Tafuta

Vatican News
Hekima ya Mungu imefumbatwa katika Fumbo la Msalaba! Hekima ya Mungu imefumbatwa katika Fumbo la Msalaba! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili VIII ya Mwaka: Hekima ya Mungu

Kristo Yesu ni nguvu, hekima na ufunuo wa Mwenyezi Mungu. Injili inakazia uongofu ili kuweza kuwasaidia wengine. Uadilifu mbele ya Mungu ni namna pekee ya kuishi kadiri ya hekima ya Mungu. Ni lazima hekima yetu ifuate hekima ya Kristo, kujenga mahusiano mema na Mungu, na watu tunaokaa nao, familia zetu, jumuiya zetu na hata mazingira yetu.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mwandishi wa hekaya za Esopo aliulizwa wakati fulani ni kitu gani/kipi muhimu zaidi ulimwenguni? Akajibu ni ulimi. Na akaulizwa tena ni kitu gani/kipi kiharibifu au hatari zaidi ulimwenguni? Akajibu ni ulimi. Naye mwanafalsafa Socrates anasema maumbile yametupatia masikio mawili na macho mawili lakini ulimi mmoja tu lengo likiwa ni kuona na kusikia zaidi kuliko kuongea.

Kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira au kwa Kilatini ‘Ecclesiasticus’ ni kitabu chenye kuwakilisha hekima ya Kiyahudi katika Israeli. Siraki au Sira, mwana wa Eleazari (50:27; 51:30) alikuwa mtu aliyesoma vizuri kutoka kwenye familia muhimu huko Yerusalemu kama miaka 40 kabla ya uvamizi wa utamaduni wa Kigiriki katika Palestina kati ya mwaka 220 na 116 KK (50:1-21). Hiyo changamoto ya hatari ya uvamizi wa utamaduni mpya ilimfanya mwandishi kufundisha kuwa hekima ya kweli imo katika Israeli iliyojengwa kuzunguka Torati. Kama ilivyo kwa waandishi wa kitabu cha Mithali na Mhubiri, Yoshua bin Sira anainoesha hekima kama ‘Sheria ya Musa’ ambayo wanadamu wanaiona na kuing’amua wenyewe binafsi kama kumwogopa Mungu.

Kitabu hiki kinatambua kuwa mwanadamu kaumbwa na Mungu kwa mpango maalumu na ni tofauti kabisa na viumbe vingine (16:24; 17:12) – wanadamu wana uwezo wa kuelewa na uwezo wa kufanya uchaguzi. Uhuru wa binadamu ni muhimu na sharti muhimu la msingi kwa uhusiano wa kweli na Mungu – 15:11. Kwa namna ya pekee, katika somo la kwanza twaona mwandishi akiongelea habari juu ya uwezo wa kufikiri na kusema – katika sura ya 26 na 27 ya kitabu hiki. Sira anaamini pia kwamba ufundi wa kusema na utoaji hoja bayana vinatambulisha tabia. Mwandishi anakazia habari juu ya uungwana na urafiki na mambo yanayoweza kuhatarisha mambo hayo.

Katika somo la pili, Mtume Paulo anakazia habari ya ufufuko wa mwili. Wakorinto walidharau habari hii na uwezekano huo. Walipinga fundisho hilo la Paulo. Paulo anaongea habari ya mwili – 1Kor. 12 … na sura yote ya 1Kor. 15… Paulo anasisitiza kwamba jinsi Kristo alivyofufuka katika mwili ni jinsi hiyo pia wale wamwaminio watafufuka siku ya mwisho. Kifo hakina nguvu kwa mfuasi wa Kristo. Mtume Paulo anaongea habari hii ya ufufuko akitumia msisitizo toka Agano la Kale – Isa. 25:8 – ataangamiza mauti milele na Hosea 13:14 …. Ee mauti, mapigo yako yapo wapi? Ee kuzimu, uharibifu wako uko wapi? Na baada ya hapa Mtume Paulo anaongelea nguvu ya upendo dhidi ya sheria na dhambi. Kadiri ya Paulo, hii ndiyo hekima ya kweli.

