Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Mtawatambua watu kwa maneno na matendo yao! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Mtawatambua watu kwa maneno na matendo yao! 

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VIII: Acha unafiki!

Yesu anatutahadharisha kwamba, inawezekana watu hawa kwa nje wakavaa ngozi ya kondoo wakati kwa ndani ni mbwa mwitu wenye kurarua na kutafuna wengine. Ndiyo maana lazima kuwapima endapo nia yao, mitazamo na maneno yao vinaendana na mafundisho ya Injili. Zaidi ya hapo lazima kuyaangalia pia matunda yao katika jamii.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S., - Vatican.

Katika maisha na mahusiano yetu ya kila siku: kwenye familiya zetu, sehemu za kazi, katika jumuiya zetu za kitawa na ndani ya Kanisa, tunatambua jinsi ilivyo rahisi kuona makosa ya wengine na kuwahukumu wakati ambapo tunashindwa kuona makosa na mapungufu yetu wenyewe. Wewe na mimi leo hii Yesu anatuambia, “Mnafiki wewe, itoe boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.”

Injili ya leo inakamilisha ile hotuba ya Yesu juu ya mambo muhimu kuhusu maisha na mwenendo wa kila aliye mkristo. Katika Dominika mbili zilizopita Yesu amekuwa akitoa mafundisho ambayo kwa mtazamo wa kibinadamu ni magumu kuyapokea. Tumemsikia Yesu akiwatangaza kuwa wana heri wale ambao ni masikini, wenye njaa, wale wanaolia na wanaoteswa kwa ajili yake. Hakika dunia inawaona watu hawa kuwa ni watu wasio na furaha. Pia Yesu anawapa ole wale ambao dunia inawatazama kama watu walio na bahati: matajiri, walioshiba, na wale wanaoponda raha katika maisha.

Kama haitoshi, Yesu anawafundisha wafuasi wake kwamba hawapaswi kulipa ovu kwa ovu bali wanatakiwa kuwapenda na kuwatakia mema maadui zao. Haya yote ni mafundisho magumu ambayo mara nyingi tunashindwa kuyatekeleza. Mara nyingi Injili inatukwaza kwa sababu inatutaka tubadilike. Badala ya kubadilika tunajaribu kupindisha na kuupoza ujumbe wa Injili ili uendane na mitazamo yetu binafsi. Mbaya zaidi tunawafundisha wengine kuamini na kutenda kadiri ya mitazamo hiyo. Mfano wapo wakristo ambao husema kuwa ni kweli mkristo hapaswi kulipa kisasi lakini adui anapozidi lazima kumfundisha somo, yaani kulipa kisasi. Baadhi ya wazazi na walezi huwafundisha watoto wao kulipa kisasi pale ambapo watoto wenzao wananyanyua mkono kuwapiga.

Kuna mifano mingine mingi katika nyanja mbalimbali za maisha ambapo tunajikuta tukipotosha ukweli wa Injili. Hata mwaliko ambao Yesu anatupatia leo hii wa kuingia ndani ya dhamiri zetu na kuyafanyia kazi mapungufu yetu kabla ya kuangalia mapungufu ya wengine si jambo rahisi kufanya. Tunahitaji kuwa wanyenyekevu kufanya hivyo. Tunakumbuka kuwa siku moja wafuasi wa Yesu walimwendea Mwalimu wao na kumwambia kuwa mafarisayo wanakwazwa na maneno yake. Kwa kweli ilikuwa ni haki yao kukwazwa naye kwa sababu mitazamo yao ilikuwa ni mitazamo ya kidunia.

Naye Yesu akawajibu wanafunzi wake akisema, “Waacheni; hao ni viongozi vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.” (Mt.15:14). Hata hivyo katika mazingira ambayo Mwinjili Luka anatupatia Injili ya leo, walengwa si Mafarisayo au Wayahudi bali wafuasi wake mwenyewe kwani hata wao wako katika hatari ya kuwa viongozi vipofu. Ujumbe huu ni muhimu hasa kwetu sisi ambao tunajiamini kupita kiasi na tuko tayari kutoa maelekezo ya kuwarekebisha wengine huku tukisahau kujitafiti mioyo yetu wenyewe na kujirekebisha.

Kanisa la karne za mwanzo wale wote waliokuwa wamebatizwa walijulikana kwa jina la “walioangaziwa”. Hii ni kwa sababu mwanga wa Kristo ulikuwa umewafungua macho ili kuweza kuitazama dunia na kuwatazama wengine kwa jicho la Mungu. Huu ni ukweli ambao unapaswa kuongoza maisha yetu hata leo. Sisi sote tuliobatizwa tunapaswa kuwa na uwezo wa kuishi na kuwaongoza wengine kadiri ya mapenzi ya Mungu. Ili kufanya hivyo lazima tuwe tumeunganika kabisa na kujiweka chini ya maongozi ya Yesu aliye Mwalimu na Kiongozi wetu. Kinyume cha hapo kuna hatari ya kuwapotosha wengine.  

