Muujiza wa harusi ya Kana ni mwendelezo wa ufunuo wa utukufu wa Kristo Yesu, utakaofikia kilele chake pale Msalabani! Muujiza wa harusi ya Kana ni mwendelezo wa ufunuo wa utukufu wa Kristo Yesu, utakaofikia kilele chake pale Msalabani! 

Tafakari: Jumapili II Mwaka C: Muujiza wa Harusi ya Kana!

Muujiza wa Kana ya Galilaya unautajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kwani unaashilia: Sakramenti ya Ubatizo, Karamu ya Bwana, inayojulikana pia kama Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Ndoa, pengine inayobeba uzito wa juu katika tafakari ya leo, kwa kuonesha kwa kina nafasi ya Bikira Maria katika maisha ya waamini. "Hawana Divai" .

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Doodoma.

Wapendwa taifa la Mungu, baada ya adhimisho la Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, ambapo sisi tumetumwa kushuhudia utukufu wa Mungu na kushiriki katika ujenzi wa huo ufalme, leo tunaona kuwa ili hayo yaonekane au yapate kutendeka hatuna budi kuwajali wengine. Katika Injili ya leo Bwana wetu Yesu Kristo amelidhihirisha hili katika harusi ya Kana. Tabia na sifa ya Mungu ni kutujali sisi wanae na katika tendo hilo muujiza unatokea.

Mnapotindikiwa na divai ya furaha, upendo, uaminifu na udumifu katika maisha yenu ya ndoa na familia, jitahidini kumkaribisha Bikira Maria, ili awapelekee sala zenu kwa Kristo Yesu anaendelea kujifunua kwa njia ya muujiza wa Harusi ya Kana ya Galilaya! Ni ufunuo kama ule uliofanywa kwa Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali na siku ile mbingu na dunia zilipofunguka wakati wa ubatizo wake kwenye mto Yordani, maji yote yakatakaswa, tayari kuwafanya watoto wa Mungu wazaliwe upya kwa: Neno, Maji na Roho Mtakatifu. Matunda ya ufunuo wa Yesu kwenye harusi ya Kana ya Galilaya ni kwamba, wafuasi wake waliweza kumwamini.

Muujiza wa Kana ya Galilaya unautajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kwani unaashilia: Sakramenti ya Ubatizo, Karamu ya Bwana, inayojulikana pia kama Fumbo la Ekaristi Takatifu pamoja na Sakramenti ya Ndoa, pengine inayobeba uzito wa juu katika tafakari ya leo, kwa kuonesha kwa kina nafasi ya Bikira Maria katika maisha ya waamini.  "Hawana Divai" Ni maneno machache kutoka kwa Bikira Maria, lakini yanayonesha upendo na mshikamano, changamoto kwa waamini kumwalika Kristo katika maisha ya familia zao, divai ya furaha ya ndani, upendo, umoja, amani na mshikamano inapoanza kuwantindikia na matokeo yake kukukosana uaminifu, uvumilivu na subira katika maisha ya ndoa.

Mwinjili Yohane anasema Yesu anafunua utukufu wake katika tendo la kugeuza maji kuwa divai. Yohane analinganisha tendo hili na ukamilifu wa lengo la ujio wa Kristo – kufunua utukufu wa Mungu. Mwishoni wa Injili yake, Yohani anasema kuwa aliandika neno hilo yaani injili, ili watu wapate kuamini – Yoh. 20:20. Mwanzo wa ukamilifu wa lengo hilo ulionekana tayari pale Kana. Yohani anajua wazi kuwa tendo hili la kujifunua lilikamilika pia katika tendo la kujitoa msalabani, pale roho alitolewa – Yoh. 20:22. Tunaona kuwa katika tendo la Kana Yesu anamwambia mama yake saa yangu haijatimia. Saa ya Yesu kadiri ya Yohani ilitimia ule muda kwa kutukuzwa Msalabani na katika ufufuko. Ni saa ambayo amewavuta wote kwake – Yoh. 12:32.  Ni ile saa alipotoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba – Yoh. 13:1. Kile kilichofanyika pale Kana kilikuwa ni mwanzo wa kuonekana kwa utukufu wake hadharani. Pale Kana, Yesu alifunua utukufu wake, wafuasi wake walimwamini na Bikira Maria anakuwa mama mshindi dhidi ya shetani.

Kwa namna ya pekee, tunaona katika somo hili la Injili ufunuo wa utukufu wa Mungu. Somo hili laongea kuhusu ukamilifu wa ahadi ya Mungu. Mungu amekamilika katika yote. Na ukamilifu wetu ni kushiriki katika huo mpango wa Mungu wa ukombozi. Mt. Fransis wa Assisi anatambua wazi mpango huu wa Mungu na anatamka wazi akisema ‘Ee Mungu unifanye niwe chombo chako cha amani, upendo, huruma, upatanisho’ n.k. Mtakatifu huyu anakabidhi maisha yake yote kwa Mungu. Anajiweka huru kuwa chombo chake Mungu.