Injili ya leo inakamilisha fundisho tulilosikia tangu wiki mbili zilizopita – hotuba ya uwandani. Tulianza na heri na ole na wiki iliyopita tukaalikwa kuwapenda adui zetu. Wiki hii tunamsikia Yesu akiongea kuhusu uthabiti wa moyo. Yesu aliongea kwa mifano na lengo lilikuwa kuwasaidia wasikilizaji kuelewa fundisho hasa pale ambapo mmoja hakuwa na uelewa sahihi – Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu. Je, wote si watatumbukia shimoni? Katika Injili ya Mathayo maneno haya yanaelekezwa kwa Waandishi na Mafarisayo – 15:14. Mwinjili Luka anaelekeza fundisho kama hilo kwa wafuasi – walio vipofu mpaka waweze kung’amua – na tumeona hili katika hotuba kwa wiki mbili zilizopita. Baada ya kuelewa watawafundisha wengine. Mfano kama utaonaje kibanzi katika jicho la mwenzako na usione boriti katika jicho lako? Ni mwito wa kujitafakari.

Katika sehemu hii ya Injili tunaona Yesu mara baada ya kuwaita wafuasi wake. Yesu anafundisha kwa mifano mbele ya wafuasi wake ili wapate kuelewa na kuwa tayari kuwafundisha wengine baada ya kifo chake – Lk. 24:46-48. Injili inakazia uongofu ili kuweza kuwasaidia wengine. Uadilifu mbele ya Mungu ni namna pekee ya kuishi kadiri ya hekima ya Mungu. Ni lazima hekima yetu ifuate hekima ya Kristo, kujenga mahusiano mema na Mungu, na watu tunaokaa nao, familia zetu, jumuiya zetu na hata mazingira yetu. Tunaambiwa kuwa mtu hujielewa katika kutenda, kusema na kufikiri. Tunaambiwa kuwa watu wengi wana hamu ya kumjua Mungu. Watu wengi wana kiu ya kumjua Mungu wa kweli.

Hatuna budi kutambua kuwa tuna hazina zote za kimungu. Kila mti hutambulikana kwa matunda yake. Watu hawachumi figi toka katika miiba, wala kukusanya zabibu kutoka machakani. Mtu mwema toka ndani ya moyo wake huzaa matunda mema. Mwandishi wa Waraka wa Yakobo 3:1-18 anaongea kuhusu nguvu ya ulimi. Anaongea juu ya kazi ya ualimu na kwa kifupi anasema – kazi ya mwalimu ilikuwa ya muhimu na ya kuheshimiwa, hata hivyo ilikuwa katika hatari ya kutumiwa vibaya. Anaendelea akiongea kuhusu hekima ya kweli – nani kati yenu ana hekima na ufahamu? Basi aoneshe matendo yake yatokayo katika mwenendo mwema na kutendeka kwa upole na hekima – Yak. 3:13. Anamalizia sehemu hii akiongea kuhusu tunda la uadilifu, kwamba tunda la uadilifu huzalishwa na mpenda amani.

Je, hekima ya wakati wetu huu ni ipi? Bila shaka kwa sababu ya imani yetu, hekima ya kweli bado ni Kristo. Je sisi waamini tunaishi vyema hekima hii? Tunaifundishaje hekima hii, yaani Kristo, ili watu na ulimwengu upate majibu sahihi na kulinda watu wake kama alivyofanya mwandishi wa kitabu cha Hekima? Je tunakabilianaje na mila na desturi chonganishi zinazokinzana na imani yetu, mila na desturi zetu za wakati wetu huu? Tunatoa majibu gani? Je sisi waamini tunashuhudia na kufundisha nini katika ulimwengu huu geugeu?

Mtu mmoja anasema usihukumu mtu kwenye jukwaa alilosimamia mwingine bali hukumu kutoka jukwaa ulilosimamia, yaani toka mahali ulipo wewe unayetaka kutoa hukumu. Je, tunatambua vizuri kuwa jukwaa letu ni Kristo? Na ni kutoka katika jukwa hili tu twaweza toa hukumu? Kwamba hekima ya kweli ni Yesu Kristo Mwana wa Mungu? Tumsifu Yesu Kristo. 

26 February 2019, 14:21