Tafuta

Manabii ni wajumbe wa Neno la Mungu kati ya watu wao! Manabii ni wajumbe wa Neno la Mungu kati ya watu wao! 

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili IV ya Mwaka C: Unabii

Ugomvi ulitokea pale ambapo Yesu alipoongea ukweli juu ya mapenzi ya Mungu. Yeye alikuwa Nabii, Yule ambaye anaongea mahali pa Mungu, msemaji wa Mungu. Alama ya unabii ni hii ‘hivi ndivyo asemavyo Mungu’. Nabii huongea Neno la Mungu iwe linafaa au halifai. Nabii husema ukweli mchungu, na hapa ndo ugomvi huanza. Somo la Injili laonesha wazi hali hiyo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mhubiri maarufu Padre Munachi anasimulia kisa cha Askofu mmoja mzalendo huko Nigeria ambaye baada ya kupata daraja la uaskofu, anarudi katika jimbo lake na kupata mapokezi makubwa. Watu wale walikuwa na imani ya kawaida tu na hata pengine hawakujua vizuri nafasi ya cheo cha askofu katika kanisa katoliki. Wengi walimpongeza kama mtu ambaye tayari njia yake ya mbinguni iko wazi. Wakamwahidi kuwa wangekuwa wote wakristo kama angeondoa amri moja katika amri kumi. Kabla hawajasema ni amri ipi, askofu akawakumbusha kuwa amri za Mungu haziwezi kuguswa na mwanadamu. Hapa sherehe yote ikaharibika. Ilibidi askofu aondoke haraka katika mazingira yale kwani hali ilikuwa mbaya kabisa. Hiki ndicho kilichompata Yesu pia katika Injili ya leo.

Kama yule Askofu, hapa tunaona Yesu anarudi nyumbani mara baada ya ubatizo wake ambapo Roho Mtakatifu anashuka juu yake na anatangazwa kuwa ni mwana mpendelevu wa Mungu. Na watu wake walimpokea kwa shangwe. Wote waliongea vizuri juu yake. Ugomvi ulitokea pale ambapo Yesu alipoongea ukweli juu ya mapenzi ya Mungu. Yeye alikuwa Nabii, Yule ambaye anaongea mahali pa Mungu, msemaji wa Mungu. Alama ya unabii ni hii ‘hivi ndivyo asemavyo Mungu’. Nabii huongea Neno la Mungu iwe linafaa au halifai. Nabii husema ukweli mchungu, na hapa ndo ugomvi huanza. Somo la Injili laonesha wazi hali hiyo. Ukweli anaosema Yesu upo katika Injili ya leo ni kwamba kulikuwa na wajane wengi …. Wao waliamini Mungu ambaye walimtengeneza wao. Walibinafsisha mapenzi ya Mungu na kujiona kuwa wao ndio wateule tu na wengine hawawezi kupata nafasi hii. Hivyo hawakuwa tayari kupokea ukweli mwingine.

Katika somo la kwanza tunaona habari juu ya ufunuo wa upendo mkuu wa Mungu – kabla sijakuumba nilikujua na kabla hujuzaliwa nalikutakasa – nabii alitengwa kwa ajili ya Mungu. Sisi katika ubatizo ni kama nabii – kumwabudu Mungu, kutii amri zake, kutangaza Neno lake, kutumikiana na kupendana. Wito wetu ni kuwa tayari – 1Fal. 18:46, Ayu. 38:3; 40:7, Mt. 25:13. Hakuna ajuaye kitakachotokea kwanza – kama Bwana Yesu atarudi na utukufu na malaika wake mwisho wa nyakati au kama tutaitwa mbele ya kiti cha haki mwisho wa maisha ya hapa duniania. Mt. Pt. 1Pt. 5:6-10 anatoa jibu – basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari … muwe na kiasi, kesheni n.k

Katika somo la pili – Wakorintho wanashindana ni zawadi ipi ni kubwa zaida – kuongea kwa lugha, unabii, ufahamu wa fumbo la Mungu au imani. Mt. Paulo anasema ni upendo. Ule upendo utokao kwa Mungu kwa njia ya Kristo. Upendo usio na mipaka – Agape – upendo utokao kwa Mungu Baba kwa njia ya mwanae.  Sababu ya ukuu wa upendo ni kwamba watoka kwa Mungu. Vipaji vya Roho Mtakatifu vina ukomo, isipokuwa upendo. Sababu Mungu ni upendo – 1Yoh. 4:8 na kwamba upendo watoka wa Mungu – 1Yoh. 4:7 na wote wampendao wabaki kwake – 1Yoh. 3:24.

Pengine hatuoni kitu cha pekee sana, yaani kama changamoto kutoka masomo yetu ya leo. Kikubwa tulichona ni ule utayari wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Tumeona katika maisha ya Yesu, ya nabii Yeremia na katika somo la pili. Je ni kwa namna gani tunaweza kufananisha maisha yetu na na maisha yao? Kwamba ‘hivi ndivyo asemavyo Mungu? Na kusema tu ukweli wa Neno la Mungu hata kama hili litagharimu maisha yetu? Mtu mmoja amekuwa akirudia kusema na hasa anapopata changamoto katika kuutafuta ukweli kuwa watu wengi wanasema kile wasichonuia. Kwa maana nyingine wengi wetu hatusemi ukweli ulivyo. Padre Ricardo Maria amekuwa anaendesha kipindi hasa kupitia Redio Ukweli ya Jimbo Katoliki Morogoro – ‘ukweli ulivyo’ na katika kipindi hiki huwa anarudia tu na tena kwa msisitizo mafundisho ya Kanisa Katoliki jinsi yalivyo bila kupindisha ukweli au kuongeza neno la ziada. Sijui kwa wale ambapo redio hii inasikika ni wangapi wamefaidika na fundisho hili.

Mtakatifu John Fischer wakati akielekea mnara la London mahali ambapo angenyongwa, alifungua Biblia katika Agano Jipya bila kuwa na sehemu rasmi ya kusoma huku akisali ‘Bwana, nioneshe neno la heri siku ya leo’. Alipofungua Biblia, macho yake yakaangukia katika Injili ya Yohane: na uzima wa milele ndio huu, wakujue wewe, Mungu pekee wa kweli, na wamjue Yesu Kristo uliyemtuma – Yoh. 17:3.’ Akamalizia akisema, hii ndiyo hekima kamilifu nikielekea mwisho wa maisha yangu hapa duniani.Ndugu zangu, tukifanya hivyo na kuishi hivyo mpaka mwisho tutakuwa tumetimiza mapenzi yake Mungu na kuwa manabii wake katika ulimwengu wetu wa leo.

Tumsifu Yesu Kristo.

01 February 2019, 14:27