Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeunda kikosi kazi kushughulikia ndoa zenye utata! Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeunda kikosi kazi kushughulikia ndoa zenye utata! 

Maaskofu nchini Italia waunda kikosi kazi kushughulia ndoa tata!

Umoja wa Maaskofu Kanda ya Emilia Romagna-Italia, umeandaa kikosi kazi kwa ajili ya kuwasindikiza, kung’amua na kuwahusisha waamini wanaohitaji, ikiwa ni pamoja na wachumba wanaotarajia kufunga ndoa. Kikosi kazi kimepewa dhamana ya kuwaangalia wanandoa wenye changamoto na walioko hatarini kutengana; wanandoa waliokwishakutengana au kuachana kabisa.

Na Padre Celestine Nyanda, - Vatican.

Katika kutekeleza Wosia wa kitume Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya Familia, Umoja wa maaskofu wa kanda ya Emilia Romagna, nchini Italia, hivi karibuni wametoa mwongozo ili kuwasindikiza, kung’amua na kuwahusisha waamini wanaojikuta kwenye changamoto za ndoa na familia zao. Maaskofu hawa wanatoa pongezi na kuonesha ukaribu wao kwa wale ambao wanajisikia kuitwa katika wito wa ndoa na wanajiandaa kuadhimisha Sakramenti hiyo takatifu; na kwa familia wanaoishi sakramenti ya ndoa kwa imani na uaminifu. Kwa upande mwingine, wanadhihirisha masikitiko yao na wanaonesha ukaribu wao kwa wale wote wanaoishi katika hali ngumu na changamoto za kiuchumi, kupoteza kazi, mahangaiko ya afya na vilema, kupoteza wapendwa wao kwa kifo, na wanaosumbuka na madonda na maumivu ya kutengana ama kuachana kabisa, au waliomo kwenye hali tete na dhaifu ya mahusiano.

Maaskofu wa majimbo ya Emilia Romagna wanapenda kusisitiza tena juu ya uzuri na neema za matunda ya utakatifu zinazobubujika kutoka katika Sakramenti ya ndoa. Kanisa katika Wosia wa Kitume Amoris laetitia, yaani Furaha ya Upendo ndani ya Familia, katika nyaraka na maelekezo yote kuhusu ndoa na familia, halina lengo la kurahisisha mambo au kufundisha kinyume cha mapenzi ya Mungu eti kwa sababu tu ya kuwapendezesha watu. Kanisa haliongozi, halifundishi wala kutakatifuza kwa kufuata mitindo ya kisasa, kana kwamba linashindana kwa fashion; bali linaendeleza dhamana na utume lilivyokabidhiwa na Kristo katika misingi ya kweli kadiri ya mazingira ya nyakati na nafasi katika historia ya mwanadamu, ili roho za waamini zipate wokovu unaokusudiwa na Kristo mwenyewe.

Umoja wa Maaskofu Kanda ya Emilia Romagna-Italia, umeandaa kikosi kazi kwa ajili ya kuwasindikiza, kung’amua na kuwahusisha waamini wanaohitaji, ikiwa ni pamoja na wachumba wanaotarajia kufunga ndoa. Kikosi kazi kimepewa dhamana ya kuwaangalia wanandoa wenye changamoto na walioko hatarini kutengana; wanandoa waliokwishakutengana au kuachana kabisa, wanaoishi na wenza wengine kwa ndoa ya kiserikali ama kuishi bila ndoa, waliotelekeza watoto, na walio kwenye mahusiano ya watoto wa wazazi mseto.

Hizi ni kati ya changamoto zinazokabili ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Kikosi kazi hicho kinajumuisha mapadri, watawa wa kike na wa kiume, waamini walei, na wanandoa. Malengo ambatanishi ya kikosi kazi hiki, ni pamoja na juhudi za kuokoa ndoa ili wasitengane, uwajibikaji katika familia na malezi ya watoto kwa wale waliotengana, uhakika wa dhamiri ya kwamba ndoa ilikuwa batili ama la, uwezekano wa upatanisho, kuponya ndoa na kurudisha mahusiano ya wanandoa waliotengana, na kuzingatia hali ya aliyetelekezwa.

Kwa upande mwingine, kikosi kazi hiki kinalenga kusaidia kutazama: hali ya mahusiano ya pili kwa mwenza mwingine baada ya kutengana na mwenza wa ndoa ya awali; kuangalia hali, usalama na malezi bora ya watoto; ubora wa mahusiano ya hawa wazazi wa muungano wa pili. Ni kikosi ambacho kinapasa kuchunguza hali ya kujisadaka katika familia na bidii ya kuishi maisha ya kikristo; ufahamu ya kwamba wanaishi kinyume na taratibu za Kanisa; uwezekano ama la, wa kurudi nyuma katika ndoa ya awali bila kuanguka katika makosa na hatari zingine; na athari za mahusiano haya ya pili kwa familia na jumuiya nzima ya kikristo, kwa namna ya pekee athari kwa vijana wanaojiandaa kuingia katika wito wa ndoa.

Maaskofu wa kanda ya Emilia Romagna-Italia wanasisitiza kwamba, lengo la awali, sio kuruhusu watu kuungama na kukominika kinyume cha taratibu, bali ni kuwasindikiza katika hija ya maisha ili kuboresha maisha yao kiroho, kimwili na kijamii. Ifahamike pia kwamba, sio rahisi kutoa jibu la jumla kwa uhalisia mpana na mgumu kiasi hiki, kwa changamoto za ndoa na familia kwa dunia ya leo. Kumbe hilo haliondoi ukweli kwamba wapo watakaoweza kurudi kushiriki sakramenti za Upatanisho na Ekaristi Takatifu, iwapo wataendana na taratibu zilizowekwa na kadiri ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa juu ya sakramenti za Ndoa, Upatanisho na Ekaristi Takatifu.

Kumbe, hija hii ya wanandoa isijeikaeleweka kana kwamba ni kozi ya muda fulani, la hasha! Itambulike kuwa ni hija ya maisha kwa wanandoa husika na kwa malengo yanayoendana na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu vinamualika mwamini kuongoka kutoka undani wa moyo wake, lakini pia ni Mungu mwenye utaratibu kiasi kwamba kila tukio linaendana na matokeo yake yanayopaswa kuheshimiwa ili kuepuka kujipoteza zaidi binafsi, kuumiza na kukwaza wengine. Kufuatana na hayo, hija ya wanandoa wenye changamoto za maisha, iwaelekeze kufahamu zawadi na thamani ya mwili na jinsia.

Waamini watambue umuhimu wa ndoa na familia; maisha ya useja na kujikatalia; nafasi na uwajibikaji wa wazazi; urafiki na udugu wa kweli kwa wenye mahusiano kati ya mwanamke na mwanamume. Waamini wajifunze kuhudumia wagonjwa, wafungwa, yatima pamoja na kuonesha ukarimu kwa wahitaji. Waendelee kujikita katika malezi ya watoto na vijana katika jumuiya ya wakristo mfano kwenye michezo, sanaa kama vile nyimbo, muziki, ngojera, na maagizo; huku wao wenyewe wakijikita zaidi katika maisha ya sala, ibada na uchaji kwa Mungu.

Italia: Ndoa na familia
30 January 2019, 17:33