Kanisa nchini Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa sasa! Kanisa nchini Tanzania limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza kwa sasa! 

Mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu nchini Tanzania

Hivi sasa kila kijiji nchini Tanzania kina shule ya msingi na ongezeko limefikia idadi ya shule za msingi 17,659 zikiwemo zilizo chini ya Kanisa Katoliki 204. Pia, kuna shule za sekondari katika kila kata, ambazo zipo 4,883 nchi nzima zikiwemo 266 zilizo chini ya Kanisa Katoliki. Idadi hiyo ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu katika ngazi mbalimbali nchini Tanzania!

Na Mwandishi maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Moshi, Kilimanjaro

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema taasisi binafsi na mashirika ya dini yaendelee kuangalia namna ya kupanga gharama za huduma wanazotoa zikiwemo za elimu na afya ili ziwiane na hali halisi ya vipato vya wananchi. “Hivi sasa, Serikali kupitia vyombo mbalimbali inachukua hatua za makusudi za udhibiti ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma zenye viwango, ambapo baadhi ya wadau na wamiliki wanailalamikia Serikali kuwa inawakandamiza na kuwawekea masharti magumu.”

Ameyasema hayo Februari 22, 2019, wakati akizindua shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro. Amezindua shule hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli. Waziri Mkuu amesema lengo la udhibiti huo ni kuimarisha viwango na ubora wa elimu inayotolewa, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali. Amesema utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA). Pia, Waziri Mkuu amesema ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.

Akizungumzia kuhusu mafanikio ya sekta ya elimu, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imepata mafanikio makubwa sana katika upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya na maji.  ”Hivi sasa kila kijiji nchini kina shule ya msingi na ongezeko limefikia idadi ya shule za msingi 17,659 zikiwemo zilizo chini ya Kanisa Katoliki 204. Pia, tumejenga shule za sekondari katika kila kata, ambazo zipo 4,883 nchi nzima zikiwemo 266 zilizo chini ya Kanisa Katoliki.”  Amesema idadi hiyo ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata elimu katika ngazi mbalimbali nchini na kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi wanatekeleza mpango wa elimu msingi bila ada.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Serikali inatoa kiasi cha shilingi bilioni 24.4 kila mwezi kwa ajili ya kugharimia mpango wa elimu msingi bila ada, kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata fursa bila vikwazo.  Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeongeza idadi ya wanufaika na Elimu ya Juu kwa kuongeza bajeti ya fedha za mikopo kwa wanafunzi, ambapo kwa sasa inatoa zaidi ya shilingi bilioni 483 kwa mwaka. ”Kwa upande wa afya tunaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa kujenga zahanati katika kila kijiji, kuimarisha vituo vya afya na ujenzi wa Hospitali 67 katika Halmashauri na Hospitali 4 za Rufaa kwenye Mikoa ambayo haikuwa na Hospitali za Rufaa. Upatakinaji wa dawa umeimarika kwa zaidi ya asilimia 90.”  Waziri Mkuu amesema licha ya mikakati waliyonayo na namafanikio wanayoyapata, Serikali inathamini sana mchango wa sekta binafsi na taasisi za dini katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kutowaficha ndani watoto wenye mahitaji maalumu na badala yake wawapeleke shule kwa kuwa nao wanahaki ya kupata elimu kama watoto wengine.  ”Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri hakikisheni watoto wote wenye mahitaji maalumu kwenye maeneo yenu wanapelekwa shule na wachukulieni hatua wote watakaobainika wamewaficha watoto hao.” Akiwa shuleni hapo Waziri Mkuu ameshuhudia mmoja wa wanafunzi wa kidato cha kwanza, Joseph Joachim  ambaye hana mikono akiandika kwa kutumia vidole vya miguu. ”Mwanafunzi huyu anandika muandiko mzuri kupita hata wanaotumia mikono haya ni maajabu ya Mwenyezi Mungu.”

Awali, Mkuu wa shule hiyo Padri Patrick Asanterabi alisema ujenzi wa shule hiyo hadi hivi sasa umepita katika awamu saba tangu kazi ya ujenzi ilipoanza rasmi mwaka 2015. Kwa sasa shule inawanafunzi 74 huku lengo ni kufikisha ni wanafunzi 500 itakapokamilika. Alisema ujenzi huo ulianza kwa tukio la kubariki kazi kwa ‘kupiga jembe la kwanza’ lililofanywa na Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, wakati huo akiwa Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi.  “Kuanzia hapo, miundombinu mbalimbali ilijengwa ikiwemo, madarasa, vyoo, mabweni, ukumbi wa shule, jengo la utawala, nyumba ya masista, jiko na uwekaji wa mifumo ya umeme na maji.”  Alisema shule imedhamiria kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na wengine, ili kuhakikisha wanakuwa na ulewa mzuri utakaowawezesha kupata matokeo mazuri na kuendelea na masomo pamoja na kujitegemea.

Kwa upande wake, Askofu Isaac Amani wa Jimbo kuu la Arusha ambaye ndie muasisi wa shule hiyo alisema alipata wazo hilo baada ya mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa anasoma shule ya Mtakatifu Francis kumtembelea. Alisema mwafunzi huyo ambaye ni mlemavu wa macho alikuwa akisoma shule ya msingi alimuuliza kuwa baada ya kumaliza watakwenda wapi kuendelea na masomo kwani alisikia wenzao wanapangiwa shule ambazo miundombinu yake si rafiki kwao ndipo akapata wazo la kuanzisha ujenzi wa shule hiyo.

25 February 2019, 12:20