Tafuta

Vatican News
Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania inaendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa Kanda ya kati nchini Tanzania. Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, Tanzania inaendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa Kanda ya kati nchini Tanzania. 

Hospitali ya Mt. Gaspar, Itigi: Matumaini ya watu Kanda ya Kati!

Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wakisukumwa na kauli mbiu ya Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya hapa Itigi 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini. Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma hii ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Mt. Gaspar na Mzee Ali Hassan Mwinyi tarehe 15 Mei 1989.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 27 ya Wagonjwa Duniani kwa mwaka 2019 anapenda kuhimiza roho ya ukarimu na sadaka ili kushinda kishawishi cha uchu wa kutaka kupata faida kubwa kwa hasara ya utu na heshima ya binadamu. Taasisi za afya zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki ziwe ni mfano bora wa huduma kwa wagonjwa, kwa kuongozwa na tunu msingi za Kiinjili. Ziwe ni chemchemi ya ukarimu, huruma na upendo badala ya kugeuzwa kuwa ni “kichaka” cha kuwanyonya wagonjwa. Kipaumbele cha kwanza ni utu, heshima na huduma kwa wagonjwa na wala si faida.

Baba Mtakatifu anawataka wadau katika sekta ya afya kutambua kwamba, hii ni huduma shirikishi inayohitaji kushirikiana, kuaminiana, kushikamana na hatimaye kujenga urafiki. Hii ni amana na utajiri mkubwa hasa pale sadaka inapotolewa kwa ajili ya wengine! Furaha ya kujitoa kwa ajili ya wengine ni kipimo thabiti cha afya ya Mkristo! Baba Mtakatifu anawakabidhi watu wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mfariji wa wagonjwa, ili awasaidie watu kushirikishana karama kwa moyo radhi, kwa kusikilizana na kupokeana jinsi walivyo; kwa kuishi na kushirikiana kama ndugu katika Kristo Yesu. Kwa njia hii, wataweza pia kutambua mahitaji ya jirani zao na hivyo kutoa kwa ukarimu na hivyo kuendelea kujifunza kujisadaka kwa ajili ya wengine!

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Jumamosi, tarehe 16 Februari 2019 amezindua mashine ya “CT Scan” na “Endoscopy” ambazo zimesaidia kupata uhakika wa uchunguzi na kugundua matatizo walionayo wagonjwa na hivi kuwarahisishia wagonjwa kutokwenda mbali kutafuta huduma hizi muhimu. Makamu wa Rais ametumia fursa hii kuwawashukuru na kuwapongeza Wamisionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu pamoja na wafanyakazi wa Gospitali ya Mtakatifu Gaspar kwa kazi kubwa wanaoifanya kwa ajili ya watanzania. Amewataka kutambua kwamba, hii ni taasisi ya kidini kumbe, wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, juhudi, maarifa, upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Watambue kwamba, mashine wanazotumia ni za gharama kubwa, kumbe, wanapaswa kuzitumia vizuri na kama kukitoea hitilafu, wawe wepesi kutoa taarifa, ili zifanyiwe marekebisho na huduma iendelee kutolewa! Makamu wa Rais amesema, amezisikia changamoto zinazowakabili na kukumbushia kwamba, hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania alikutana na kuzungumza na viongozi wa dini na kwamba, Serikali inaendelea kuyafanyia kazi maombi yao na baada ya muda wataweza kupata mrejesho, hasa kuhusu kodi. Serikali ya Tanzania inapenda kuitia shime Hospitali ya Mtakatifu Gaspar kusonga mbele kwa nia ya kuiwezesha kujikita kitaalam zaidi kwa magonjwa ya watoto ndani na nje ya Tanzania. Hili ni jambo jema, na Serikali itaipatia taasisi hii ushirikiano wa dhati kwa ajili ya huduma bora kwa watanzania na hasa maskini!

