Vatican News
Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019: Kenya: Vipaumbele: Imani na Upendo! Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019: Kenya: Vipaumbele: Imani na Upendo! 

Mpango Mkakati Mwezi Oktoba 2019: Kenya: Imani na Upendo!

Askofu Joseph Alessandro, Mwenyekiti wa Tume ya Kimisionari, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anakaza kusema, imani kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kushuhudiwa na kumwilishwa katika matendo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba 2019 unaongozwa na kauli mbiu “Mmebatizwa na kutumwa: Kanisa la Kristo katika utume”.  Kanisa linataka kuendeleza wito na utume wake wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, agizo kutoka kwa Kristo mwenyewe kwa wafuasi wake. Maadhimisho haya ni muda wa: sala, katekesi, tafakari na matendo ya huruma! Ni wakati kwa waamini walei kutambua haki, dhamana na wajibu wao katika maisha na utume kwa Kanisa. Hii ni fursa ya kuwahimiza waamini kujiwekea sera na mikakati ya kuyategemeza Makanisa mahalia: kwa njia ya rasilimali watu, vitu na fedha, ili Kanisa liendelee kutangaza Injili ya huruma na upendo hadi miisho ya dunia!

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kujikita zaidi katika utekelezaji wa mambo makuu manne: Mosi, waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Sala. Pili ni ushuhuda wa wamisionari watakatifu, wafiadini na waungama imani, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Tatu ni majiundo makini, endelevu na fungamani ya kimisionari kwa kujikita katika: Biblia, Katekesi, Tasaufi na Taalimungu. Nne ni huduma ya upendo kama kielelezo cha imani tendaji!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, maadhimisho ya Mpango Mkakati wa Mwezi Oktoba, 2019, ni chachu ya kuamsha ari, maisha na utume wa kimisionari nchini Kenya. Askofu Joseph Alessandro, Mwenyekiti wa Tume ya Kimisionari, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya anakaza kusema, imani kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kushuhudiwa na kumwilishwa katika matendo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huu ni wakati wa kuimarisha Katekesi ili kukazia mambo msingi katika imani; kuendelea kupyaisha Mafundisho Jamii ya Kanisa, Kanuni maadili na utu wema. Ushuhuda wa watakatifu, iwe ni chachu ya maboresho katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Kenya: Oktoba 2019
16 February 2019, 10:36