AMECEA inataka kushiriki kikamilifu katika mkutano wa Kanisa Kuwalinda Watoto Dhidi ya Nyanyaso ili kujiwekea mbinu mkakati! AMECEA inataka kushiriki kikamilifu katika mkutano wa Kanisa Kuwalinda Watoto Dhidi ya Nyanyaso ili kujiwekea mbinu mkakati! 

AMECEA: Kushiriki kikamilifu mkutano wa Kanisa kulinda watoto!

Nyanyaso dhidi ya watoto wadogo Barani Afrika: Ni watoto kupelekwa mstari wa mbele vitani kama chambo; kufanyishwa kazi za suluba kwenye mashamba makubwa na migodi ya madini; ndoa za shuruti; utumwa wa watoto majumbani na vipigo! Hawa ni watoto wanaonyanyasika utu wao kutokana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, bila kusahau ukeketaji kwa watoto wa kike.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 mjini Vatican ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Siku ya kwanza wajumbe watafanya tafakari ya kina kuhusu wajibu wa Askofu mahalia: kichungaji na kisheria.

Siku ya Pili: Je, Askofu mahalia anawajibika kwa na nani?: hapa ni mahali pa kuangalia mfumo mzima, taratibu na kanuni katika mchakato mzima wa utekelezaji wake. Hapa umuhimu wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa unapaswa kuzingatiwa. Siku ya tatu, viongozi wa Kanisa watajikita katika dhana ya ukweli na uwazi ndani ya Kanisa, Serikali na kwa watu wa Mungu katika ujumla wao! Changamoto kubwa hapa ni mchakato wa Kanisa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kubadili mwelekeo na mtazamo kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, hivi karibuni limehitimisha kikao cha wajumbe wanaoshiriki katika mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo mjini Vatican. Askofu mkuu Thomas Luke Msusa, SMM, Makamu Mwenyekiti wa AMECEA anasema, AMECEA iko tayari kusikiliza kwa makini yale yote yatakayojiri, ili kuchukua hatua madhubuti zikazosaidia kuimarisha ulinzi kwa watoto katika mazingira ya Kanisa. Hata Barani Afrika, kuna nyanyaso dhidi ya watoto wadogo; nyanyaso ambazo zinavuka kiwango cha ngono na kutikisa zaidi ustawi na maendeleo ya watoto hawa!

Nyanyaso dhidi ya watoto wadogo Barani Afrika zinaonekana kwa watoto: kupelekwa mstari wa mbele vitani kama chambo; watoto kufanyishwa kazi za suluba kwenye mashamba makubwa na migodi ya madini; ndoa za shuruti; utumwa wa watoto majumbani pamoja na vipigo! Hawa ni watoto wanaonyanyasika utu na heshima yao kutokana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake, bila kusahau ukeketaji kwa watoto wa kike. Hizi ndizo changamoto za nyanyaso za kijinsia katika ujumla wake, Barani Afrika. Umefika wakati kwa AMECEA kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso mbali mbali wanazokabiliana nazo katika maisha yao.

Ni katika muktadha huu, umaskini, ujinga na maradhi vinaingia pia kwani waathirika wakuu ni watoto, ambao kimsingi ni tumaini la Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mustakabali na hatima ya watoto hawa inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; kwa kuwaundia mazingira bora ya malezi na makuzi; ustawi na maendeleo yao: kiroho na kimwili; kwa kulinda utu na heshima yao sanjari na kuzingatia haki zao msingi. Nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kashfa inayopaswa kupewa uzito wa juu zaidi, ingawa Barani Afrika changamoto hii inapaswa kuangaliwa kwa kina na mapana, ili kupambana na changamoto mamboleo.

Watoto yatima, watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, yote haya ni mambo yanayoathiri ustawi na maendeleo ya watoto: kiroho na kimwili. Haya yote ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika sera na mbinu mkakati wa kulinda na kuwaendeleza watoto wadogo. Kwa upande wake, Padre Anthony Makunde, Katibu Mkuu wa AMECEA, anasema, kikao hiki kimewapatia fursa Maaskofu kutoka AMECEA kutafakari kwa pamoja changamoto ya ulinzi wa Kanisa kwa watoto wadogo pamoja na kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika Nchi za AMECEA. Maaskofu wamebainisha maeneo tete yanayopaswa kuvaliwa njuga. Kikao hiki kiliandaliwa na Idara ya Shughuli za Kichungaji, AMECEA. Nyanyaso dhidi ya watoto wadogo zimepangwa kama ifuatavyo: Nyanyaso za kijinsia; Nyanyaso kimwili; Nyanyaso za kihisia: Nyanyaso kwa kutotimiza wajibu pamoja na unyonyaji.

AMECEA: Ulinzi wa watoto
16 February 2019, 14:03