Ifuatayo ni taarifa fupi ya Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar: Mhe. Makamu wa Rais, awali ya yote tunayo furaha kubwa kukukaribisha wewe pamoja na msafara wako katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Manyoni, Singida, nchini Tanzania. Mhe. Makamu wa Rais, kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya Hospitali na Watumishi wote wa Hospitali na Chuo cha Uuguzi cha Mt. Gaspar, tunayo furaha kubwa kukupa taarifa fupi ya Taasisi yetu. Mhe. Makamu wa Rais, Taasisi yetu ipo katika sehemu kubwa mbili; moja ni Hospitali na sehemu ya pili ni Chuo cha Uuguzi. Taasisi hizi zipo chini ya kurugenzi moja inayosimamiwa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S.

HISTORIA FUPI YA HOSPITALI: Mhe. Makamu wa Rais, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu wakisukumwa na kauli mbiu ya Elimisha, Tibu na Fariji walianza rasmi kutoa huduma za afya hapa Itigi 15 Septemba 1987. Lengo kuu likiwa ni kutoa huduma kwa maskini. Nia hii njema ilizidi kukuwa na baada ya miaka miwili huduma hii ilipanuka na hivyo kufunguliwa rasmi kwa Hospitali ya Mt. Gaspar na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi tarehe 15 Mei 1989.

UKUBWA NA SHUGHULI ZA HOSPITALI: Mhe. Makamu wa Rais, katika kipindi hiki chote cha miaka 30 ya uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Mt. Gaspar, Hospitali imeendelea kupanuka na kukua katika shughuli zake na Mwezi Novemba Mwaka 2010 serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuipandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Rufaa ngazi ya mkoa.

 IDADI YA VITANDA: Mhe. Makamu wa Rais, Hospitali ina jumla ya vitanda 320. Katika wodi kuu nne ambazo ni:-Wodi ya magonjwa mchanganyiko (Medical ward), Wodi ya Upasuaji (Surgical ward), Wodi ya Uzazi na Magonjwa ya Kike (Obstetrics & Gynaecology), Wodi ya watoto chini ya miaka 12 (Paediatrics ward) na Wodi maalum na ya magonjwa ya mlipuko ((Privates & Isolation)

IDADI YA WATUMISHI: Mhe. Makamu wa Rais, kwa hivi sasa Hospitali ina jumla ya watumishi 297 kati yao 50 tu wanalipwa ruzuku na Serikali. Hospitali inayo madaktari bingwa 5 kutoka fani zifuatazo: Upasuaji madaktari bingwa wawili, Watoto daktari bingwa mmoja, Magonjwa ya Kike na uzazi madaktari bingwa wawili. Aidha tunao madaktari 8 wa shahada ya kwanza (MDs) na madaktari wasaidizi 4 (AMO) kati yao mmoja ni AMO Radiologist, na mwingine ni AMO Ophthalmologist. Tunao Clinical Officers 4 mmoja kati yao akiwa Dental Therapist. Madaktari hawa wanafanya kazi zao wakishirikiana na Lab. Scientist 2, Lab Technologist 9, Lab Technician 2, Pharmacist 1, Pharmaceutical Technician 2, Radiographer 3 na Physiotherapist 1. Aidha tunao wauguzi 75 na Bio Medical Technician 2. Wahudumu wengine ni 182.

IDADI YA WAGONJWA NA SEHEMU WATOKAKO: Mhe. Makamu wa Rais, Mwaka 2018 tuliwahudumia wagonjwa wa nje 31,450 na Wagonjwa wa ndani 6,110. Wagonjwa tunaowahudumia ni kutoka katika mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro, Mbeya, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora, Kigoma na Rukwa. Tangu tuanze kutoa huduma ya afya hapa Itigi tumekuwa tukipeleka vijijini huduma za kliniki tembezi (RCH). Huduma hii ya RCH tunaitoa katika vijiji vya Kitaraka, Kazikazi na Doroto tulivyopewa kwa ushirikiano na Halmashauri yetu ya Itigi. Katika kliniki tembezi kwa mwaka 2018 tuliwahudumia akina mama wajawazito zaidi 700 na kuwapatia chanjo zaidi ya watoto 4,500

