina mipaka wala ubaguzi, wale wanaoendekeza mipaka na kuwabagua wengine, wao wenyewe hujikuta nje ya mpango wa ukombozi wa Mungu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo yetu ya leo yanatuingiza katika tafakari pana ya unabii wa Kristo, unabii ambao umekuwa chemichemi ya utume wa kinabii kwetu sote tuliobatizwa kwa jina lake. Kristo ndiye nabii mkuu, ndiye utimilifu wa unabii, ni kwa ajili yake walipata kuwapo manabii wote wa Agano la Kale na ni kwa jina lake kanisa linapata utume wake wa kinabii. Kristo ndiye unabii kwa sababu unabii linaoutekeleza Kanisa ni kufundisha ukweli kama ulivyofunuliwa na Kristo mwenyewe.

Katika unabii huu wa Kristo, leo tunaalikwa kwanza kuutwaa wajibu wetu wa kinabii. Tunasema kuutwaa kwa sababu tayari kwa njia ya ubatizo kila mmoja wetu anajaliwa kushiriki katika unabii huo. Lakini kwa namna ya pekee kabisa masomo ya leo yanatuonesha kuwa utume wa unabii huambatana pia na kukataliwa. Kupo kukataliwa kwa yule anayetekeleza unabii lakini pia kupo kukataliwa kwa ujumbe anaoutoa. Ndivyo pia ilivyotokea kwa Yesu akiwa kwao Nazareti, ilitokewa kwa manabii wa Agano la kale na inatokewa hadi leo katika  Kanisa. Swali tunaloweza kujiuliza ni moja tu, kwa nini? Je ni mapenzi ya Mungu kuwa ujumbe wake ukutane na vikwazo na kukataliwa? Au Je ukweli wa kimungu umepoteza uhalisia au unakosa uhalisia kwenye maisha ya mwanadamu? Ni kwa sababu ya wajumbe wa unabii au walengwa wa unabii? Kwa nini?

Kwa hakika ni vigumu kupata jibu moja linaloweza kutosheleza kuelezea kukataliwa kwa utume wa unabii kwa sababu ya utofauti wa mazingira na changamoto zinazobadilika badilika kadiri ya nyakati. Pamoja na hayo, mwaliko wa Mtume Paulo katika somo la pili unatupatia msingi mzuri wa kuanzia: mwaliko wa kuyafanya yote kwa upendo. Anayeupokea utume wa unabii, aupokee kwa upendo. Aufikishe kwa watu kwa upendo na autekeleze kwa upendo. Wale wanaofikishiwa ujumbe wa unabii wausikie kwa upendo na waupokee kwa upendo na upendo ukiwa katikati ya yote utaleta matunda katika utume mzima wa unabii Kristo aliloliachia Kanisa lake na anaowapa wote wanaobatizwa kwa jina lake.

Liturujia J4 ya Mwaka C wa Kanisa

 

02 February 2019, 11:17