Jukumu la kiongozi yeyote si kuwavuta watu kwake bali kuwapeleka kwa Yesu. Kiongozi anaposahau kuwa yeye naye ni mfusi wa Yesu, hujikuta akijiweka juu ya Yesu na kufanya mambo ambayo hata Yesu mwenyewe hakutaka hakuyafanya. Huwahukumu wengine bila huruma na huwatangazia adhabu kali dhidi yao. Yesu anawaita wanafiki wale wote wanaowahukumu wengine na anatualika sisi sote kuingia ndani ya dhamiri zetu na kuona jinsi tulivyo. Kama tutafanya hivyo bila kujihurumia tutagundua kuwa sisi ni wadhambi pengine zaidi ya wale tunaowahukumu. Hivyo tutatambua kuwa ni sisi ambao tunahitaji kuongoka kwanza ili tuweze kuwasaidia wengine.

Ni mwaliko mgumu kidogo kwa kuwa unatuhitaji kuwa wanyenyekevu n amara nyingi hatupendi kuwa wanyenyekevu. Hata hivyo hakuna jinsi lazima tufanye hivyo ili kuondoa boriti lililopo katika jicho letu na ambalo linatuzuia kuona vizuri. Kila moja wetu ana boriti lake jichoni linalomzuia asione sawasawa. Boriti hili linaweza kuwa ni la chuki, kiburi, majivuno, dharau, masengenyo, ujinga, na tamaa ya kuwatawala wengine na kadharika. Mambo hayo na mengine mengi kama hayo ni boriti zinazotuzuia kuona vizuri kama jinsi aonavyo Mungu na zinatufanya tuwahukumu wengine kwa ukali tofauti na huruma ya Mungu kwa watu hao. Mbaya zaidi tunaweza kujikuta kuwa tuna zaidi ya boriti moja machoni hiyo tunakuwa vipofu wanaotembea katika giza totoro.

Yesu anatualika sisi sote tuwe wanyenyekevu kwake. Anasema kuwa mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini mwanafunzi aliyehitimu vizuri, yaani aliyefuatilia vizuri mafundisho ya mwalimu wake hulingana na mwalimu wake. Jambo hili linatupa faraja kwamba endapo tutazingatia na kuishi mafundisho yake twaweza kufanana naye katika namna yetu ya kuwaza, kuchagua na kutenda. Hapo ndipo tunapoweza kuwaongoza wenzetu, nasi tunaweza kuwa walimu wadogo, yaani wasaidizi wake. Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia waalimu kama hawa wanaotuongoza katika njia ileile aliyopita Yesu.

Hata hivyo Yesu anatambua kuwa wapo walimu wengine wa uwongo japo wanakuja kwa jina lake. Dunia yetu ya leo imejaa walimu kama hawa ambao Yesu anatutaka tujiepushe nao. Anatupatia pia vigezo vya kuwapima na kuweza kuwatambua na kuwatofautisha na wale walimu wema. Mara nyingi tumezoea kuwasifu na kuwahesabu watu kuwa ni wema kutokana na mambo mbalimbali ambayo huyafanya kwa nje. Yesu anatutahadharisha kwamba inawezekana watu hawa kwa nje wakavaa ngozi ya kondoo wakati kwa ndani ni mbwa mwitu wenye kurarua na kutafuna wengine.

Ndiyo maana lazima kuwapima endapo nia yao, mitazamo na maneno yao vinaendana na mafundisho ya Injili. Zaidi ya hapo lazima kuyaangalia pia matunda yao katika jamii. Kipimo anachokitumia Yesu ni kipimo kilekile ambacho Yoshua Bin Sira anakitumia katika somo la kwanza. Tunaweza kuwatambua walimu wa uwongo kutokana na maneno na mitazamo yao ambayo hayajengi bali hubomoa, huleta ubaguzi, chuki, utengano na mafarakano katika jamii. Walimu na viongozi wema ni wale ambao maneno na mitazamo yao hujenga, huleta umoja na mshikamano katika jamii. Ni wale ambao hujiweka chini wa maongozi ya Roho wa Kristo na kazi zao huleta matunda ya upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi.

Ndugu yangu wewe na mimi hatuwezi kukwepa kuwa viongozi katika maisha yetu ya familia, kazi na jumuiya mbalimbali katika Kanisa na jamii. Leo hii kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza, ni nani au ni nini msingi unaongoza maisha yangu? Je, ninafanya nini ili kuondoa boriti lililopo katika jicho langu?

Jumapili 8 ya Mwaka
28 February 2019, 14:59