Tafuta

Vatican News
Upendo kwa Mungu na jirani ndio dira na mwelekeo wa maisha ya Kikristo! Upendo kwa Mungu na jirani ndio dira na mwelekeo wa maisha ya Kikristo!  (Vatican Media)

Tafakari Neno la Mungu Jumapili VII ya Mwaka: Upendo kwa jirani!

Kristo Yesu, kwa maisha na matendo yake ametupa kielelezo na mfano halisi wa huruma na upendo wa Mungu. Tunatambua fika ni jinsi gani katika maisha yake ya utume hapa duniani alivyowahurumia na kuwapenda watu huku akiwasamehe wakosefu. Upeo wa huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu wote unajidhihirisha katika Fumbo la Msalaba.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. –Vatican.

Leo tunapewa changamoto kubwa: “Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.” Huu ndiyo ujumbe mkuu katika Dominika hii ya saba. Tukisoma katika Injili ya Mtakatifu Mathayo 22: 35-40 na katika Injili ya Mtakatifu Marko 12: 28-34, tunamkuta Bwana wetu Yesu Kristo akiongelea juu ya amri iliyo kuu kuliko amri zote, ambayo ni upendo. Amri hii kiuhalisia imegawanyika katika sehemu mbili yaani upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Amri hii ndiyo msingi unaopaswa kuongoza mtindo wa maisha ya kikristo.

Yesu kwa kuongea juu ya upendo hakuwa anaongea juu ya kitu kipya. Upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani ulikuwa pia ndiyo msingi wa maisha ya Waisraeli kama tunavyosoma katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 6: 4-5 na katika kitabu cha Walawi 19:18. Pamoja na hayo Yesu alileta upya wa amri ya mapendo pale aliposema, “…mpendane kama kama vile nilivyowapenda ninyi.” (Yohane 13: 34). Hapa Yesu anatualika tumtazame yeye kama kigezo cha kuelekeza upendo wetu kwa wengine na si kutumia vigezo vyetu wenyewe. Kuna msemo wa Kiswahili unaosema, “mpende akupendae, usimche asiyekupenda”. Huu si mtazamo wa waswahili tu bali ni mtazamo wa kibinadamu kwa jumla.

Kwa kawaida tunawapenda wale wanaotupenda, wale ambao ni marafiki zetu, wale wanaotufurahisha na wale wanaotuunga mkono kwa namna moja au nyingine. Tunapenda kuwalipa fadhila wale wanaotufadhili na kututendea mema na hao ndo tunaowaombea baraka kwa Mungu na mafanikio katika maisha yao. Kinyume chake, wale wanaotuchukia au kutupinga kwa namna fulani tunawahesabu kuwa ni maadui zetu. Huwa hatuko tayari kushirikiana nao, tunawabagua na tunajiweka mbali nao. Hawa wanapotukosea au kutuumiza, sisi nasi tunatafuta namna ya kulipa kisasi. Si rahisi kwetu kuwaombea mema watu hawa bali huwa tunawaombea mabaya kama msemo mwingine wa Kiswahili unavyosema, “adui yako mwombee njaa.”

Kinyume na mtazamo huo wa kibinadamu Yesu anataka kila aliye mfuasi wake awe tayari kuwapenda hata maadui zake, kuwatendea mema wale wote wanaomdhulumu au kumtendea ubaya. Fundisho hili la Yesu lina msingi wake katika huruma na upendo wa Mungu. Huyu ndiye Mungu waliyemfahamu Waisraeli katika historia na uhusiano wao naye. Mara nyingi Waisraeli walilivunja Agano na Mungu, wakakosa uaminifu kwake na kujiweka mbali naye. Kwa mwenendo wao huu walistahili adhabu lakini mara zote Mungu alijidhihirisha kwao kuwa ni Mungu mwenye subira, upendo na mwenye kusamehe daima. Huu ndiyo ukweli ambao mzaburi wa Zaburi ya 102 anaoushuhudia akisema, “Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, wala hakutulipa kadiri ya maovu yetu.” Huyu ndiye Mungu ambaye Yesu alikuja kutufunulia hapa ulimwenguni. Yesu anapotufundisha kuwapenda adui zetu anataka tufanane na Mungu Baba yetu aliye na upendo na huruma kwa watu wote.

