Tafuta

Vatican News
Patriaki Cyrill wa Moscow na Urussi nzima asema, amani ya kweli inapata chimbuko lake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu! Patriaki Cyrill wa Moscow na Urussi nzima asema, amani ya kweli inapata chimbuko lake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu!  (AFP or licensors)

Patriaki Cyrill wa Moscow na Urussi: Ujumbe wa Noeli kwa 2019

Patriaki Cyrill katika ujumbe huu amekazia zaidi umuhimu wa amani inayobubujika kutoka katika undani wa moyo wa mtu; wito na dhamana ya Wakristo katika ulimwengu mamboleo na kwamba, Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani na furaha kwa watu wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Upendo na huruma ya Mungu vimefunuliwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa Mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwakirimia amani ya kweli. Lakini kwa bahati mbaya, amani hii bado inakumbana na kizingiti cha vita, machafuko na mipasuko ya kijamii! Hiki ni kiini cha ujumbe wa Noeli kutoka kwa Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urussi nzima katika maadhimisho ya Noeli kwa Mwaka 2019 ambayo kwa mujibu wa Kalenda ya Juliani, maadhimisho haya yamefanyika hapo tarehe 7 Januari 2019.

Patriaki Cyrill katika ujumbe huu amekazia zaidi umuhimu wa amani inayobubujika kutoka katika undani wa moyo wa mtu; wito na dhamana ya Wakristo katika ulimwengu mamboleo na kwamba, Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani duniani. Wito wa Wakristo unafumbatwa katika utukufu wa ufunuo wa Mwana wa Mungu, changamoto na mwaliko kwa waamini kukataa kishawishi cha kumezwa na malimwengu, kwa kujivika silaha za mwanga tayari kumwendea Kristo Yesu kwa nyimbo za furaha, ili hatimaye, furaha hii iweze pia kumwilishwa katika maisha ya watu wengi, hasa wale wanaoteseka zaidi sehemu mbali mbali za dunia.

Katika mkesha wa Noeli, Patriaki Cyrill, amewataka waamini kuimarisha fadhila ya imani, matumaini na mapendo kama njia ya kuzama katika Fumbo la Umwilisho, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu alidhihirishwa katika mwili, akajulikana kuwa na haki katika roho; akaonekana na Malaika, akahubiriwa katika mataifa, akaaminiwa katika ulimwengu na akachukuliwa juu katika utukufu. Amani ya Kristo inaweza kudumu katika moyo wa mwamini, ikiwa kama, atashika Amri za Mungu na kuzimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Amani ya kweli ni kiungo na daraja linalowaunganisha waamini na Mwenyezi Mungu.

Upendo wa Mungu unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama alivyofanya Mwenyezi Mungu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ambalo linapenyeza upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Upendo na huruma ya Mungu iwaguse maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama ilivyokuwa kwa kwa Kristo Yesu, kuzaliwa katika Pango la kulishia wanyama na wachungaji kondeni, wakawa ni mashuhuda wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu.

Mwanga angavu na utukufu wa Mwana wa Mungu ukawafikia hata Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, ili kwenda kumtafuta Mfalme aliyezaliwa na hatimaye, kumpatia zawadi zao yaani: wanaleta manemane, dhahabu na uvumba, zinaonesha: Umungu wake, Ubinadamu; Sadaka ya mateso hadi kifo chake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu! Zawadi zote hizi zinafumbata kwa namna ya pekee, Fumbo la Umwilisho wa Mwana wa Mungu, pengine kwa macho ya kibinadamu si rahisi sana kuweza kulielewa, lakini, ikumbukwe kwamba, binadamu ameshirikishwa upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifi. Ukuu na utukufu wa Mungu umefumbatwa katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.

Noeli Urussi 2019

 

 

08 January 2019, 14:47