HUDUMA TUNAZOTOA: Mhe. Makamu wa Rais, pamoja na huduma za kibingwa tunazotoa, huduma hizi zinaweza kutolewa tu kwa sababu tunavyo vipimo vya kisasa, kama:CT Scan, Endoscopy, Digital X-Ray, ECG,  Ultra sound na Ecocardiogram. Aidha hivi karibuni tumetatua changamoto iliyokuwa inatukabili kwa muda mrefu ya chumba cha maiti ambapo tumeweka majokofu yenye uwezo wa kuhifadhi miili sita kwa wakati mmoja.

Mhe. Makamu wa Rais, ili kuweza kubaini kwa undani matatizo ya wagonjwa katika Maabara yetu tunavyo vipimo vyote vya kisasa, kama vile Hormones, Electrolytes, Gene Expert na Blood Culture. Hivi karibuni tumenunua Centrifugal Mashine ya kutenganisha damu na plasma. Aidha ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa zitumikazo kwa njia ya mishipa (Drips) Hospitali inazalisha maji haya yenyewe. Taasisi ipo katika mpango wa kuhakikisha inazalisha maji hayo kwa kiwango kikubwa ili kutoa huduma hiyo kwa wengine na kuunga mkono Serikali yetu katika sera ya viwanda haswa vya dawa.

VIFAA TIBA UNAVYO VIZINDUA; Bodi ya Wakurugenzi iliona hitaji la wagonjwa haswa wa pembezoni la kupatiwa huduma za kiwango cha juu na zenye ubora. Hivyo bodi ya wakurugenzi iliamua kununua mashine ya CT Scan na Endoscopy ambazo utazifungua leo. Vifaa tiba hivi vimesaidia kupata uhakika wa uchunguzi na kugundua matatizo walionayo wagonjwa na hivi kuwarahisishia wagonjwa kutokwenda mbali kutafuta huduma hizi muhimu.

 Hivyo kwa kauli moja bodi ya wakurugenzi mwaka 2015 iliamua kununua mashine ya kisasa ya CT-Scan yenye ukubwa wa slide 64 yenye thamani ya Tshs, 1.5 bilioni (Dolla 700,000) na UPS inayoilinda mashine hii yenye thamani ya Tshs.99 millioni. ( dolla 45,000.00). Fedha hizi zote zilitolewa na Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu.

Aidha hitaji la vipimo vya kisasa kwa wagonjwa wetu lilizidi kukua na hii ilipelekea kuona umuhimu wa kununua mashine ya kiwango cha juu cha utafiti wa magonjwa ndani ya mfumo wa chakula (Endoscopy) mwaka 2018 yenye thamani ya Tshs. 338, 800, 000. 00. (Dolla 154,000). Hivyo vifaa tiba unavyovizindua leo vina thamani ya karibu ya Tshs, Bilioni mbili. Tunawashukuru sana Shirika la Wamisionari wa Damu Takatifu ya Yesu na wale wote waliosaidia kuhakikisha vifaa tiba hivi vinapatikana. 

SHUKRANI: Mhe. Makamu wa Rais, kwa niaba ya wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu na watumishi wenzangu tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia ili kuweza kuifanya Taasisi hii kuonekana hivi ilivyo. Ni ukweli usiopingika kuwa bila msaada wa serikali tusingeweza kufanya hayo tunayoyafanya. Nitaje machache kati ya mengi: Ruzuku kwa watumishi: Kwa mwaka 2018 Serikali imeweza kutupatia zaidi ya Tshs. Milioni 450 kama ruzuku kwa watumishi.  