Pamoja na kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo, mara nyingi tunashindwa kufuata fundisho hili. Katika somo la kwanza Daudi anatupa changamoto kwamba yawezekana kuishi fundisho hili endapo tutaamua huku tukisaidiwa na neema toka kwa Mungu. Kwa sababu ya husuda na wivu dhidi ya mafanikio ya Daudi, Sauli alijikuta akijenga uadui dhidi ya Daudi na alikuwa akitafuta kila njia ili aweze kumwangamiza.  Wakati ambapo Daudi alikuwa na uwezo wa kumtenda lolote adui na mtesi wake, yeye anaamua kutomtenda ubaya. Anakataa ushauri wa Abishai wa kutaka kumdhuru Sauli, anaamua kumsamehe. Huu ni mfano mzuri wa jinsi ambao Yesu anataka sisi tuliowafuasi wake tuishi.

Kwa bahati nzuri, Yesu hatufundishi Injili kwa maneno au kwa nadharia tu bali yeye mwenyewe alikuwa wa kwanza kuiishi Injili hiyo. Kwa maisha na matendo yake ametupa kielelezo na mfano halisi wa huruma na upendo wa Mungu. Tunatambua fika ni jinsi gani katika maisha yake ya utume hapa duniani alivyowahurumia na kuwapenda watu huku akiwasamehe wakosefu. Upeo wa huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu wote unajidhihirisha Msalabani ambapo Yesu anatoa maisha yake na anamwaga Damu yake kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu wote. Yeye mwenyewe alisema hakuna upendo mkubwa zaidi kuliko wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Rej. Yohane 15: 13).

Tunapotaka kujua ni nini maana ya kuwapenda maadui lazima tusogee chini ya Msalaba wa Yesu. Katika ukimya tutasikia sauti yake ikisema, “Baba uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo.” (Luka 23:34). Anachokifanya Yesu hapa ni kinyume kabisa na kile ambacho sisi hufanya mahakamani. Yesu akiwa msalabani katika mateso makali na mahangaiko makubwa, anapata nguvu ya kwatetea watesi na wauwaji wake, akiwaombea msamaha kwa Hakimu mwenye haki. Si kawaida yetu kumtetea mtuhumiwa mahakamani. Huwa tunajaribu kutafuta kila ushahidi hata wa uongo ili mradi mtuhumiwa aweze kutiwa hatiani na kuhukumiwa.

Siyo rahisi kuichagua njia hii anayotuamuru Yesu kuifuata. Tunahitaji neema na msaada wa pekee kufanya hivyo. Kila tunapoyaelekeza macho na mioyo yetu na kumtazama Mungu Baba mwenye kuwapenda watu wote bila ubaguzi tunapata neema na nguvu ya kuwapenda wengine kama Mungu anavyowapenda. Yeye huruhusu mvua inyeshe kwa wema na wabaya. (Rej. Mathayo 5: 45). Tukitaka kuwapenda na kuwasamehe maadui wetu lazima tusogee chini ya Msalaba wa Yesu na turuhusu sala yake kwa Mungu Baba kwa watesi wake iwe sala yetu. Tunatiwa nguvu pia na maombezi ya watakatifu ambao walijitahidi kufanana na Yesu katika maisha yao na hata katika kifo.  Akiwa kufani kwa kupigwa mawe, Mtakatifu Stefano alifanana na Yesu kwa kuwaombea msamaha wauaji wake akisema, “…Bwana usiwahesabie dhambi hii.” (Matendo 7: 60). Kwa maombezi yake na maombezi ya watakatifu wote tujaliwe neema ili mioyo yetu ifanane na Moyo Mtakatifu wa Yesu wenye kuwapenda wote hata maadui.

Jumapili 7 ya Mwaka
22 February 2019, 15:48