Tafuta

Vatican News
Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel ameteuliwa kuwa ni Rais wa Tume ya Haki na Upatanisho nchini Ethiopia Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel ameteuliwa kuwa ni Rais wa Tume ya Haki na Upatanisho nchini Ethiopia 

Kardinali Souraphiel: Tume ya Haki na Upatanisho Ethiopia!

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia, ameteuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Bwana Abiy Ahmed Ali kuwa Rais wa Tume ya Haki na Upatanisho nchini Ethiopia. Makamu wake ni Yetnebersh Nigussie, mwana harakati maarufu nchini Ethiopia. Lengo ni kuanzisha mchakato wa ujenzi wa umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huruma na msamaha ni utambulisho wa watoto wa Mungu na ushuhuda wa upendo. Msamaha una nguvu inayoleta uponyaji wa ndani katika maisha ya mwamini. Msamaha humweka mtu huru na kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano katika ukweli na matumaini! Kwa hakika familia ya Mungu nchini Ethiopia ina kiu ya haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wongofu wa kweli, haki, toba na upatanisho, umoja na mshikamano; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; haki msingi, utu na heshima ya binadamu ni kati ya mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa kuwainjilisha wanasiasa Barani Afrika, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho kati ya watu! Wanasiasa wawe mstari wa mbele kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kuheshimu, kuthamini na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kudumisha uongozi bora unaofumbatwa katika utawala wa sheria daima kwa kujikita katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa njia hii, hata wanasiasa wanaweza kuwa kweli ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia.

Hivi karibuni, Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia, ameteuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Bwana Abiy Ahmed Ali kuwa Rais wa Tume ya Haki na Upatanisho nchini Ethiopia. Makamu wake ni Yetnebersh Nigussie, mwana harakati maarufu nchini Ethiopia. Lengo ni kuanzisha mchakato wa ujenzi wa umoja, mshikamano na upatanisho wa kitaifa. Tume hii inaundwa na wajumbe 41 walioteuliwa hivi karibuni na Bunge la Ethiopia. Hawa ni watu wanaotoka katika medani mbali mbali za maisha. Ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko ni kati ya changamoto kubwa zilizokwamisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Ethiopia. Tume ya Haki na Upatanisho nchini Ethiopia pamoja na mambo mengine, inapaswa kujikita katika kupambanua changamoto za ulinzi na usalama; haki na amani; ili kurejesha tena tunu hizi msingi nchini Ethiopia.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao na Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, anaishauri Jumuiya ya Kimataifa ijikite katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu na wajenzi wa amani; kwa kukataa falsafa ya vita, kinzani na mipasuko na kuanza kujikita katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Ethiopia na Eritrea ni mfano bora wa kuigwa; jitihada hizi zinapaswa pia kuigwa na Sudan ya Kusini na kwamba, kuna matumaini huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ingawa bado vita imepamba moto!

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 21 Januari 2019, alikutana na kuzungumza na Bwana Abiy Ahmed Ali, Waziri Mkuu wa Ethiopia, ambaye baadaye alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu Msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili, wamekazia umuhimu wa uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo kati ya Vatican na Ethiopia. Baba Mtakatifu amepongeza juhudi zinazoendelea kutekelezwa na Serikali ya Bwana Abiy Ahmed Ali katika kukuza na kudumisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, ustawi na maendeleo fungamani ya watu wa Mungu nchini Ethiopia. Katika muktadha huu, viongozi hawa wamegusia pia mchango wa Ukristo katika historia ya Ethiopia pamoja na kuzipongeza taasisi za Kanisa Katoliki katika kuchangia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ethiopia hususan katika sekta ya elimu na afya.

Baba Mtakatifu na mgeni wake, katika mazungumzo yao, wamejikita pia katika hali ya ukanda wa Afrika na kwa namna ya pekee, umuhimu wa nchi za Kiafrika kutafuta suluhu ya amani katika vita, migogoro na kinzani zinaendelea kulimeng’enyua Bara la Afrika na kwamba, kipaumbele kwa sasa kiwe ni kwa ajili ya maendeleo endelevu na fungamani: kisiasa na kiuchumi Barani Afrika. Baba Mtakatifu ameipongeza Ethiopia katika jitihada zake za kuleta amani na upatanisho kwenye Nchi za Pembe ya Afrika, hasa baada ya Ethiopia na Eritrea kutiliana sahihi mkataba wa amani!

Ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Vatican imekuwa na umuhimu wa pekee sana, baada ya miaka ishirini ya vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha maafa na majanga makubwa kwa maisha ya watu na mali zao, tarehe 18 Septemba 2018, Ethiopia na Eritrea viliwekeana sahihi mkataba wa amani, tukio ambalo hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amelikumbuka kwa heshima kubwa, katika hotuba yake kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza watu wa Mungu nchini Ethiopia na Eritrea kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, kama cheche za matumaini mapya kwa Nchi za Pembe ya Afrika na Afrika katika ujumla wake.

Kunako mwaka 2014, wakati wa hija ya kitume ya Maaskofu wa Ethiopia na Eritrea, Baba Mtakatifu Francisko aliwahimiza kuwekeza katika miradi ya kijamii na kiuchumi ili kupambana na umaskini wa hali na kipato. Kwani eneo hili limekuwa linakumbukwa na ukame pamoja na baa la njaa, hali ambayo inanyanyasa na kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Injili ya huduma ya upendo, iwe ni faraja kwa familia ya Mungu katika eneo la Pembe ya Afrika. Ukosefu wa fursa za ajira, wimbi kubwa la watoto yatima waliowapoteza wazazi wao kutokana na vita, njaa na umaskini wamekuwa daima mbele ya macho ya Baba Mtakatifu Francisko anaikumbuka familia ya Mungu iliyoko kwenye Pembe ya Afrika.

Vita, umaskini na hali ngumu ya maisha ni kati ya changamoto zinazopelekea vijana wengi kuthubutu kuhatarisha maisha yao jangwani na kwenye Bahari ya Mediterrania, ili kutafuta, usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Lakini, kwa bahati mbaya, leo hii, Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la maisha na matumaini ya watu wengi kutoka Afrika! Katika mazingira kama haya, Kanisa nchini Ethiopia linapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Tume ya Haki: Ethiopia
16 February 2019, 14:31