Tafuta

Vatican News
Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza kuwasili nchini Panama kushiriki maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019 Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameanza kuwasili nchini Panama kushiriki maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani 2019  (ANSA)

Siku ya XXXIV Vijana Duniani 2019: Vijana waanza kuingia Panama!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio muhimu sana, linaloacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za vijana wengi wanaohudhuria. Hili ni jukwaa lenye utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Hiki ni kipindi cha neema na changamoto kwa vijana kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano, tunza na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya, ili waweze kukita maisha yao katika imani, udugu na mapendo.

Makundi ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa sasa yanaelekea nchini Panama, tayari kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, moto wa kuotea mbali katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya! Vijana wanajiandaa kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko atakapowasili nchini Panama hapo tarehe 23 Januari 2019. Katika maadhimisho haya, vijana watajisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa ya Mungu inayowajibika kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Vijana wamebeba zawadi mbali mbali watakazowaachia waamini na watu wote wenye mapenzi mema watakaowakaribisha kwenye makazi yao wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Pengine, vijana wengi wangetamani kuhudhuria kwenye maadhimisho haya, lakini kutokana na kubanwa na mitihani, wataendelea kuwasindikiza vijana wenzao kwa njia ya sala, sadaka pamoja na kufuatilia matukio yote haya kwenye vyombo vya mawasiliano na mitandao ya jamii. Vijana wamekuwa na maandalizi mbali mbali katika majimbo na nchi wanakotoka, ili kweli tukio hili liweze kuacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya.

Takwimu zinaonesha kwamba, vijana 13, 500 kutoka Poland, wakiwa wanasindikizwa na Mapadre 200, kati yao Mapadre wa Jimbo ni 20 pamoja na watu wa kujitolea 300, wengi wao wakiwa ni kwa ajili ya huduma ya kwanza, tayari “wametinga timu” nchini Panama. Hili ni kati ya makundi makubwa ya vijana kutoka Barani Ulaya yanayoshiriki Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama. Kuna Maaskofu 12 wanaoongozwa na Askofu mkuu Wojciech Polak, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland.

Italia inawakilishwa na vijana 900 chini ya uongozi wa Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio muhimu sana, linaloacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za vijana wengi wanaohudhuria. Hili ni jukwaa lenye utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Hiki ni kipindi cha neema na changamoto kwa vijana kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili duniani, tayari kushiriki katika ujenzi wa utamaduni wa haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu licha ya tofauti zao msingi.

Siku ya Vijana Panama 2019

 

15 January 2019, 08:36