Dawa na vifaa tiba: Kwa mwaka 2018 Serikali imetupatia dawa na vifaa tiba kutoka Stoo ya dawa (MSD) vyenye thamani ya zaidi ya Tshs. Milioni 80. Aidha imetupatia mashine ya GeneXpert ambayo imetusaidia kuwatambua wagonjwa wa TB. Vibali kwa madaktari toka nje ya nchi: Kwa ushirikiano mkubwa tumeweza kupatiwa vibali kwa madaktari wa kutoka nje ya nchi wanaopenda kuja kushirikiana nasi katika kutoa huduma za kibingwa. Zaidi ya hayo yote mazingira rafiki na ya utulivu ya kufanyia kazi tunayopewa na serikali ya mkoa, wilaya na Halmashauri yetu ya Itigi yote haya yanatufanya tuseme asante sana kwa Serikali yetu. Mungu awabariki.

MATARAJIO: Ushirikiano tulionao na serikali utaendelezwa na kuzidi kukua ili kuhakikisha huduma bora za afya zinawafikia hata wale wasiokuwa na kipato kikubwa. Tunania ya kutoa huduma zote za kibingwa kwa watoto (Super Specialized Services) kwa kuwa tunayo makubaliano na Hospitali ya Baba Mtakatifu ambayo ipo Roma – Italia “Bambino Gesù” ambayo ni hospitali maalumu kwa watoto tu. Tumekubaliana nao kutusaidia kutoa mafunzo na kubadilishana ujuzi na utaalamu. Ni nia yetu tutambulike hapa Tanzania na hata Afrika mashariki kuwa mabingwa kwa huduma ya watoto.

CHANGAMOTO: Mhe. Makamu wa Rais, kwenye mafanikio hapakosi changamoto ambazo sisi tunazichukua kama fursa: Ruzuku ya Serikali: Tunaomba ruzuku ya serikali iongezwe ili tuweze kutoa huduma kwa gharama ndogo zaidi. Aidha baadhi ya watumishi wanaolipwa ruzuku ya Serikali bado hawalipwi katika ngazi stahiki na hii inapelekea hospitali kujaziliza katika mishahara ya watumishi hawa. Kuondolewa kodi ya SDL. Pamoja na kupewa ruzuku na serikali bado serikali inaidai taasisi yetu kulipa kodi ya SDL Jambo hili linaonyesha kuwa sisi tunaendesha hospitali kwa faida. Hii tunaona kuwa ni dhana kinzani na dhana ya serikali kutupatia ruzuku.

Tunatanguliza shukrani za dhati iwapo kodi hii itaondolewa kwa hospitali yetu. Aidha tunaomba ikiwezekana tusamehewe deni la SDL la kiasi cha Tshs. Milioni 333, 389, 925. 00 tunalodaiwa na TRA. Tunatambua kuwa deni hili lipo kisheria lakini kama tukililipa huduma zetu zitaathirika kwa kiwango kikubwa na zaidi wananchi wanaokuja kupata huduma kwetu watakuwa waathirika wa kwanza. Uhaba wa watumishi: tunao bado uhaba mkubwa wa madaktari bingwa wa Idara mbalimbali nikizitaja chache ENT, Orthopaedics, Internal Medicine, Emergency na Radiology. Dawa na Vifaa tiba: Bado kuna tatizo la upatikanaji wa baadhi ya dawa na vifaa tiba.

Huduma ya Idara ya dharura (Emergency Department). Bado hatujawa na Idara ya Dharura inayolingana na hadhi ya Hospitali. Ni hitaji lisilo na mbadala kwa sasa kutokana na miundo mbinu ya barabara ilivyoboreshwa na ongezeko la huduma za pikipiki (boda boda). Bila kusahau ongezeko la watu katika mikoa jirani hususani Dodoma. Mhe. Makamu wa Rais, Mwisho tunakushukuru sana kwa kufika kwetu na tunakukaribisha tena na tena. Tunawaombea safari njema na majukumu mema.

Naomba Kuwasilisha.

Hospitali ya Mt. Gaspar
16 February 2019, 16:04