Mwinjili Yohane anamtaja Bikira Maria mara mbili katika Injili yake. Kwanza katika harusi ya Kana na mara ya pili pale msalabani. Yohani apenda kuonesha jinsi mama Maria alivyoshiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi pamoja na mwanawe. Neno la Mungu siku ya leo, latupa changamoto juu ya namna ya kushiriki utukufu wa Mungu. Somo la pili toka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho watosha kuonesha au kutukumbusha kuwa vipaji alivyotujalia Mungu, vyatosha kufanya miujiza. Hatuna budi nasi pia kuangalia matumizi ya vipaji hivyo. Kwanza kila mmoja wetu hana budi kutambua vipaji alivyo navyo na pili kuangalia matumizi yake.

Mtoto mmoja alimwomba baba yake amsimulie hadithi nzuri. Baba yake alikuwa anahangaika sana kuitunza familia yake. Kwa hakika hakuwa na muda wa kukaa na familia yake. Mahangaiko yake yakawa ni kupata chakula n.k. ili familia yake ikae vizuri. Huku akidhani kuwa amefanya tendo zuri kwa mwanae, akamnunulia kompyuta nzuri sana na CD nyingi na nzuri zenye hadithi nzuri za watoto. Lakina hata baada ya kufanya hayo yote akaona bado mtoto wake hana furaha. Baba yake akamwuliza kulikoni. Mtoto akamwambia ni sawa baba, umeninunulia kompyuta nzuri na CD nzuri, lakini wakati nasikiliza hizo hadithi, kompyuta hii haiwezi kunipakata kwa mikono kama ambavyo ungefanya wewe.

Ndugu zangu hatuna budi kujiuliza ni kwa namna gani tunatumia vipaji vyetu na uwezo wetu kwa faida ya wengine. Pengine neno la Mungu siku ya leo litupe changamoto juu ya namna tunavyotumia vipaji vyetu. Tunaka miiujiza? Basi tuwajali wengine na tuwapatie mambo matakatifu. Katika masomo yetu ya leo tumeona kuwa ahadi ya Mungu ni kamilifu – somo la kwanza. Katika somo la pili tumeona kuwa vipaji alivyotujalia Mwenyezi Mungu vinatosha kufanya miujiza na katika Injili tumeona habari juu ya ufunuo wa Mungu na uweza wake. Pale Kana Yesu anafunua utukufu wake, wafuasi wanamwamini na Bikira Maria anakuwa mama wa ushindi dhidi ya shetani. Hatuna budi kujitoa kwa ajili ya wengine. Na hii itawezekana tu kama tutakaa na Bwana kama Mama Maria alivyofanya, kuyasikiliza mahitaji na mahangaiko yao na kuyapeleka kwa Yesu. Tukimtumainia Mungu hatutaaibika millele. Somo la kwanza linatuambia kuwa ahadi ya Mungu ni kamilifu na timilifu.

Hatuna budi kujiuliza wakati wetu huu au katika mazingira yetu haya watu wanahitaji kitu gani? Ni divai ipi iliyo nzuri zaidi? Divai hiyo ni ipi? Yule baba alimpatia mwanae kompyuta wakati mtoto hakuwa anahitaji kompyuta. Kumbe mtoto alihaji kubebwa mikononi na baba yake. Je Mungu amekupatia kitu gani na umeshirikishaje wengine. Je unakitambua kipaji hicho, umekitoa au umekificha sababu ya ubinafsi au uchoyo? Pengine tunataka kufanya miujiza bila kuwa na Bwana wa miujiza. Haitawezekana.

Biblia inaeleza miujiza kama tukio lililosababishwa na kuingilia kati kwa pekee kwa Mungu, halifuati sheria za maumbile na huleta ujumbe kwa watu waishio sasa na wale wajao – Kut. 4:4-5 ‘ Bwana akamwambia; haya nyosha mkono wako umkamate mkia. Akanyosha mkono, akamkamata, nyoka akageuka tena kuwa fimbo mkononi mwake’. Miujiza ni ishara za wokovu na zinazoleta ufunuo kutoka kwa Mungu. Miujiza ya Yesu ilifungamana na utangazaji wake wa ufalme wa mwisho wa Mungu – Mt. 4:23 … ‘alizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao na kuitangaza injili ya ufalme. Akaponya kila ugonjwa na maradhi katika watu’. Petro na Paulo wanakishudhudia kipaji cha namna hiyo hiyo kutoka kwa Mungu – Mdo. 3:1-11 – uponyaji katika jina la Yesu … Petro akasema, fedha na dhahabu mimi sina, lakini niliyonayo ninakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, inuka na tembea….’.

Tutafakari sana leo ufahamu wetu wa mapenzi ya Mungu kwetu na tutende kama Bwana alivyotenda. Hakuna muujiza mwingine zaidi ya kukaa na Bwana wa Uzima, yaani Yesu Kristo Bwana Wetu. Kama tunataka kutenda miujiza hatuna budi kukaa na Bwana wa uzima. Tukifanya hivyo hatutatindikiwa na divai iliyo bora na nzuri na tutatenda miujiza mingi.

Tumsifu Yesu Kristo.

15 January 2019, 15:41