Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Panama 2019 ni uamuzi wa busara ya kichungaji: hata watoto wa maskini wanashiriki kikamilifu! Maadhimisho ya Siku ya Vijana Panama 2019 ni uamuzi wa busara ya kichungaji: hata watoto wa maskini wanashiriki kikamilifu!  (AFP or licensors)

Panama 2019: Hata watoto wa maskini wameshiriki kikamilifu!

Kwa uamuzi huu wa kichungaji, vijana wengi kutoka Amerika ya Kusini ambao kimsingi wanaogelea katika umaskini mkubwa wameweza kushiriki kwa kukutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kushirikishana ndoto, miradi na changamoto za maisha, ili hatimaye, waweze kugundua kwamba, wao ndio wadau wakuu wa mageuzi na upyaisho wa Kanisa na Jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu José Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, 24 Januari 2019 ili kufungua rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, alimshukuru kwa uwepo wake, ambao unapania kuimarisha imani ya vijana kwa Kristo Yesu ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima. Maaskofu Katoliki Panama wanamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuchagua Panama kuwa ni kitovu cha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Kwa uamuzi huu wa kichungaji, vijana wengi kutoka Amerika ya Kusini ambao kimsingi wanaogelea katika umaskini mkubwa wameweza kushiriki kwa kukutana na vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kushirikishana ndoto, miradi na changamoto za maisha, ili hatimaye, waweze kugundua kwamba, wao ndio wadau wakuu wa mageuzi na upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ya Mungu nchini Panama imemkaribisha Baba Mtakatifu kwa mshangao na heshima kubwa. Uwepo wake, miongoni mwao unatajirishwa na furaha ya watu wa Mungu yaani: wakleri, watawa, lakini zaidi waamini walei ambao ni nguzo msingi ya maisha na utume wa Kanisa nchini Panama.

Katika mkesha huo wa ufunguzi, Askofu mkuu José Domingo Ulloa Mendieta aliwatambulisha watakatifu walinzi na wasimamizi wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Wengi wao ni wale wanaotoka Amerika ya Kusini yaani: Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero, kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wake kiasi cha kuyasadaka maisha haya kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Awe ni mfano kwa vijana wanaotembea katika Njia ya Msalaba huku wakiwa makini katika maisha na wakiwa wanaangaziwa na mwanga wau pendo wa Bikira Maria.

Wengine ni Mtakatifu Rosa wa Lima, mtu wa sala; Yohane Bosco, baba na mwalimu wa vijana. Wametambulishwa pia Mtakatifu Yohane Paulo II aliyefanikiwa kuwaonesha vijana Uso wa Kristo mwingi wa huruma na mapendo na mwishoni ni Mtakatifu Juan Diego, muasisi wa Ibada ya Bikira Maria, chemchemi ya furaha ya uinjilishaji.

Jimbo kuu la Panama
26 January 2019, 12:26