Tafuta

Askofu Filbert Felician Mhasi, akiwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania Askofu Filbert Felician Mhasi, akiwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania 

Askofu Filbert Felician Mhasi: Tunduru-Masasi, Kumenoga

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na muasisi wa Jimbo la Tunduru-Masasi, alimtaka Askofu Filbert Felician Mhasi kuwa “Myao-Mkatoliki”, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa kutambua kwamba, Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi lina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu anao wajibu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kwani kimsingi, yeye ni mwalimu, kuhani na mchungaji. Askofu ni mtumishi wa Kristo na mgawaji wa Mafumbo ya Mungu kwa watu wake, kwani amekabidhiwa ushuhuda wa Injili ya ukweli na huduma ya Roho Mtakatifu na ya haki. Uaskofu ni huduma, kumbe, Askofu anapaswa kuhubiri Neno wakati ufaao na wakati usiofaa, anapaswa kuonya kwa uvumilivu na mafundisho yote. Katika Kanisa Katoliki linalokusanyika kwa kifungo cha upendo, Askofu anaunganishwa katika urika kwa Maaskofu.

Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na muasisi wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Jumapili tarehe 17 Februari 2019 amemweka wakfu na kumsimika Askofu Filbert Felician Mhasi kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi. Pamoja na wosia wa Kiaskofu kadiri Ibada ya kuwekwa wakfu kwa Askofu mpya, Kardinali Pengo alimtaka Askofu Filbert Felician Mhasi kuwa “Myao-Mkatoliki”, ili kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam kwa kutambua kwamba, Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi lina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam.

Kumbe, tofauti zao za kidini na kiimani ziwe ni utajiri na amana kubwa kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu, Kusini mwa Tanzania! Kardinali Pengo amewaalika Maaskofu Katoliki Tanzania kumpokea na kumkaribisha Askofu Filbert Felician Mhasi katika urika wao pamoja na kuhakikisha kwamba, wanampatia ushirikiano mwema, ili aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara! Askofu Mhasi atoe kipambele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kumwongoza katika mapito yake!

Kwa upande wake, Askofu Filbert Felician Mhasi katika hotuba yake ya shukrani, kwa Mwenyezi Mungu, viongozi na makundi mbali mbali, amesema kwamba, ataendelea kujenga na kudumisha umoja, ushirikiano na mafungamano ya kijamii katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Anapenda kuwa mstari wa mbele katika kulinda: haki msingi za binadamu, utu na heshima yao; ataendelea kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, ili Tanzania iendelee kuwa ni kisiwa cha haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kwamba, watanzania waendelee kuwa kweli ni wacha Mungu. Yuko tayari kushikamana na familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ameitaka Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Tunduru Masasi kuishi na kufanya kazi kwa pamoja kama familia ya Mungu inayowajibikiana; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa dhati; kwa kila mwanafamilia kutekeleza dhamana na wajibu wake, ili kuweza kumrahisishia Askofu Jimbo dhamana na utume wake. Hii ndiyo dhamana na wajibu unaopaswa kutekelezwa na familia ya Mungu nchini Tanzania katika ujumla wake!

Wakati huo huo, Askofu Mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo Katoliki Songea katika mahubiri yake kwenye Masifu ya Jioni, tarehe 16 Februari 2019, alijikita zaidi katika “dhana ya Kristo Mchungaji mwema” sehemu ya Injili ya Yoh. 10:1-20. Askofu mkuu Dallu ameitaka familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Tunduru- Masasi kumkubali na kumpokea, ili aweze kuwaonesha malisho mazuri. Amekemea tabia inayoendelea kujitokeza kwa wakulima na wafugaji kusigana na matokeo yake ni maafa kwa watu na mali zao.

Amekazia pia dhana ya umisionari katika maisha na utume wa Kanisa, kwamba, waamini wanaitwa na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa miaka mingi, Kanisa la Tanzania linajivunia umisionari wake. Hii ni changamoto ya kuondokana na dhana potofu kuhusu umisionari, kwa kukazia nidhamu, uwajibikaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Rais John Pombe Magufuli katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, amewaomba viongozi wa dini kuendelea kumwombea yeye pamoja na viongozi wote wa Serikali ya awamu ya tano, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa watanzania. Amepanga kila mwanzo wa mwaka kukutana na kuzungumza na viongozi wa dini ili kushauriana. Serikali ya Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika huduma ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii.

Sherehe hii pia imehudhuriwa na Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa, ambaye Tunduru-Masasi “ni maeneo yake ya kujidai” ameona na kushuhudia maisha na utume wa Kanisa kusini mwa Tanzania na bado anaendelea kushuhudia matendo makuu ya Mungu kwa familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi!

Askofu Flavian Matindi Kassala, Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika mahojiano maalum na Vatican News anakiri kwamba, kumekuwepo na mapokezi makubwa kwa msafara wa viongozi na waamini waliokwenda kushiriki katika Ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Askofu Filbert Felician Mhasi wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi. Sasa ni wakati wa kuendeleza furaha hii kama sehemu ya ushuhuda wa furaha ya Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Askofu Flavian Matindi Kassala, amewapongeza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka Tunduru-Masasi waliohudhuria, ikikumbukwa kwamba, hili ni eneo ambalo lina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam, lakini wanaishi kwa umoja na upendo; kwa kuthaminiana na kuheshimiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi! Kanisa kwa upande wake, litaendelea kujipambanua katika huduma kwa watu wote wa Mungu bila ubaguzi, kwani huu ndio utume na umisionari wake!

Askofu Filbert Mhasi
20 February 2019, 13:55